Na Hassan Hamad OMKR
KATIBU Mkuu wa Chama cha Wananchi CUF, Maalim Seif Sharif Hamad ametoa
wito kwa Mwenyekiti wa Tume ya Kuratibu Maoni ya Wananchi juu ya
Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Sinde Warioba na tume yake kuweka
bayana muundo wa Mabaraza ya Katiba ya Wilaya yatakayo jadili maoni ya
wananchi, ili kuepusha Mabaraza hayo kutawaliwa na wajumbe wa chama
kimoja.
Maalim Seif alisema hayo jana huko katika viwanja vya Alabama
Michenzani, wakati alipokuwa akihutubia mkutano wa hadhara ulioandaliwa
na chama hicho, ikiwa ni siku moja kabla ya Tume hiyo ya kuratibu maoni
ya wananchi juu ya mabadiliko ya Katiba kuanza kazi hiyo katika Wilaya
ya Mjini hii leo tarehe 06/12/2012.
Maalim Seif ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, alisema
baada ya hatua hiyo ya kuchukua maoni ya wananchi kukamilika, tume
itarudi ofisini kuyajadili na baadaye yataundwa Mabaraza ya Katiba ya
Wilaya ambayo pia yataweza kujadili maoni hayo ya wananchi, kabla ya
kuchukuliwa hatua nyengine.
Alisema kuwa lazima kuwe na uwazi na wananchi waelezwe Mabaraza hayo
yataundwa na wajumbe wepi, ili kuondoa dhana mbaya inayoweza kujengwa na
wananchi kuwa wajumbe hao watatoka katika chama kimoja cha siasa.
Alisema dhana kama hiyo ikijengeka inaweza kusababisha dosari katika
mchakato mzima wa mabadiliko ya Katiba, hivyo tume hiyo ichukue hatua za
makusudi kulitolea ufafanuzi suala hilo.
“Mheshimiwa Warioba lazima muwe wawazi, hadi sasa Mabaraza ya Katiba ya
Wilaya hapana anayejua muundo wake, vyenginevyo unaweza ukakuta wajumbe
wote wanatoka katika chama kimoja”, alishauri Maalim Seif.
Aidha, Maalim Seif alisema uwazi pia unahitajika wakati wa kuundwa kwa
Bunge la Katiba, ambapo mbali ya Wabunge wote na Wawakilishi wote kuwa
wajumbe kuna wajumbe wengine 164, ambao watateuliwa na Rais wa Jamhuri
ya Muungano kwa ushirikiano na Rais wa Zanzibar, lakini hadi sasa
utaratibu gani utatumiwa kuwapata wajumbe hao haufahamiki.
Alisema ili kujenga imani kwa wananchi na kuepusha dhana mbaya
itahitajika uadilifu mkubwa kwa Rais, hasa kwa wale watakaotoka Zanzibar
basi kuna haja wawe angalau 55, na vile vile wasitoke katika chama
kimoja cha siasa.
Aidha, Maalim Seif alisema hata katika suala la kura ya maoni
itakayokuja kufuatia huko mbele, bado kuna masuala mengine ya kujiuliza,
kuhusu utaratiubu upi utatumika, wakati wa kura hiyo kwa Wazanzibari
wanaoishi Tanzania Bara na watu wa Tanzania Bara wanaoishi Zanzibar.
Alieleza kuwa hofu hiyo inakuja kwa vile sheria ya mabadilikko ya katiba
inasema mabadiliko hayo yatapitishwa, iwapo angalau nusu ya wananchi wa
kila upande kati ya Tanzania Bara na Zanzibar wataunga mkono mabadiliko
hayo, hivyo amehimiza mambo hayo lazima kwanza yawekwe wazi.
Kuhusu maoni ya wananchi juu ya mabadiliko ya Katiba, Maalim Seif
ametowa wito kwa Wazanzibari kutoa maoni ambayo yatazingatia zaidi
maslahi ya Zanzibar, na kusema kuwa mfumo wa Muungano wa serikali mbili
uliopo sasa kamwe hauwezi kuleta ufumbuzi wa matatizo ndani ya Muungano
yaliyodumu tokea Muungano huo ulipoanzishwa.
Aidha aliwafahamisha wananchi hao kuondokana na dhana ya serikali mbili
kwani haina maslahi ya nchi kwani hata rais wa Zanzibar huwa anabezwa
katika kufanya baadhi ya maamuzi kwa nchi yake.
“Mimi sina haja ya kuficha wala kutafuna maneno, mimi ni muumini wa
Muungano wa Mkataba, maana ni imani yangu kuwa muundo wa Muungano huu
tuliuonao hauwezi kuondoa kasoro zilizopo hadi kiama”, alisema Katibu
Mkuu wa CUF.
Alitoa wito kwa wananchi katika Wilaya ya Mjini kujitokeza kwa wingi
kwenda kutoa maoni kuanzia leo, na wasikubali kudanganywa na baadhi ya
watu wanaotoa fedha kuwarubuni wakatoe maoni, kama wanavyowaelekeza wao.
Mapema, Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Umma na Haki za Binaadamu wa CUF,
Salum Bimani aliwataka Wazanzibari kuweka mbele maslahi ya Zanzibar
katika zoezi la kutoa maoni ya katiba na kuweka kando itikadi zao za
vyama vya siasa.
Kaimu Naibu Katibu Mkuu wa CUF Zanzibar Hamad Massoud Hamad, kwa upande
wake amesema Chama hicho kimezidi kuimarika kuliko wakati wowote tangu
kuanzishwa kwake, na kuwaomba wananchi waendelee kukiunga mkono ili
kutimiza malengo yake ya kutetea maslahi ya Zanzibar ndani na nje ya
nchi.
Chanzo ZanziNews
Post a Comment