Hussein Ramadhani ‘Sharo Milionea’ (27)
..........
Kwa ufupi
“Alijitahidi, amejipatia usafiri maskini ya Mungu,
kapata pa kulala, katoka Dar kwenda Tanga kuwaona wazazi kwa gharama
zake mauti yamemkuta. Jambo la msingi tumuachie Mungu na kuondoa mawazo
mabaya kuhusu na kifo chake.”
............
............
Gari la mwigizaji hiyo lilipoteza mwelekeo
na kupinduka mara kadhaa wakati akiwa safarini kutoka Dar es Salaam
kwenda kijijini kwao, Lusanga mkoani Tanga, na kusababisha kifo chake
saa 2.30 juzi usiku.
Mwandishi wa gazeti hili alifika nyumbani kwa wazazi wa msanii huyo jana na kupokewa na vilio vya waombolezaji.
“Masikini mdogo wangu, ametutoka akiwa
mdogo, masikini mama yetu, ndoto za kujengewa nyumba na kuboreshewa
maisha zimeishia barabarani,” ni maneno aliyokuwa akiyatoa dada wa
marehemu.
Dada huyo aitwaye Rehema Kadiri (38)
alilieleza Mwananchi kuwa msanii huyo alikuwa akienda kijijini, Lusanga
kumpelekea mama yake mzazi fedha kwa ajili ya kulimia shamba.
Alisema ahadi hiyo alikuwa ameitoa wiki
iliyopita alipokuwa amekwenda kijijini hapo kuhudhuria kumbukumbu ya
marehemu babu yake, Mkieta Juma aliyefariki dunia mwaka juzi.
Mazingira ya ajali
Mwenyekiti wa Serikali ya Kitongiji cha Songa
Kibaoni, Kijiji cha Songa, wilayani Muheza, Abdi Zawadi alisema
ilipofika saa 2.30 usiku wakazi wa eneo hilo walisikia kishindo kikubwa
ndipo wakaenda kushuhudia.
Alisema walipofika eneo la tukio, walikuta
gari aina ya Harrier likiwa limepinduka, huku mwili wa mwanaume mmoja
ukiwa pembeni, ndipo walipomfuata na kumkuta ameshakufa.
“Tulimtambua kuwa ni Sharomilionea baada ya
kupekuwa mfukoni na kukuta kitambulisho cha mpiga kura kikiwa na jina
la Hussein Ramadhani kikionyesha kuwa alijindikisha Lusanga, tukapaiga
simu Kituo cha Polisi Muheza na askari wakaja kuuchukua mwili.
Mwananchi ilipofia eneo la tukio
ilishuhudia mti mkubwa aina ya mjohoro uliogongwa baada ya gari hilo
kuachia njia, ukiwa umeanguka na gari kupinduka hadi umbali wa mita kama
50.
Watu walioshuhudia ajali hiyo walisema
ndani ya gari hilo lalikuwamo dereva peke yake, likiendeshwa kwa mwendo
mkali, na baada ya kupinduka dereva huyo ambaye ndiye msanii
Sharomilionea alitupwa nje.
“Hata kama angekuwa amefunga mkanda, kiukweli kwa jinsi gari
hilo lilivyogonga mti mkubwa vile na kuuangusha, lazima angekatika kwani
katupwa mbali sana,” alisema Bakari Hassan.
Kauli ya polisi
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Tanga, Costantine
Massawe alisema ajali hiyo ilitokea katika eneo la Songa Kibaoni, Wilaya
ya Muheza na Sharomilionea (sasa marehemu) ndiye aliyekuwa akiendesha
gari hilo.
Umati hospitalini
Katika Hospitali Teule wilayani Muheza, umati wa
wananchi ulifurika baada ya kusikia aliyefariki katika ajali hiyo
alikuwa msanii huyo.
Katika mji wa Muheza na vitongoji vyake wananchi
walimiminika hospitalini hapo wakiongozwa na Mbunge wa Jimbo la Muheza,
Herbert Mntangi na Mkuu wa Wilaya ya Muheza, Subira Mgalu kushuhudia
hali hiyo.
Mntangi alilazimika kufanya kazi ya ziada ya
kuwasihi wananchi waliokusanyika chumba cha maiti wakiwa na shauku ya
kuingia ndani kuushuhudia mwili wa msanii huyo.
“Jamani naomba fanyeni subira, subirini wataalamu
wafanye uchunguzi kwanza, lakini pia inabidi uandaliwe utaratibu maalumu
wa namna ya kuushuhudia mwili.
“Hivi mnavyofanya vurugu siyo ustaarabu,” alisema
Mntangi, na baada ya kauli yake ndipo wananchi wakaachia lango la chumba
cha maiti.
Kaimu Mganga Mkuu wa Hospitali hiyo, Julius Mgema
alisema polisi ndiyo walioufikisha mwili wa marehemu hospitalini hapo
saa 3 usiku na wakaupeleka kwenye chumba cha kuhifadhia maiti kwa ajili
ya taratibu nyingine.
