Featured

    Featured Posts

    Social Icons

Loading...

KUUA AMA KUUA BILA KUKUSUDIA: UCHAMBUZI MFUPI (TUMEICHAPISHA TENA KUTOKANA NA MAOMBI YA WADAU)



KUUA AMA KUUA BILA KUKUSUDIA: UCHAMBUZI MFUPI

Salaam kwa wote.

Nimeonelea kutoa uchambuzi mfupi wa kawaida kuhusu jambo nililolitaja hapo juu. Uchambuzi huu unatokana na kubaini kwamba watu wengi nilioongea nao hapa na pale juu ya kuua na kuua bila kukusudia,wameonesha kuchanganyikiwa na maana halisi ya makosa hayo mawili.


Nikiri kwamba eneo hili ni gumu sana hasa kwa mtu wa kawaida ambaye hajapitia taaluma ya sheria. Ni mahala panapohitaji umakini wa hali ya juu ili kuweza kuelewa juu ya maana halisi ya
makosa hayo mawili.Napenda nitoe angalizo kuwa katika uchambuzi huu sitapenda kunukuu vifungu vya sheria kwa kirefu sana ili kurahisisha uchambuzi wangu kwa wasomaji wa kawaida. Ila ifahamike kuwa sheria ya msingi inayoongoza makosa haya mawili ni Sheria ya Kanuni ya Adhabu, Sura ya 16 ya Sheria za Tanzania.


Kwa ujumla, Kuua na Kuua bila ya kukusudia ni makosa ambayo mtu huyatenda dhidi ya mtu mwingine ambayo huhesabika ni kutenda kosa dhidi ya dola.Makosa haya yanatofautiana na makundi mengi sana kama vile makosa dhidi ya vitu,na migawanyo mingine.Sasa haya makosa ya Kuua na Kuua bila ya kukusudia, ni makosa yaliyowekwa chini ya makosa dhidi ya binadamu. Bila shaka ni kwa mujibu wa Kanuni ya Adhabu ya Tanzania.(Kanuni ya adhabu ni mwongozo unaoelezea makosa mbalimbali katika Tanzania huku ikieleza adhabu inayopaswa kutolewa kwa mtu atakayekutwa na hatia katika kosa aliloshitakiwa nalo).


Labda utajiuliza ni kwa nini tuna hiyo Sheria ya Kanuni ya Adhabu. Ndiyo, Kanuni ya Adhabu ndiyo inayoainisha ni matendo gani yanayojenga kosa fulani na kwamba kosa hilo likithibitishwa pasi na shaka yoyote mahakamani,basi aliyetenda kosa hilo ataadhibiwa adhabu fulani. Tambueni kwamba Sheria ya Kanuni ya Adhabu inaainisha makosa ya Jinai tu ambayo dola ndiyo inayoyasimamia.Ndio maana tunasema makosa ya jinai ni makosa yanayofanywa na watu dhidi ya dola.Hii ni tofauti na mashauri ya madai ambayo huwa ni kati ya mtu na mtu mwingine. Dhana hii ni ngumu kidogo,iweje ameuliwa Stewart kisha pasemwe kwamba dola ndiyo iliyokosewa?Ndiyo,kwa maana dola ndiyo yenye jukumu la kulinda maisha ya watu wake na mali zao ndiyo maana ikaweka misingi ya kisheria na kueleza mkururo wa makosa na adhabu zake ili wenye kuogopa waogope kufanya makosa lakini almuhimu maisha ya watu na mali zao viwe salama salimini.


Kwa kukuweka sawa zaidi, ndio maana utaona kwamba dola huwa haiingilii kati makosa yetu tunayotendeana sisi kwa sisi kama vile kudaiana,mikataba halali iliyoparaganyika na mambo mengine kama hayo.Tukifanyiana makosa hayo,sisi wenyewe ndio tunaiomba mahakama (mhimili mwingine wa dola) itusaidie kutatua tatizo hilo kwani ni tatizo lililoibuka kati ya mtu na mtu au mtu na kikundi au kikundi na kikundi.Tena huwa tunaanzia mbaaali saaana kabla ya kufika mahakamani.Lakini kwenye makosa ya jinai, aa,hakuna sumile,ukituhumiwa tu kutenda kosa fulani,utakamatwa, utafunguliwa mashitaka,utafikishwa mahakamani,kesi itasomwa na kusikilizwa na mwisho hukumu itatolewa.Labda mtenda kosa aamue kujificha na asijulikane kamwe hadi mwisho wa maisha yake.Lakini bado katika mazingira fulani shauri dhidi yake laweza kuendeshwa pasipo yeye kuwepo mahakamani.

