IMEELEZWA
kuwa vurugu za kikundi cha Waislamu zilizotokea Mbagala hivi karibuni ni
matokeo ya muda mrefu ya serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM)
inayoongozwa na Rais Jakaya Kikwete kupuuzia kushughulikia matatizo yao.
Kauli hiyo
ilitolewa jana jijini Dar es Salaam na wajumbe wa Kamati Kuu ya Chama
cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Mabere Marando na Profesa
Abdallah Safari, wakati wakizungumza na waandishi wa habari juu ya
msimamo wa chama hicho dhidi ya vurugu za kidini zilizotikisa Jiji la
Dar es Salaam wiki hii.
Marando
alisema kuwakamata viongozi wa Kiislamu pasipo kushughulikia matatizo
yao si njia sahihi kwani kuna hatari ya kuzalisha Waislamu wengi wenye
msimamo mkali dhidi ya serikali na kuifanya nchi kutotawalika.
“Kabla ya
uhuru Waislamu walikuwa na taasisi zao serikali ya TANU, kwa ajili ya
kulinda masilahi yake ikavifutilia mbali na kuamua kuwawekea Waislamu
Bakwata na kutunga sheria za kuongoza, nataka mtambue matatizo ya
Waislamu wote hayasimamiwi na Bakwata, waitwe Waislamu na waulizwe shida
zao,” alisema Marando.
Aliongeza
kuwa kabla ya uhuru Waislamu walipambana kwa kuamini walikuwa
wakinyanyaswa na kwamba baada ya uhuru hawakuona mabadiliko yoyote,
hivyo wanalazimika kujitafutia uhuru mwingine mbali na ule wa kutoka
katika mikono ya wakoloni.
Alisema
serikali isisubiri vifo vitokee ndiyo ione umuhimu wa kushughulikia
matatizo hayo na badala yake ijipe muda wa kukaa na makundi yote
kutafuta muafaka.
“Siamini
kama kuna tatizo baina ya Waislamu na Wakristo bali mfumo wa serikali
unawalazimisha Waislamu kuamini hivyo kwa kuwa wametengwa, hawasikilizwi
hawathaminiwi na sasa wako kama yatima kwanini?” alihoji Marando.
Akizungumzia
utekwaji wa watu unaoendelea nchini, Marando alisema serikali haiwezi
kukwepa lawama hizo na kwamba matamshi ya viongozi wa Ikulu kuwa
hawamfahamu Ramadhani Ighondu ni hadaa kwa Watanzania.
“Sheikh
Farid alipotea katika mazingira ya ajabu na hili ni jukumu la serikali
kujua hatima ya raia wake lakini leo tunaona vyombo vya ulinzi vikisema
havihusiki wala havina habari na kupotea kwake, haya ni majibu kama yale
yale yaliyotolewa kwa Dk. Ulimboka,” aliongeza Marando.
Kwa upande
wake Profesa Safari alizungumzia kitendo cha Jeshi la Wananchi wa
Tanzania kuingilia kati kutuliza ghasia inaonesha kuwa serikali
imeshindwa kuongoza nchi kwa kufuata sheria.
“Jeshi la
Wananchi limefuata nini mtaani? Kuna tishio gani la amani
inayowalazimisha wao kuingia mtaani? Kwa kuwa tunafahamu suala la
kutangaza hali ya hatari na jeshi kuingia mtaani lazima liwe na baraka
ya Bunge,” alisema Safari.
Aliongeza
kuwa mara nyingi serikali imeshauriwa kutatua migogoro baina ya Waislamu
na serikali, lakini ushauri huo umekuwa ukipuuzwa.
Tanzania Daima
Post a Comment