Featured

    Featured Posts

    Social Icons

Loading...

NANI ''CCM-B'',CHADEMA AU CUF ?



Madhumuni ya Chama cha wananchi CUF kama yalivyo katika Katiba  yake ni, “Kuwaunganisha watanzania wakatae uonevu,kudhalilishwa,kunyanyaswa,kubaguliwa au maovu mengine yanayoweza kufanywa dhidi ya heshima ya utu wa binaadama, yawe yanayotendwa na Serikali, kikundi cha watu walio na uwezo kwa ajili ya mabavu yao au kwa ajili ya kujinufaisha kwao kiuchumi au kisiasa na kiitikadi au kwa kujali dini, kabila jinsia au rangi zao”. (Kifungu cha, 6[1] Katiba ya CUF uk.12)

Na, JUMA DUNI HAJI

Kwa kiasi miaka miwili sasa ndugu zetu wa CHADEMA wamekuwa wafanikiwa wakisambaza na kufanya siasa nyepesi nyepepi za maji taka kwa watanzania bara kwamba eti CUF ni “CCM-B” kwa sababu ya kuunda Serikali ya Umoja wa kitaifa Zanzibar (Government of National Unity Zanzibar) Dhamiri yangu leo ni kufanya uchambuzi na kuweka wazi kwamba hoja ni “U-CCM-B” au choyo na Kuchukizwa kwa CHADEMA kwa wazanzibari kusikilizana? au ni ukosefu wa dira na agenda sahihi ya kisiasa? Hoja hii ya “U-CCM–B” imerejewa tena na viongozi wa CHADEMA pale Mheshimiwa. James Mbatia alipokubali uteuzi wa Rais Kikwete wa kumteua kuwa mbunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano Watanzania wanapaswa kufahamu kwamba kilichopo pale Zanzibar ni SERIKALI YA UMOJA WA KITAIFA SIYO VYAMA VYA UMOJA WA KITAIFA. Hakuna chama cha CUF wala CCM ambacho kimeungana na kufanya viwili hivyo kufanya umoja unaoitwa CCM-CUF Taifa au vinginevyo. Serikali ya umoja wa kitaifa ilipatikana baada ya kura ya maoni ya Tarehe 31 Julai, 2010 kupigwa na asilimia 66.3 ya wazanzibari bila kujali ni chama gani walikubali kuundwa Serikali hiyo ya GNU. Ni wananchi wa Zanzibar siyo wanachama wa vyama waliopiga kura ya maoni. Tunapokutana katika baraza la mawaziri hatukutani viongozi wa vyama , bali ni Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la
Mapinduzi (Siyo Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi) wanaokutana na kujadili masuala ya maendeleo ya nchi yao na wala si maendeleo ya vyama vyao, wakati wowote chama cha Mapinduzi wanapokutana huwa wanazungumza masuala ya chama chao, na CUF huzungumza chama chao. Kwenye baraza la mawaziri tunazungumza nyaraka za  wizara za Serikali siyo za idara ya chama chochote kati ya hivyo viwili. Sasa huu “U-CCM-B au A” unatoka wapi.

Kama hoja ni chama kuingia Serikalini! Hebu tuone  “UCCM-B” upo wapi?

