Featured

    Featured Posts

    Social Icons

Loading...

IDADI YA WATU YAMTISHA JK


Rais Jakaya Kikwete, akibonyeza kompyuta ndogo kuzindua matokeo ya Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012, kwenye hafla ya uzinduzi viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam jana. Wengine ni Makamu wa Rais, Dk. Mohamed Gharib Bilal (kulia), Waziri Mkuu, Mizengo Pinda (wa pili kushoto) na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi.
,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,
Rais Jakaya Kikwete jana alitangaza matokeo ya awali ya Sensa ya Watu na Makazi iliyofanyika Agosti hadi Septemba, mwaka jana Tanzania Bara na Zanzibar, huku akionyesha wasiwasi wake kuhusu kasi kubwa ya ongezeko la watu nchini, ambao wameongezeka kutoka 34,443,603 waliohesabiwa mwaka 2002 kufikia 44,929,002 waliohesabiwa mwaka jana.
 Kutokana na wasiwasi huo, Rais Kikwete ametaja mikakati mbalimbali na kuwataka Watanzania kuitumia ili kudhibiti hali hiyo, ikiwamo kuzaa kwa mpango.

Rais Kikwete alitangaza hayo katika hafla ya uzinduzi wa matokeo ya sensa hiyo, katika viwanja vya Mnazi Mmoja, jijini Dar es Salaam.


Hafla hiyo ilihudhuriwa pia na Makamu wa Rais, Dk. Mohammed Gharib Bilal; Waziri Mkuu, Mizengo Pinda; Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi; baadhi ya mawaziri; wabunge; wajumbe wa Baraza la Wawakilishi la Zanzibar; viongozi wa serikali; dini; vyama vya siasa; hiari, mashirika ya kimataifa mabalozi na wakazi wa jiji la Dar es Salaam na vitongoji vyake.

 Rais Kikwete alisema katika idadi ya watu wote waliohesabiwa katika Sensa ya mwaka jana, 43,625,434 ni walioko Tanzania Bara na 1,303,568 walioko visiwani Zanzibar.
 Alisema Sensa ya mwaka jana (2012), imekamilisha jumla ya sensa tano zilizokwisha kufanyika, huku sensa ya kwanza ikiwa imefanyika mwaka 1967 baada ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.
 Sensa nyingine za watu na makazi, zilifanyika mwaka 1978, 1988 na 2002.  Rais Kikwete alisema kwa mujibu wa matokeo ya sensa ya mwaka huo (1967), idadi ya Watanzania walikuwa 12,313,504.
 Alisema matokeo hayo ya Sensa ya mwaka jana, yanaonyesha kuwa katika kipindi cha miaka 45 iliyopita kutoka mwaka 1967, watu milioni 33 wameongezeka nchini.
 Pia alisema kutoka mwaka 2002 hadi mwaka jana, matokeo ya sensa hiyo yanaonyesha kuwa watu milioni 10.5 wameongezeka nchini.
 “Kwa kasi hii ya ongezeko la watu, kufikia mwaka 2016 Tanzania itakuwa na watu milioni 51. Ni mzigo mkubwa kwa taifa, jamii na kwa uchumi wa kuwahudumia watu,” alisema Rais Kikwete.

