• Fedha za mafisadi zawatokea puani wabunge
BUNGE jana liliwaka moto baada ya baadhi ya wabunge kuwanyooshea vidole wenzao kwa madai kupokea rushwa kwa lengo la kuwapigia debe mafisadi wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) wanaowafilisi Watanzania.
Wabunge hao wanadaiwa kuwaunga mkono mafisadi ili Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, na Katibu Mkuu wake, Eliakimu Maswi, waonekane hawafai.
Akichangia mjadala wa hotuba ya bajeti kwa wizara hiyo jana, Mbunge wa Rombo, Joseph Selasini (CHADEMA), alisema kwa wiki nzima waziri na watendaji wake walikuwa wakidhalilishwa na baadhi ya watu kwa kupitia wabunge wakitaka Rais Jakaya Kikwete awaondoe kwa madai kuwa walikiuka sheria ya manunuzi ya umma na kuipa zabuni kampuni ya PUMA Energy.
“Mheshimiwa mwenyekiti baadhi ya makampuni ya mafuta yalikuwa hapa Dodoma na kutoa chochote kwa wabunge na hili si kwa upande wa serikali ya CCM bali wabunge wa pande zote tukiwemo wapinzani. Msione watu wanazungumza kwa nguvu hapa kutetea, hawa wamepewa chochote,” alisema.
Huku akishangiliwa na karibu wabunge wote, Selasiani alisema wanaohoji kuwepo ukiukwaji wa sheria ya manunuzi ya umma anawashangaa kwani katika jambo la msingi lazima uamuzi uwe mgumu huku akitolea mfano wa Yesu Kristo alivyoivunja Sabato aliyoiweka mwenyewe.
“Mheshimiwa mwenyekiti Maswi ametishwa tunajua hilo, ametumiwa meseji za vitisho, ameombwa rushwa na baadhi ya wabunge wenzetu hapa. Tunawajua wako wabunge wanafanya biashara na TANESCO, lakini humu waongea kwa nguvu na jazba wakijifanya watetezi wa wananchi kumbe ni nguvu ya rushwa,” alisema.
Selasini alimtadharisha Waziri Muhongo kuwa yeye ni msomi asiyetokana na siasa hivyo hawajui wanasiasa lakini ni vema afanye kazi kwa nguvu bila kutetereka na atawazoea.
Mbunge huyo pia alipendekeza sheria ya wahujumu uchumi irejeshwe ili wahusika wakiwemo wabunge waliohusika katika sakata hilo wahukumiwe kama wahaini.
“Wako wenzetu humu wamekuwa wakijifanya wapambanaji wanaongea kwa nguvu kuhusu ufisadi lakini leo wamekuwa madalali wa mafisadi na hawa wako kote CCM na huku kwetu wapinzani,” alisema.
Selasini alizungumza baada ya kutanguliwa na wabunge wenzake, Anne Killango Malecela wa Same Mashariki na Christopher Ole Sendeka wa Simanjiro (CCM), ambao walionekana kupishana katika kuwaunga mkono waziri na watendaji wake.
Licha ya kuwapongeza waziri na watendaji wake, Ole Sendeka alisema anapaswa kuwaeleza wananchi hali iliyopo ili mambo yakiharibika wasimshangae.
Alisema mitambo inayotumika kuzalisha umeme sasa ni ya kampuni binafsi inayoiuzia TANESCO uniti moja kwa dola senti 23 halafu shirika hilo linauza kwa dola senti 12 ambayo ni hasara ya dola senti 11.
“Hii ni mikakati ya kifisadi kwenye sekta ya gesi kwani kampuni za Songas zinauziwa gesi kwa bei ya kutupwa ndiyo maana wanaweza kuuza umeme wao kwa bei nafuu.
Sendeka alitaka kamati itakayoundwa kumchunguza Mkurugenzi wa TANESCO, William Mhando, iwachunguze pia na watendaji waliotoa zabuni za mafuta kinyume na sheria ya manunuzi kwa kisingizio cha bei nafuu ili wachukuliwe hatua.