Madhumuni ya Chama cha wananchi CUF kama yalivyo katika Katiba  yake kifungu cha, 6[8] Katiba ya CUF uk.13) ni “kushika hatamu za dola ili dola au serikali itekeleze vizuri itikadi na sera za chama na ustawi wa Taifa letu” Chama cha siasa ambacho hakina malengo ya kuunda serikali na au kuingia serikalini kuweza kusimamia utekelezaji mzuri wa sera na itikadi na badala yake inajielekeza katika kazi ya kulipua “MABOMU” na kung’ang’ania kupiga kelele za ufisadi hali chama chenyewe na watendaji wake wakiamini kuwa ufisadi ni sehemu ya njia ya kupata manufaa ya kisiasa na kiuchumi, tunavishukuru vyombo vya habari kwa kutujulisha kuhusu hali hii. Hebu tujikumbushe tuone “UCCM-B” upo wapi? Mwaka 1991 Mheshimiwa Ali Hassan Mwinyi Rais wa CCM alimteua Mabere Marando (NCCR) kuwa mjumbe wa Tume ya kuratibu maoni ya wananchi juu kuanzishwa mfumo wa Chama kimoja au vyama vingi chini ya Mwenyekiti Jaji Nyalali, Mwaka 2001, Mabere Marando huyu huyu alichaguliwa na bunge  kuwa Mbunge wa Bunge la EAC akiwa NCCR na kumshida marehemu Bob Makani aliyesimamishwa na CHADEMA, CHADEMA wakarudia, lugha hii wanaowaambia wazanzibari kwamba NCCR Mageuzi ni CCM-B. Leo Mheshimiwa. Marando ni CHADEMA, U-CCM–B wake umeyayuka maana kaingia katika chama kitakatifu kinachopokea maono kutoka kwa Mungu?

Mwaka 2008 Mheshimiwa Rais  Jakaya Kikwete alimteua Zitto Kabwe kuwa mjumbe wa Kamati ya Madini chini ya Mzee Jaji Mark Bomani. Iliandikwa kuwa Mheshimiwa Mbowe amekatisha masomoni yake kutoka nchini ujerumani alikuja kwenye kikao kuthibitisha uteuzi huo, Si Zitto Kabwe wala  chama cha CHADEMA kilichojitangaza kuwa wao ni CCM-B ! , Mwaka huu Rais Kikwete amemteua Prof. Mwesiga Baregu kuwa mjumbe wa Kamati ya kuratibu maoni ya uandikwaji wa katiba ya Jamhuri ya Muungano. Viongozi wa CHADEMA Mr. Slaa na Tundu Lissu wakampongeza Rais na Prof. Baregu, lakini muasisi wa CHADEMA akasema uteuzi huo wa Mheshimiwa Kikwete una “UDINI” akimaanisha WAISLAMU WAMO KATIKA HUO UTEUZI WA KIKWETE!!! HATA hivyo CHADEMA haijawa CCM-B.

John Mnyika na Tundu Lissu walikua na kesi za uchaguzi dhidi ya CCM kule Singida na pale Ubungo. Kesi hizi wameshinda zote chini ya utetezi wa mwanasheria Mkuu wa Serikali ya CCM. Hawasemwi kwamba wametetewa na mwanasheria  wa serikali ya CCM na hivyo ni CCM-B!, April 17, 2012 umefanyika uchaguzi mwengine wa EAC pale bungeni na CHADEMA walikua na wabunge 43 kati ya 48 wa chama hicho wakati kura zikipigwa. Antony Komu mgombea wa CHADEMA alipata  kura 93, kura 50 kati ya hizo zilikua za  wabunge wa CCM. CHADEMA wakaenda mahakamani ili uchaguzi urudiwe ili wapate nafasi ya kuwapata wabunge zaidi kumchagua Komu. Hapa UCCM-B. haukuwepo? Tarehe 22/08/2012 Mahakama kuu kanda ya Tabora imetengua matokeo ya Uchaguzi Jimbo la Igunga na kuwapa ushindi wa kesi hiyo CHADEMA. Uchaguzi utarudiwa. Jee CHADEMA wamesaidiwa na Jaji wa Serikali ya CCM na hivyo na wao ni CCM-B?  Mheshimiwa, James Mbatia alikua na kesi ya uchaguzi ya Jimbo la Kawe lakini akashindwa na Halima Mdee (CHADEMA). Mbatia akaenda Mahakamani kisheria. Viongozi wa CHADEMA wakatafuta njia za kiungwana kumaliza tatizo hilo nje ya Mahakama. Tarehe 6 Februari 2012 makatibu wakuu wa NCCR-Mageuzi Samwel Ruhuza na Wilbroad Slaa walikubaliana kufutwa kwa kesi hiyo No.101/2010 na kumuacha Halima Mdee abaki kuwa Mbunge. Jee Halima nae ni NCCR-B au Mbatia CHADEMA-B?