Bila shaka tunakwenda pamoja.

Sasa hayo makosa mawili niliyoyataja hapo juu (Kuua na Kuua bila ya kukusudia) pia ni katika makosa ya jinai ambapo mtu yoyote atakayetuhumiwa kuyakatisha maisha ya mtu mwingine, dola itamkamata,itamweka rumande,itamfungulia mashitaka na mwisho hukumu kutolewa.

KUUA
Kosa hili limeainishwa katika fungu la 196 la Kanuni ya Adhabu, Sura ya 16.Mtu atasemekana kuwa ametenda kosa la kuua pale itakapobainika pasi na shaka yoyote kwamba mtu huyo alidhamiria kukatisha maisha ya mtu mwingine.Mbinu nyingi zinaweza kutumika katika kufikia malengo hayo.Mtu anaweza akajipanga mwenyewe na kumuwinda adui yake hadi akapata nafasi nzuri na kutimiza lengo lake la mauaji.Anaweza mtu akatumia silaha kama bunduki, kisu, panga, gongo na vitu vingine kama hivyo.Mwingine anaweza akamtumia mtu mwingine kutekeleza azma yake. Bila shaka ni kwa makubaliano maalum.Pia mtu anaweza akatumia kikundi cha watu katika kufkia lengo hilo.Anaweza pia akatumia kikundi cha wataalamu wenye uwezo wa kutotumia panga wala bunduki,lakini wakatumia mbinu za kitaalamu kama vile matumizi ya sumu na tindikali kwa lengo hilo hilo la kuondoa maisha ya mtu.Alimuradi njia kadhaa zinaweza zikatumika.

Adhabu ya kosa hilo litakapothibiti, ni kunyongwa hadi kufa.

KUUA BILA YA KUKUSUDIA.
Kosa hili limeainishwa katika fungu la 195 la Sheria ya Kanuni ya Adhabu, Sura ya 16.Mtu atasemekana kuwa ametenda kosa la Kuua bila ya kukusudia pale itakapobainika kuwa amekatisha maisha ya mtu bila ya kuwa na dhamira ya kufanya hivyo.Kwa maana nyingine, mauaji yamefanywa bila ya dhamira iliyoratibiwa kikamilifu ili kutenda kosa la mauaji.Hapa napo ni pagumu maana unaweza ukajiuliza ni kwa namna gani tunaweza tukatambua kuwa mtuhumiwa au mshitakiwa ameuwa bila ya dhamira au kukusudia kuua?

Kwa maswali hayo, tunarudi kulekule ambako inabidi wataalamu waangalie mazingira halisi ya tukio lenyewe namna lilivyotokea.Pia wapelelezi ni budi wafanye uchunguzi wa kina ili kujiridhisha kuwa ni kwa namna gani mtuhumiwa anaweza akawa kweli ameua bila ya kukusudia.Lakini ikumbukwe pia kwamba ni mahakama ndiyo itakayotoa tamko kwamba huyo mtuhumiwa ni kweli ametenda kosa hilo la kuua bila ya kukusudia.Nisisitize tena kwamba ni jukumu la upande wa mashitaka kukusanya ushahidi wenye mashiko ambao utairidhisha mahakama kwamba kweli mtuhumiwa ametenda kosa hilo.Pale upande wa mashitaka utakapo wasilisha ushahidi dhaifu mbele ya mahakama, basi mtuhumiwa ataachiliwa huru.

Pale itakapothibitika kwamba mtuhumiwa kweli ametenda kosa hilo la kuua bila ya kukusudia, ukomo wa juu wa adhabu yake huwa ni kufungwa maisha.Adhabu ndogo itategemea ni kwa namna gani mtuhumiwa atakavyo jitetea na ni kwa namna gani mahakama itakavyopokea maombi ya mtuhumiwa huyo na namna shauri zima lilivyoendeshwa.Adhabu hiyo inaweza ikapunguzwa.

