Baada ya kuisoma taarifa ile ambayo kiuhalisia kuna sehemu imepotoshwa kwa maana kwamba au ukweli wa mambo yalivyoendeshwa mpaka kufikia maamuzi unajaribu kufichwa, hasa kwenye kipengele cha uamuzi wa pingamizi la mchezaji Kelvin Yondani.
Kwa taarifa za uhakika nilizonazo ni kwamba kikao cha kamati ya Sheria, maadili na hadhi za wachezaji kilichokutana jana kilihudhuriwa na wajumbe watano Lloyd Nchunga, Iman Madega, Ismail Aden Rage, Omar Gumbo, Hussein Mwamba pamoja na Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mwanasheria Alex Mgongolwa.
Katika kikao hicho wajumbe walijadiliana katika kuweza kutatua na kupata suluhisho la mchezaji Kelvin Yondani ambaye amesajiliwa na vilabu viwili vikubwa vya Simba na Yanga lakini wakashindwa kupata muafaka kwa njia ya majadiliano, ndipo wakaamua kutumia njia ambayo ipo nje ya kanuni kwa kuamua kupiga kura miongoni mwa wajumbe. Kura zikapigwa huku Rage, Gumbo, na Mwamba wakipiga kura Yondani aidhinishwe Simba huku kura za Iman Madega, Nchunga, na Mwenyekiti Mgongolwa zikitaka mchezaji huyo aidhinishwe kucheza Yanga. Kwa maana hiyo matokeo ya kura yakashindwa kuamua kesi. Lakini kwa kuwa mwenyekiti ana mamlaka makubwa na uwezo wa kupiga kura ya Veto basi akachukua jukumu hilo na kupiga kura akimuidhinisha Yondani aende Yanga.
Kiuhalisia na namna ya demokrasia ilivyo mtu mmoja hawezi kupiga kura mara mbili kwenye ushindani mmoja kwa sababu kutakuwa hakuna usawa. Hivyo haikuwa sahihi kwa Mwenyekiti kupiga kura mara mbili.
Lakini kabla ya kufikia yote haya, hakuna utaratibu wowote duniani kwenye masuala ya usajili unaolekeza ikitokea hali kama iliyopo kwa Yondani basi zipigwe kura. Kiuhlasia ilibidi sheria zilizopo zenye kuamua kesi kama hiyo zifuatwe. Inajulikana wazi kwamba ni kosa kwa mchezaji kusaini mkataba na timu mbili tofauti kwa wakati mmoja na adhabu zake zimeanishwa kabisa kwa klabu iliyocheza rafu na mchezaji mwenyewe. Na katika sheria hizo hakuna mahala kunapoelekeza uwepo wa upigaji kura kuamua kesi ya namna ya Yondani au Twitte.
Sawa basi hata kama kamati iliamua kutumia mfumo wa upigaji kura basi ungepaswa kuwa na usawa na sio kama ilivyotendeka. Haiwezekani mtu mmoja ambaye tayari ameshaonyesha yupo upande mmoja kati pande mbili zinazopingana tena zenye wajumbe sawa apewe nafasi ya kupiga kura mbili.
Lakini haikutakiwa jambo hili lifike kwenye hatua hii - sheria ziliwekwa na shirikisho la soka chini ya muongozo wa kanuni zinazoongoza soka zilibidi zifuatwe katika uamuzi wa mapingamizi haya ili kuweza kukomesha vitendo vya namna ambavyo vinarudisha nyuma maendeleo ya soka letu.
Chanzo:Shaffih Dauda.
Post a Comment