Mwaka 2001 Rais Mkapa alimteua Mh. Hamad Rashid kuwa Mbunge, wakati huo siasa za ushabiki na mapambano zilikua kubwa mno na CHADEMA kilikuwepo- hoja ya CCM-B hawakuisema. Mwaka 2009 Mheshimiwa Rais Kikwete alimteuwa Mheshimiwa, Ismail Jusa kuwa Mbunge Hoja za “UCCM-B” haikuwepo! Mwalimu Nyerere aliwahi kumpigia kura Paulo Ndorobo wa NCCR-Mageuzi jimbo la Musoma  na Mheshimiwa Ndorobo akashinda Nyerere alikuwa NCCR?

Kuna lugha ya kiswahili ya kuonewa bata kwa sababu ya umbo na sifa zake. Bata akitembea huambiwa anakata viuno kama mrembo wa Tanzania. Hivyo ndivyo alivyoumbwa, hakuchagua kukata viuno anapotembea na wala hajui kwamba anafanya hivyo. Bata huyu huyu anapotafuta chakula kwenye tope huambiwa anakula uchafu sina hakika kwamba CHADEMA wanapokubali uteuzi wa Rais huyu huyu ikawa ni sahihi chakula chao safi, lakini wengine wanapoteuliwa na Rais, kwa CHADEMA hua sawa na kula tope za choo. Kwa  CHADEMA  kuku anapokwenda haja kubwa hua anakunya, lakini bata huambiwa kahara, hakunya: wote wamekunya mmoja amekunya kutu ngumu mwengine kanya kutu laini, wote wamekunya mavi ya kuku na yote yananuka.Vipi CHADEMA wao wajione watakatifu wanapopata uteuzi kwa Rais wengine wawe wamekufuru, huu ni unafiki na uzandiki wa viongozi wanaotaka eti wapewe dhamana ya kuongoza nchi kwa akili kama za Panzi. Kule Kigoma CCM na CHADEMA walikubaliana na CCM kuunda Serikali ya Halmashauri ya Kigoma nusu kwa nusu ya madiwani kwa miaka mitano. Hoja ya CCM kuioa CHADEMA CCM-B haikutajwa, yaani yale kwa CHADEMA  yalikua na mavi ya kuku CUF na CCM Zanzibar ni uharo wa bata. Kule Arusha kulikua na Serikali ya aina hiyo, mpaka yalipotokea malumbano na upuuzi wa wawakilishi wa wananchi [madiwani] walipozuiliwa na chama chao CHADEMA kuwawakilisha barazani.

Wengi tumezoweshwa kwamba siasa ni uongo na mchezo mchafu, Hapana, Moja ya suala ambalo CUF na viongozi wake tunalisimamia na kutaka watanzania waamini kuwa Siasa si uongo wala si mchezo mchafu bali baadhi ya wafanya siasa[wanasiasa] ndio waongo na wachafu. Kama viongozi wanaweza kusema uongo wa kiwango cha uharo wa bata wakiwa nje ya Ikulu watakunya nini hawa wakiingia ikulu? Kama kuna viongozi wanaweza kuiba wake za watu na kuja jukwaani kujisifu kwamba wao ni wezi wa wake za watu, jee wakiwa ikulu watafanyaje hawa?, watawapanga foleni wanawake wote waliopo pale kwa uwezo wa  madaraka yao ya urais na kuwalazimisha kufanya nao ngono. Hivyo tunategemea hawa wakajenge nyumba ya umalaya pale ikulu, je nyie ndiyo munashangilia hayo? Eti kunja ngumi, ngumi gani ya wizi wa wake za watu? Eti kunja ngumi, ngumi ya kutengeneza vifo vya watanzania wenzetu? Watanzania muna kila sababu za kutafakari na kuchukua maamuzi sahihi juu ya hatma na mustakbali wa maisha yenu ya sasa na kizazi kijacho, wapi pa kuunganisha nguvu zenu ili mabadiliko ya kweli kiuchumi na kisiasa yaweze kupatikana. Siasa za milipuko na mihemuko za leo linasemwa hili na kesho linasemwa vinginevyo jambo hilohilo hazina nafasi kwa CUF ya DIRA YA MABADILIKO.