Labda ungependa kujua sasa ni kwa namna gani mahakama inaweza ikafikia uamuzi wa kumtia hatiani mshitakiwa wa kosa la Kuua bila ya kukusudia.Hapa kuna mambo mengi, lakini cha msingi ni kuangalia na kujiridhisha bila ya shaka yoyote kuhusu namna tukio lenyewe lilivyotokea.Kwa mfano dereva aliyeingiza gari yake kwa ghafla mbele ya gari lingine na kusababisha gari la nyuma yake kuligonga na mara madereva hao wakaacha sukani zao na kuanza kubishana na kutukanana na kutahamaki wakarukiana maungoni huku mmoja akimsukuma mwenziwe kwa nguvu hadi chini na kufa papo hapo,utaona kuwa hapa hakuna aliyekuwa na dhamira ya kuua isipokuwa hali ya ghadhabu na mihemko ya mishipa ya hasira kali zimepelekea hali ya kifo.Hivyo kwa namna yoyote ile itachukuliwa kuwa aliyeua ameuwa bila ya kukusudia.

Pia chukua mfano wa kero ndogo ya nyumbani iliyopelekea mke kukasirika ghafla na kumsukuma mume hadi kuangukia kwenye ncha ya meza ya kioo iliyokuwa chumbani sababu iliyopelekea mume huyo kufariki dunia.Ni dhahiri kabisa kosa hilo litajumuishwa kuwa ni Kuua bila ya kukusudia.Lakini ifahamike kwamba ili kufukia maamuzi hayo, mahakama ni lazima iwe imesikiliza kwa makini mkusanyiko wa mambo mengi yaliyoelezwa mahakamani hapo na upande wa mashitaka na ule wa utetezi.

Mnaweza mkatafakari pia inakuwaje kwa mtu aliyelewa chakari kisha akafanya jambo bila ya kujifahamu na kusababisha kifo cha mtu mwingine.Kama itathibitika kwamba mtuhumiwa alikuwa amelewa chakari kiasi ya kutojitambua ni kitu gani alichokuwa anafanya,basi anaweza akaadhibiwa kwa kosa la kuua bila ya kukusudia.

Kwa upande mwingine,Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai ya mwaka 1985,imetoa pia haki ya mtuhumiwa wa kosa la mauaji ya bila kukusudia kuomba dhamana ili awe nje ya kizuizi akisubiri kuendelea kusikilizwa kwa shauri lake hadi kutolewa hukumu.Maombi ya dhamana yatawasilishwa mahakamani na upande wa utetezi na pindi mahakama itakaporidhika na maombi hayo itatoa dhamana kwa mshitakiwa bila shaka dhamana hiyo itakwenda sawia na masharti kadhaa.Mshitakiwa atakapotimiza masharti hayo ya dhamana ataachiliwa huru kwa muda kama nilivyoeleza hapo juu.

Mwisho
Ni imani yangu kuwa sasa wale waliokuwa wanapata shida ya kutofautisha makosa haya mawili, watakuwa wamepata uwelewa mpana zaidi. Kumbuka kwamba ni mambo ya kiufundi zaidi yanayoangaliwa katika kumshitaki mtu aidha kwa kosa la Kuua au Kuua bila ya kukusudia. Lakini kumbukeni kwamba kuna dhana moja kongwe katika sheria isemayo “kila mtu ni mwema
mbele ya sheria hadi pale mahakama itakapo mtia hatiani”.Maana yake ni kwamba watu wote wanaotuhumiwa na makosa mbalimbali,bado wanatakiwa wahesabiwe kuwa ni watu wema kana kwamba hakuna tuhuma yoyote juu yao hadi pale mahakama itakapotoa maamuzi juu ya tuhuma zinazowakabili.

Nikipata nafasi katika katika siku zijazo kupitia uwanja huu, ninaweza nikafanyia uchambuzi wa kina juu ya suala la dhamana.Nini maana ya dhamana,nani anapaswa kupewa dhamana,ni nani
anayetoa dhamana na ni makosa yepi mtuhumiwa anaweza akapewa dhamana.Lakini je mtu anaweza akakataliwa dhamana hata kama kosa alilotenda linadhaminika?

Nawashukuruni na Allah awabariki.

Imetayarishwa na:

Ndugu Maulana Ayoub Ali
Kitivo cha sheria,Chuo Kikuu Huria cha Tanzania
Makao Makuu,Dar Es salaam.
+255 713 046 591
libila@yahoo.com,maulana.ayoub@out.ac.tz
Imehaririwa na Ndugu,Alex B.Makulilo akiwa Ughaibuni,Ujarumani.
author

This post was written by: Author Name

Your description comes here!

Get Free Email Updates to your Inbox!

Post a Comment

CodeNirvana
Chediel . Powered by Blogger.
© Copyright Rundugai Blog
Back To Top