Naye Kilango pamoja na kutumia muda mwingi kumsifu Maswi, lakini alipingana na Sendeka akisema kuwa hakuna sheria ya manunuzi iliyokiukwa na vile vile akatumia muda huo kumpongeza msemaji mkuu wa kambi rasmi ya upinzani kwa wizara hiyo, John Mnyika kwa hotuba yake.
Kilango aliyeonekana kuzunguka ukumbini na kuteta na Waziri Muhongo wakati wa asubuhi akiwa na kitabu cha hotuba ya upinzani, alisema kuwa amempongeza msemaji wa upinzani kwa vile masuala mengi ya ufisadi wa TANESCO aliyoyasema ni ya CCM waliyoyasema juzi kwenye kamati yao ya chama.
“ Tarehe 25 usiku kuanzia saa 3 mpaka 6 wabunge wa CCM tukutana na tukawa na mazungumzo marefu hivyo napongeza msemaji wa upinzani kwa vile yale aliyosema ukurasa wa 10 mpaka 16 ndiyo yale tuliyojadili kwa kirefu naona waliyapatapata,” alisema Kilango.
Mbunge wa Mwibara, Kangi Lugora alikuwa kivutio pale alipoomba aruhusiwe kwenda mbele ya wabunge kuwaonyesha jinsi Bunge lilivyoweza kusigina mirija yote ya mafisadi ndani ya TANESCO na hivyo kuwafanya wabunge kuangua kicheko na vigelegele.
Alihoji walikuwa wapi wale wanaosema kanuni za manunuzi ya umma zimekiukwa, kwamba mbona hawakujitokeza wakati nchi ikiwa gizani. Alishangaa watu kumsakama Maswi na wenzake wakati aliokoa fedha ambayo itasaidia kununulia dawa hospitalini, madawati, vitabu na huduma nyingine.
Lugora ambaye alikuwa akishangiliwa kwa nguvu, alifafanua kuwa kwa mujibu wa mkataba ni kwamba mwenye mamlaka ya kuwanunulia mafuta IPTL ni Wizara ya Nishati na Madini wala si TANESCO.
Alisema kuwa Bunge hilo halitaki na wala halitakubali kutumika kama kichochoro cha mafisadi, hivyo waazimie kwa kauli moja kwamba waziri awaeleze kuwa hakutakuwa na mgawo wa umeme tena. Hivyo kauli za kwamba nchi haitawaliki ni za kifisadi zinazoratibiwa na wale wanaozima mitambo ili kutengeneza mgawo.
Lugora alitaka Mhando achukuliwe hatua kuanzia leo kwa kutumia madaraka vibaya kwa kumpatia mkopo mkewe Eva wakati taratibu nyingine za kuchunguzwa kwa tuhuma nyingine pamoja na wenzake zikiendelea.
Naye mbunge wa Kigoma Kusini (NCCR-Mageuzi), David Kafulila, aliibua tafrani wakati akichangia pale aliposema kuwa nchi imebakwa kutokana na serikali kufa ganzi, kauli iliyopingwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera na Uratibu), William Lukuvi, ambaye aliomba mwongozo wa kiti akidai mbunge huyo ametukana.
Hata hivyo iliwachukuwa muda kufikia muafaka baada ya Kafulila kugoma kufuta kauli hiyo alipotakiwa kufanya hivyo na Mwenyekiti wa Bunge, Mussa Zungu, akidai kuwa kwao Kigoma kubaka si matusi kwani wanabaka hata panzi.
Zungu alitumia burasa sana kumsihi Kafulila afute kauli hiyo lakini mwishowe alisimama na kusema kuwa analazimika kufanya hivyo kwa matakwa ya mwenyekiti na ndipo akaruhusiwa kuchangia.
Katika mchango wake alisema kuwa hakuna namna yoyote nchi inaweza kufikia mapinduzi ya viwanda bila kuwa na nishati ya umeme wa uhakika huku akitolea mfano nchi ya Malysia iliyokuwa na tatizo la nishati hiyo mwaka 1994 kama Tanzania.
“Wenzetu baada ya hapo walitafuta ufumbuzi wa kudumu na hivyo kuzalisha umeme wa megawati 10,000 wakati sisi tulikimbilia kwenye umeme wa dharura kwa kampuni binafsi ya APTL na leo tunazalisha megawati 1,000.
Chanzo:Tanzania Daima
Post a Comment