SUALA LA U-A na U-B unatoka wapi na unakujaje katika mahusiano ya chama kimoja na kingine wakati kilichojenga umoja ni ridhaa ya wazanzibari. Mwaka 2005 hadi 2010, wabunge wa Chama cha wananchi CUF kiliunda kambi ya upinzani na wabunge wa CHADEMA bungeni kwa miaka mitano, na Dk. Slaa akawa Naibu kiongozi wa kambi hiyo kwa muda wote wa miaka mitano. MheshimiwaZitto na wabunge wengine wa chama hiki wakishika nyadhifa za uwaziri kivuli wa Kambi hiyo. Ilikua ni Serikali kamili nje ya Serikali ya Muungano. Vyama viwili hivi viliendelea kubaki na shughuli zake ndani na nje ya Bunge. Mbona hoja ya CHADEMA kujiita CUF-B haikuja wala hawakujigamba hivyo kuwa wao ni CUF-B? Chama cha wananchi CUF kilifanya hivyo kwa sababu madhumuni yake ni: “Kuwaunganisha watanzania wakatae uonevu,kudhalilishwa,kunyanyaswa,kubaguliwa au maovu mengine yanayoweza kufanywa dhidi ya heshima ya utu wa binaadama, yawe yanayotendwa na Serikali, kikundi cha watu walio na uwezo kwa ajili ya mabavu yao au kwa ajili ya kujinufaish kwao kiuchumi au kisiasa na kiitikadi au kwa kujali dini, kabila jinsia su rangi zao”.

Muda wote huu vyama vya upinzani tumeshindwa kuungana na kukiondoa chama cha CCM kwa sababu ya udhaifu huu wa CHADEMA kujikubalisha kujigawa mafungu huku CCM ikichekelea na kutuona wajinga. Ujinga na upumbavu huu umezidi tulipogundua kwamba Viongozi wa CHADEMA wanaonesha udhaifu wao kwa kukosa furaha kuwaona wazanzibari wanasikilizana na nyinyi wananchi munafurahia hilo kwamba tuaachwe wazanzibari tuuwane na kwamba eti hicho ndiyo chama munachokitaka eti kiingie Ikulu. Msimamo huu wa CHADEMA ni kuthibitisha kwamba Wazanzibari kugombana ndiyo furaha ya viongozi wa Chama hicho, maana furaha na agenda ya muda mrefu ya baadhi ya viongozi watanganyika wawe wa CCM au CHADEMA ni kuhakikisha WAZANZIBARI tunawagawa ili tuwatawale (divide and rule them) Kama hivyo ndivyo wazanzibari hatuna sababu ya kushangaa ya jinsi viongozi wenzetu wa Tanganyika munavyotuona, maana sisi wazanzibari ambao wazee wetu akina mzee Karume na Mzee Thabit Kombo walimuamini mwalimu Nyerere kwa kuunganisha nchi mbili hizi kwa faida ya pande mbili, leo vijana wake waliorithi siasa zake wanaziendeleza kwa kutuambia eti Zanzibar siyo nchi. Wakati viongozi (Tundu Lissu) wanafurahia na kushikilia kwamba Zanzibar siyo nchi, chama hicho hicho kinashikilia hadharani kupitia kwa Joshua Nassari mbunge wa CHADEMA wa Arumeru Maashariki, anapendekeza na kusisitiza kuwa mikoa ya kaskazini ya Tanganyika kujitenga na kua taifa pekee. CUF hatuamini katika siasa za kikabila na kuigawa nchi mapande pande kwa siasa za itikadi za kimajimbo. Maana kama Arusha ijitenge na wasukuma wa Mwanza na Shinyanga ambao ni wengi na ni mikoa miwili tajiri kuliko mikoa yote nao  pia watajitenga na wale wa Mbeya watajitenga na wale kusini kwa wamakonde nao watajitenga. Kwa hivyo hata hiyo Tanganyika pia haitokuwepo. Mwalimu Nyerere aliwahi kusema mara kadhaa kwamba Tanzania ipo kwa sababu ya Zanzibar. Msimamo wetu ni kuwa wazanzibari hawako tayari tena kufanywa koloni la Tanganyika. Kinachohitajika sasa ni kurekebisha makosa yaliyofanywa miaka 50 iliyopita yaliyoasisiwa na mwalimu Nyerere mwaka 1964.

