Utamchukia kwa uvaaji wake AU pale unaposikia katoka na vidosho Lakini usiku wa jana ungempenda bure hasa anapofunga goli namzungumzia Mario Balotelli ambae alipachika magoli mawili mazuri ambayo hayakuwa na ubishi wowote ule.Magoli yake yaliiwezesha Italia kuifunga timu iliyopewa chapuo ya kuingia Fainali Ujerumani kwa Magoli 2-1.Hivyo sasa kukutana uso kwa uso na Uhispania hiyo Jumapili katika Fainali ya EURO 2012 mjini Kiev.
Alipachika goli la kwanza kwa kichwa baada ya kupata krosi safi kutoka winga ya kushoto mpira uliopishana na Golikipa wa Ujerumani Neuer aliekuwa anaelekea upande wa kushoto na mpira kupigwa kulia kwake hivyo kujaa kwenye kamba.
Goli la pili alilifunga kwa kiki kali iliyomuacha golikipa Neuer hana la kufanya hivyo kuipatia Italia goli la pili aliloshangilia kwa kuvua jezi yake na kutunisha misuli kama baunsa.Kitendo cha kuvua jezi alizawadiwa kadi ya njano kwa kosa hilo.
Wajerumani walijitahidi kuwa makini lakini juhudi hizo hazikuzaa matunda kwani Italia ilionekana kuwazidi ujanja mara kwa mara .
Waliweza kupata goli la mkwaju wa penati dakika ya pili ya nyongeza goli lililowekwa nyavuni na Mesut Ozil
Italia imeweza kuendeleza rekodi yake ya kutoshindwa na Wajerumani kwenye mashindano makubwa hiyo ikiwa ni muendelezo wa mapambano yasiyopungua nane dhidi ya wajerumani hao na zote hizo wakiwashinda hivyo kuendeleza uteja wao.
Hii sasa itakuwa mara ya tatu kwa Italia kuingia fainali za michuano hii ya mataifa ya Ulaya, na wataingia fainali kama timu inayodhaniwa kuwa dhaifu ikilinganishwa na mabingwa watetezi Uhispania.
Meneja wa Italia Cesare Prandeli anasema timu yake ilistahili ushindi kwa kupamabana walikoonyesha wachezaji wake kwa kufunga mabao ya mapema hivyo kuwanyima fursa wajerumani kutamba tena.
''Azzurri'' kama wanavyojulikana walicheza kwa tahadhari kubwa baada ya mabao hayo ili kuwazuia vijana wa Ujerumani wasiweze kupata bao kwani waliogopa kuacha ngome yao wazi pamoja na hayo Wajerumani walishindwa kuzitumia vizuri nafasi chache walizopata katika mchezo huo ambapo mara kadhaa golikipa wa Italia aliweza kucheza uzuri mashambulizi ya Wajerumani hao.
Post a Comment