UZAZI WA MPANGO

Kutokana na hali hiyo, alisema kwa upande wa taifa, kuna haja kubwa kwa serikali kuanza kujipanga vizuri kwa kuweka mikakati ya kiuchumi ili iweze kuwahudumia watu walioongezeka.
 Kwa upande wa jamii, aliitaka kuanza kujipanga vyema na kusema kupanga uzazi ni jambo la msingi sana katika jitihda za kudhibiti kasi ya ongezeko la watu nchini.
 “Vinginevyo, hali ya maisha itashuka,” alitahadharisha Rais Kikwete na kuongeza: “Ni muhimu kupanga ili ujue utazaa kwa kipindi gani na watoto wangapi ili uweze kuwahudumia.”
 Pia aliwataka Watanzania kufanya kazi kwa bidii ili kuwa na ustawi mzuri wa kiuchumi nchini.
 Alisema matokeo ya sensa ya mwaka jana yaliyotangazwa jana yamekamilika.  Hata hivyo, alisema kazi ya kutangaza matokeo ya sensa hiyo itaendelea katika mwezi ujao na kwamba, kipindi hicho itakuwa ni kwa ajili ya kujua idadi ya jinsia nchini na pia Aprili, mwaka huu, yatatangazwa matokeo ya idadi ya watu na kazi katika wilaya.
 Alisema sensa ya mwaka jana haikuwa kazi rahisi, kwani kuna watu walitumia mitumbwi, wengine kupanda milima na mabonde na wengine kupita kwenye misitu yenye wanyama wakali kwa ajili ya kufanikisha kazi hiyo.
 Rais Kikwete alisema ana uhakika ahadi iliyotolewa na Waziri wa Fedha, Dk. William Mgimwa, ya kuhakikisha makarani na wasimamizi wa sensa wanaodai posho zao, watalipwa na kusisitiza kuwa ahadi hiyo isiwe ni “kuondoa ngoma juani.”
 Alisema Sh. bilioni 124 kati ya Sh. bilioni 140 zilizohitajika, zimetumika kufanikisha kazi hiyo ya kuhesabu watu na makazi mwaka jana.
 Rais Kikwete alisema katika sensa zote zilizopita, asilimia 63 ya watu waliohesabiwa walikuwa chini ya umri wa miaka 30.
 Alisema katika sensa ya mwaka jana walifanikiwa kukusanya taarifa nyingi, ikiwa ni pamoja na kupima vigezo vya maendeleo na kuagiza taarifa hizo zipatikane kwa wakati.

 Alimpongeza Kamishna Mkuu wa Sensa ya Watu na Makazi, Hajati Amina Mrisho, kwa kazi nzuri na Watanzania kwa jumla kwa ushirikiano waliouonyesha katika zoezi hilo, ambalo alisema lilikuwa na mitihani.
 PINDA ALONGA
Awali, Pinda, ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati Kuu ya Taifa ya Sensa ya Mwaka 2012, alisema sensa ya mwaka jana kama zilivyo sensa nyingine zilizotangulia, imegharimiwa kwa pamoja na serikali na washirika wa maendeleo.
 Alisema mchango wa serikali katika kugharimia zoezi hilo umekuwa ukiongezeka kutoka sensa moja hadi nyingine.
 Pinda alisema kwa sensa ya mwaka jana, serikali ilichangia asilimia 90 kutoka asilimia 70 kwa sensa ya mwaka 2002.
 Pia alisema sensa hiyo iliendeshwa kwa kiasi kikubwa na wataalamu wa ndani kuliko ilivyokuwa kwa sensa iliyopita na kusema hatua hiyo inaonyesha kukua kwa utaalamu wa ndani katika uendeshaji wa sensa na tafiti nyingine hapa nchini.
 Alisema pamoja na faida za sensa, utekelezaji wake uliweza kutoa ajira ya muda mfupi kwa wananchi, hususan vijana, ambao hawakuwa na ajira.
 Pinda alisema jumla ya watenga maeneo ya kuhesabia watu 150, makarani na wasimamizi wa sensa 200,000 na wachambuzi wa takwimu 400 waliajiriwa katika vipindi tofauti wakati wa kipindi chote cha utekelezaji wa zoezi la sensa na kwamba, Sh. bilioni 90 zilitumika kulipa stahili zao.
 Vilevile, alisema vijana wengine wapatao 400 watapatiwa ajira ya muda mfupi wakati wa zoezi la tathmini ya sensa.
 Alisema pia wazabuni wa ndani wapatao 29 walitoa huduma na vifaa mbalimbali kwa ajili ya zoezi la sensa kwa gharama ya Sh. bilioni 11.7 pamoja na Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT).
 Pinda alisema utoaji wa zabuni hizo ulizingatia Sheria ya Ununuzi wa Umma ya Mwaka 2004 pamoja na kanuni zake za mwaka 2005.
 Alisema sensa hiyo ilifanyika kwa weledi na ufanisi mkubwa licha zoezi hilo kukabiliwa na changamoto.
 Pinda alisema kutokana na ukubwa na uzito wa zoezi la sensa, watu wanne walipoteza maisha wakati wakiwajibika kufanya kazi hiyo na wengine kujeruhiwa.

