Mbunge wa Nyamagana (Chadema), Hezekiah Wenje, jana aliuteka mkutano uliopangwa kuhutubiwa na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda ambapo wananchi waliohudhuria walimshangilia zaidi yeye (Wenje) huku wakinyoosha vidole viwili ambayo ni alama ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).
Hali hiyo ilijiri jana saa 11:00 baada ya msafara wa Waziri Mkuu kuingia katika viwanja vya Sahara huku Wenje akiwa miongoni mwa waliofuatana na Pinda.
Baada ya Pinda kuteremka kwenye gari na kuanza kuelekea kwenye meza kuu huku akisalimiana na baadhi ya wananchi, sehemu kubwa ya umati uliokuwepo walikuwa wakionyesha ishara ya vidole viwili na mara walipomuona Wenje walilipuka kwa shangwe ambapo Mbunge huyo machachari naye aliwanyooshea ishara ya vidole viwili.
Kama vile haitoshi baada ya Waziri Mkuu na viongozi wa mkoa wa Mwanza aliokuwa amefuatana nao kuketi vitini, ndipo Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, Baraka Konisaga, alisimama kwa ajili ya kufanya utambulisho na alianza kwa kumweleza Pinda kuwa hizo ndizo harakati za miji mikubwa.
Wakati Konisaga akisema hivyo, wananchi waliendelea kushangilia, hali iliyomfanya adai kuwa wanamshangilia yeye (Konisaga) kwa sababu ndiye mtawala wa eneo hilo, lakini wananchi walionekana kuguna kwa sauti kama ishara ya kutokubaliana naye.
“Hayo makofi mnanishangilia mimi, kwa sababu bila mimi hakuna mkutano,” alisema Konisaga na kupokelewa na sauti za wananchi walionekana kupingana naye wakisema weweeee! Katika utambulisho, Konisaga alianza kwa kumtambulisha Mkurugenzi wa Jiji la Mwanza, Wilson Kabwe, lakini wananchi walionekana kupinga hatua hiyo ndipo Konisaga akawaambia bila yeye (Kabwe) hakuna maendeleo Mwanza.
Hatimaye Konisaga alimtambulisha Wenje ambaye alisimama kuelekea jukwaani huku akishangiliwa kwa nguvu na wananchi ambao walikuwa wakimshangilia kwa kuimba “mbunge, mbunge, mbunge”.
Alipofika jukwaani na kupewa kipaza sauti, Wenje alianza kwa kusema: “Mheshimiwa Waziri Mkuu, hili ndilo Jiji la Mwanza. Kwa kipindi cha miaka miwili iliyopita sijawahi kuona nguo za kijana uwanjani hapa.”
Kauli yake ilizididha mlipuko wa sauti za wananchi wakimshangilia na ndipo alianza kumweleza Waziri Mkuu kwamba Jiji la Mwanza lina malalamiko mengi ya wananchi kuhusu migogoro ya ardhi.
“Mheshimiwa Waziri Mkuu, Jiji la Mwanza lina malalamiko mengi ya ardhi. Nimesema sana ndani ya Bunge, lakini mnanijibu kisanii. Nimemweleza na Waziri wa Ardhi kwamba wanaoteseka sio Chadema peke yao kwani hata wana-CCM nao wana malalamiko vilevile,” alisema.
Wenje ambaye alikuwa amepewa nafasi ya kusalimia tu, aliongeza kuwa ni matumaini yake kwamba ujio wa Waziri Mkuu katika mkoa wa Mwanza utaleta ufumbuzi wa migogoro iliyokithiri katika sekta ya ardhi.
CHANZO: NIPASHE
Post a Comment