Ninachotaka kuwakumbusha watanzania na Machadema, ni kwamba Mimi binafsi na wenzangu wengi ni wahanga wakubwa wa siasa mbovu za zamani za Zanzibar, tuliathirika sana kwa kubambikiwa kesi za uhaini na kesi za mauaji, leo ni waziri wa Serikali ya umoja wa kitaifa siyo umoja wa vyama vya CCM na CUF. Wazanzibar tumemaliza matatizo yetu ya ndani wenyewe, tumeamua kujenga nchi yetu, wakati nyinyi yenu munaitayarisha ibomoke, sisi huko tumeshatoka. Fursa ya kujenga siasa za kistaarabu, siasa za heshima, siasa zenye lengo la kuwasaidia watu wetu kuondokana na lindi la umasikini, maradhi na ujinga ipo, HATUJACHELEWA! Tuutumie vyema mchakato wa uratibu wa ukusanyaji maoni ya katiba, ipendekezwe uwepo wa UUNDWAJI WA SERIKALI YA UMOJA WA KITAIFA, CUF katika manifesto yetu ya mwaka 2010 tuliieleza hili. CUF chini ya dira ya mabadiliko[vision for change] inaamini katika mazungumzo [dialogue],

Kwa hivyo CHADEMA angalieni siasa zenu kama mnataka kuendelea na siasa za kuonja umwagaji wa damu kisha ndo muamini juu ya ‘diablogue’ endeleeni kujaribu, kama munaamini kuwa njia siasa hizo mnazozitaka zisizo na ushirikiano na wenzenu, siasa za nchi isitawalike, siasa za maandamano, siasa za propaganda chafu, siasa za kubaka wake za watu, siasa za kutaja mafisadi wazuri na mafisadi wabaya, kama mnaamini kufanya hivyo ni sehemu ya utekelezaji wa maagizo kutoka kwa Mungu. Namaliza kwa kuwaambia Zanzibar kuna Serikali ya umoja wa kitaifa , hakuna muungano wa vyama vya kitaifa, wala hakuna CCM-B wala CUF –G. Kilichopo ni Serikali siyo vyama kuunganisha nguvu kujenga taifa letu. Na ndugu zangu watanganyika hamtaweza katu kumaliza migogoro yenu ya kisiasa na kidini kama hamukuunda serikali ya umoja wa kitaifa.

Mungu Ibariki Tanzania!

Mungu Ibariki Zanzibar!



Muandishi wa makala hii ni waziri wa Afya wa serikali ya umoja wa kitaifa Zanzibar na mjumbe wa baraza kuu la uongozi CUF Taifa. Harakati za kisiasa zilimuweka ndani bila kuhukumiwa miaka mine[4]


author

This post was written by: Author Name

Your description comes here!

Get Free Email Updates to your Inbox!

Post a Comment

CodeNirvana
Chediel . Powered by Blogger.
© Copyright Rundugai Blog
Back To Top