BALOZI IDDI ANENA

Naye Balozi Iddi, ambaye ni Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo ya Sensa, alisema takwimu za sensa zitakuwa na maana kama zitatumika vizuri katika kupanga vizuri katika kupanga mipango ya maendeleo ya Watanzania.

WAZIRI WA FEDHA

Waziri wa Fedha, Dk. William Mgimwa, alisema Tanzania ina historia ya kufanya sensa kwa mafanikio na kwamba, sensa ya mwaka jana, ambayo ililenga kuchangia kuboresha maisha ya Watanzania, ilifanikiwa kutokana na kukua kwa teknolojia na matumizi yake na utayari wa serikali katika kuifanikisha.
 Alisema sensa hiyo iliyofanyika kwa miezi miwili, maandalizi yake yalianza mwaka 2004 na kwamba, wizara yake imepanga kusambaza taarifa za sensa hiyo kwa njia mbalimbali, ikiwamo tovuti ili kuzua mjadala.
 Mwakilishi wa mashirika ya kimataifa ya idadi ya watu, Mariam Khan, alisema sensa ni jambo muhimu kwa watunga sera katika kupanga mipango ya maendeleo katika milenia.
 Mapema, Hajati Mrisho alisema watahakikisha machapisho yote ya sensa yanakuwa kwa lugha ya Kiswahili kuanzia Juni, mwaka huu.

SALAMU ZA MWAKA MPYA

Wakati huo huo, Rais Kikwete amewahakikishia wakazi wa mikoa ya Lindi na Mtwara ambako gesi asilia ilipogunduliwa au popote itakapogundulika, kuwa watanufaika sawia na katu hawatasahaulika.

Rais Kikweta alitoa ahadi hiyo jana usiku katika hotuba yake kwa Taifa ya kuukaribisha mwaka mpya wa 2013 kupitia vyombo vya habari.


Alisema   rai yao ya kutaka na wao wanufaike inakubalika na Serikali inajiandaa hivyo. “Viongozi wa Mikoa ya Lindi na Mtwara kwa mfano, wanajua maelekezo niliyotoa kuhusu kuiandaa miji ya Mtwara na Lindi kupokea uchumi wa gesi,” alisema na kuongeza:


“Lakini, sharti la kutaka gesi isisafirishwe kwenda kokote na kwamba kila kitu kifanyike kwao halikubaliki. Rasilimali inayopatikana popote katika nchi hii ni mali ya taifa zima na hutumika kwa manufaa ya taifa. Katu siyo mali ya watu wa pale ilipogundulika au pale shughuli hizo zinapofanyika.”


Alisema  jumla ya makusanyo ya mapato yatokayo sehemu zote za nchi yetu na kutokana na vyanzo mbalimbali ndiyo yanayotumika kuhudumia watu wote po pote walipo.


“Huu ni msingi mzuri, ni sera nzuri na ni jambo jema la tunu, tulilorithi kwa waasisi wa Taifa letu, ambalo hatuna budi kulienzi na kulidumisha.  Nawasihi wanasiasa wenzangu tusiwaelekeze kwenye mambo mabaya wananchi tunaodai kuwapenda. Kutafuta umaarufu kwa ajenda zinazopandikiza chuki kwa watu na kuligawa au kulibomoa taifa, ni upungufu mkubwa wa uongozi na uzalendo.  Tuache siasa za ubarakara na kuwapa watu matumaini yasiyotekelezeka.  Nawaomba wananchi msiwasikilize, si watu wanaowatakia mema na wala hawaitakii mema nchi yetu,” alisema Rais kufuatia wakazi wa Mtwara kuandamana wiki iliyopita kupinga kusaririshwa kwa gesi kutoka mkoani humo kupelekwa Dar es Salaam.