Familia ilivyopokea taarifa
Kwa upande wake, Mtoto wa Mama Mdogo wa Msanii
huyo, Emmanuel Paulo alisema wao kama familia wamepokea kwa masikitiko
msiba huo na pengo lake halitaweza kuzibika kutokana na mchango wake
katika familia yao.
“Tuna masikitiko makubwa kutokana na msiba wa ndugu yetu, najua
tunaumia ila kazi ya Mungu haina makosa,” alisisitiza ndugu huyo huku
alibubujika machozi katika eneo la Hospitali ya Teule wilayani Muheza.
Aliongeza kuwa ndugu yao huyo alitokea Dar
es Salaam hadi Kata ya Hale wilayani Korogwe juzi akitumia gari yake
binafsi, kwa mujibu wa taarifa ambazo zilitolewa na rafiki yake wa
karibu.
Kwa mujibu wa Paulo, kutoka Hale kwenda Muheza, Msanii huyo aliazima gari la rafiki yake, nalilopata nalo ajali.
“Yule rafiki yake aliyeazimwa gari, alimwambia Sharomilionea kuwa gari ambayo anaiazima sio yake, bali ni ya mama yake.”
Wasanii wamlilia
Wasanii mbalimbali wamesema ni kipindi kigumu kwao
baada ya kuondokewa na wasanii wawili katika kipindi kifupi, akiwemo
Mlopelo aliyefariki Jumamosi wiki iliyopita, na jana wamemzika msanii
mwingine wa Bongo Movie, John Stephano.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti wasanii hao
walionyesha kushtushwa na kifo cha Sharo Milionea ambaye kwa siku za
karibuni alivuta mashabiki wengi kutokana na filamu za vichekesho.
Rafiki mkubwa wa marehemu Sharo Milionea, Mussa
Kitale ‘Kitale’ alisema: “Siamini kama Sharo amefariki, nilikuwa
nampigia simu ilikuwa inaita muda mrefu bila kupokewa na baadaye usiku
Tundaman akanipigia kunipa taarifa za kifo, sikuamini.
“Mzee Majuto naye akanipigia, na mjomba wa
Sharo naye alinipigia, nikaamini japo sikuamini na mpaka sasa sitaki
kuamini kama Sharo sitamuona tena.”
Rais wa Shirikisho la Filamu Tanzania (TAFF),
Simon Mwakifwamba alisema: “Ni pigo kubwa katika tasnia ya filamu,
vijana wanazidi kupuputika tena nyota zao zikiwa zinang’aa.
“Sharo amezimika kama mshumaa kwenye upepo mkali,
hatuna jinsi zaidi ya kumuombea na kuiombea familia yake, siku zote
tunasema kazi ya Mungu haina makosa.”
Steve Nyerere alisema: “Tunamalizia msiba wa
Stephano leo (jana) mimi ndio mwenyekiti wa kamati ya mazishi, kisha saa
10 (jana) tunaelekea Tanga kumzika kipenzi chetu Sharo, ambaye naweza
kusema amefariki akiwa ameanza kupata mafanikio, alianza kupata
matumaini. Ni sawa na unatupa mbegu halafu hujui kama itachipua au
itaozea ardhini.
“Sharo alianza kuchipua, ameanza kujitegemea yeye kama yeye,
sababu katika maisha lazima uanze wewe, pili uiangalie jamii inahitaji
nini kwako.
“Alijitahidi, amejipatia usafiri maskini ya Mungu,
kapata pa kulala, katoka Dar kwenda Tanga kuwaona wazazi kwa gharama
zake mauti yamemkuta. Jambo la msingi tumuachie Mungu na kuondoa mawazo
mabaya kuhusu na kifo chake.”
Filamu alizoshiriki
Sharo Milionea aliibuka katika filamu mbalimbali
akiigiza na King Majuto, ikiwemo ‘Mtoto wa Mama’ Back From New York,
Kitale na Sharo ambayo ni tangazo ambalo limeingizwa kwenye milio ya
simu.
Msanii huyo alipata umaarufu zaidi katika
matangazo yake ya Airtel Money akiwa na King Majuto pamoja na lile la
Azam Cola hasa staili yake ya kuongea ‘Kisharobalo’ akitumia maneno kama
‘Haaa! nimebugi meeeen! Ooooooh Mamaaa.
Akimzungumzia msanii huyo, Mkurugenzi wa
Mawasiliano wa Airtel, Beatrice Mallya alisema tasnia ya sanaa imepoteza
mtu muhimu kwani ndiyo alikuwa anaanza kuja juu.
“Tunasikitika kama Watanzania wengine, hasa
washabiki wake, alikuwa mcheshi, mtu wa utani na masihara...sisi kama
Airtel tutashiriki kikamilifu katika mazishi yake,” alisema Mallya
ambaye hata hivyo alisita kusema kama watasitisha urushaji matangazo
yake au la
Chanzo:Mwananchi.
Chanzo:Mwananchi.
Post a Comment