Kamanda wa Umoja wa Vijana wa CCM Mkoa wa Mara,Christopher Gachuma(kushoto) akiwa katika moja ya mikutano ya CCM(Picha na Maktaba yetu.
...............................
*Awataka vijana wawe kama ‘wendawazimu’ 2015
NA DOROTHY CHAGULA, MUSOMA
KAMANDA wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Mara, Christopher Gachuma, amewataka vijana wa chama hicho, kuwa kama ‘wendawazimu’ ifikapo mwaka 2015.
Akifafanua kauli hiyo, Gachuma ambaye pia ni Mjumbe wa NEC alisema, vijana wanapaswa kufikia hali hiyo katika kuhakikisha hadhi ya chama hicho, inarudi katika mwaka huo wa uchaguzi.
Gachuma alitoa kauli hiyo jana katika ukumbi wa CCM wilayani hapa, wakati alipokuwa akitoa nasaha zake kabla ya kuanza kwa uchaguzi wa viongozi wa umoja huo Mkoa wa Mara.
“Katika kuhakikisha hadhi ya CCM inarudi katika uchaguzi wa mwaka 2015, vijana hamna budi kuwa kama wendawazimu, yaani huwa natamani ingewezekana mvute hata bangi,” alisema.
Katika mkutano huo, Gachuma alitoa Sh milioni 6 katika kufanikisha uchaguzi huo, ikiwa ni shinikizo la wajumbe kutaka kulipwa posho baada ya kelele nyingi za “poshooo” kutawala ukumbini.
Pamoja na mambo mengine, Gachuma aliwataka makatibu wa CCM wa wilaya na mkoa, kuandaa makambi ya vijana, kwa ajili ya kile alichokiita kujenga ukakamavu na ujasiri katika kupambana na upinzani.
Katika uchaguzi huo, Ditto Manko (28) alichaguliwa kuwa mwenyekiti mpya wa UVCCM Mkoa wa Mara, baada ya kupata ushindi wa kura 274 kati ya kura 528 zilizopigwa.
Wengine waliogombea nafasi hiyo na kura zao katika mabano ni Gabriel Munassa (245) na Mariam Magesa (7).
Nafasi ya Baraza Kuu Taifa ilikuwa ikigombewa na wagombea watatu na kura walizopata katika mabano ni David Wembe, aliyeshinda kwa kura 253.
Wengine ni Fyeka Sumera (209) na Edward Misanga aliyejitoa baada ya uchaguzi katika nafasi hiyo kurudiwa kwa mara ya pili.
Katika nafasi ya mkutano mkuu CCM Taifa, Kennedy Nsenga alishinda nafasi hiyo kwa jumla ya kura 230, Yohana Munema (48) na Gabriel Munassa aliyeamua kujitoa.
Anna marwa alichaguliwa kuwakilisha nafasi ya uwakilishi wa vijana kwenda Umoja wa Wanawake (UWT) mkoa kwa ushindi wa kura 271 dhidi ya mpinzani wake, Naima Minga aliyepata kura 155.
Naye, Amon Mtega kutoka Songea anaripoti kwamba, mgombea aliyekuwa anawania nafasi ya ujumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM (NEC), Injinia Zephania Chaula kupitia Wilaya ya Ludewa, amekata rufaa ya kupinga matokeo ya uchaguzi.
Mgombea huyo amefikia uwamuzi huo kwa kile kilichodai kutotendewa haki kutokana na kukiukwa kanuni za uchaguzi zilizowekwa na chama hicho.
Akizungumza na Mtanzania jana, Chaula alisema kuwa, amefikia uamuzi huo wa kukata rufaa kupinga matokeo kwa kudai hayakuwa sahihi.
“Wajumbe walipowasili kwa ajili ya uchaguzi waliambiwa ukumbi hautoshi, jambo ambalo tulilazimika kwenda kufanyia uchaguzi nje ya ukumbi, jambo ambalo lilikuwa kinyume na taratibu.
“Kitendo cha kufanyia uchaguzi nje ya eneo husika, kiliwafanya wajumbe kubaki wakishangaa na huku baadhi ya viongozi ambao waliwania nafasi hiyo majina yao hayakurudi.
“Walikuwa wakipiga kampeni za waziwazi kwa kumtaka mgombea wao Elizabeth Haule, aweze kushinda. Hii ni kinyume cha taratibu za uchaguzi.
"Tumeanza uchaguzi kwa mizengwe mikubwa nikapata kura 521na mpinzani wangu 522, huku wa mwisho alipata kura 22 jambo lililowafanya wajumbe kubaki wanalalamika kwa mizengwe na kufanya uchaguzi urudiwe tena,” alisema.
Kwa mujibu wa Chaula, wajumbe walipoanza mchakato wa kurudia kupiga kura, ndipo kigogo mmoja alianza kupiga kampeni za waziwazi kwa kutaka mgombea wake ashinde nafasi hiyo.
Akinukuu maneno aliyosema kigogo huyo, Chaula alisema. “Ndugu wajumbe leo mshindi lazima apatikane na nimewaandalia zawadi wajumbe wote, ninatambua matatizo ya kila kata, hivyo nitawapa majenereta, barabara nk,” alisema.
Kauli hiyo iliwafanya baadhi ya wajumbe kuanza kupiga kelele kuwa, kinachofanyika siyo sahihi na kutaka kila mgombea asimame kwa miguu yake mwenyewe, ili kutoa fursa kwa wajumbe kuchagua mgombea wanayemtaka.
Hata hivyo uchaguzi ulifanyika na baadhi ya wajumbe walitoka kwa kukata tamaa na kuchukizwa kwa mizengwe iliyokuwa ikifanyika katika eneo hilo la uchaguzi, uliofanyika katika viwanja vya Shule ya Msingi Ludewa mjini.
Alisema tayari ameshawasilisha rufaa yake katika ofisi za CCM Mkoa wa Njombe na katika malalamiko hayo ameweka vielelezo vyote vya ukiukwaji wa kanuni za uchaguzi, zikiwemo CD za tukio zima.
Baadhi ya wajumbe katika uchaguzi huo waliozungumza na Mtanzania, walikiri kuwapo kwa ukiukwaji wa taratibu za uchaguzi.
“Uchaguzi wa mjumbe wa NEC, umefanyika gizani na kwenye uwanja ambao hata usalama wa kutambua kuwa, hawa ni wajumbe sahihi au si sahihi ni vigumu,” alisema mjumbe mmoja.
Chanzo:Mtanzania
Post a Comment