Rais Kikwete alisema kuwa tangu mwaka 2010 gesi nyingi imegundulika baharini na nchi kavu katika Mikoa ya Mtwara, Lindi na Pwani na kwamba utafutaji bado unaendelea na kuna matumaini kuwa gesi nyingi zaidi huenda ikagundulika.


Alisema hivi sasa Serikali inaandaa sera na sheria mpya ya gesi ili kuboresha zinazotumika wakati huu.  “Nia yetu ni kutaka kuhakikisha kuwa rasilimali hii adhimu inasimamiwa vizuri kwa manufaa ya nchi yetu na watu wake pamoja na kulinda maslahi ya wawekezaji,” alisema.


VITAMBULISHO

Kuhusu vitambulisho vya Taifa, alisema  serikali imeanza zoezi la kusajili watu na makazi kwa ajili ya kuandaa kutoa Vitambulisho vya Taifa kuanzia mwaka 2013 na kwamba Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida) ilifanya zoezi la majaribio katika mkoa wa Dar es Salaam na wilaya ya Kilombero ambalo lilifanikiwa. 

Alisema hivi sasa wanaendelea na zoezi hilo Zanzibar na kufafanua kuwa  maandalizi kwa ajili ya kutekeleza zoezi la kutoa vitambulisho nchi nzima kuanzia mwaka 2013 yanakwenda vizuri.  “Napenda kuwasihi wananchi wenzangu wakati

utakapofika kutoa ushirikiano unaostahili kwa maafisa watakaohusika na kukusanya taarifa na kutoa vitambulisho ili zoezi lifanikiwe ipasavyo.  Nawaomba muitumie vizuri fursa hii ya kujisajili na kupata vitambulisho,” alisema katika salamu hizo.

MCHAKATO WA KATIBA MPYA

Kuhusu mchakato wa Katiba Mpya, Rais Kikwete alisema Tume ya Mabadiliko ya Katiba inaendelea vyema na kuwa kwa sasa imekamilisha hatua ya kwanza ya kukusanya maoni ya mtu mmoja mmoja katika Mikoa yote nchini.
 Napenda kuchukua nafasi hii kuwashukuru wananchi kwa kujitokeza kwa wingi kutoa maoni. Zoezi linalofuata ni la kukusanya maoni ya makundi maalumu kuanzia mwezi  Januari, 2013.  Natoa wito kwa makundi hayo nayo kushiriki vizuri kwenye hatua hii muhimu.  Baada ya hatua hiyo kukamilika, Tume itaandaa Rasimu ya Katiba ambayo wanategemea itakuwa tayari mwezi Mei, 2013,” alisema. 

Alisema kwa mujibu wa ratiba ya Tume, rasimu hiyo itawasilishwa kwenye Vikao vya Mabaraza ya Katiba vitakavyofanyika kati ya mwezi Juni na Agosti, 2013 na kuongeza kuwa Tume itatangaza muundo na namna ya kuwapata Wajumbe wa Mabaraza hayo na utaratibu utakaotumika wakati wa kujadili na kutoa maoni juu ya Rasimu ya Katiba wakati huo ukiwadia.

 
“Baada ya kukamilika kwa Vikao vya Mabaraza ya Katiba, Tume itakamilisha Rasimu ya Katiba ambayo itachapishwa kwenye Gazeti la Serikali kama yalivyo matakwa ya Sheria.  Aidha, itachapishwa katika magazeti ya kawaida kwa wananchi kusoma. 

Mwezi Novemba, 2013 rasimu hiyo itawasilishwa kwenye Bunge Maalum kujadiliwa na kupitishwa.  Baada ya Bunge Maalum kupitisha Rasimu ya Katiba, Rasimu hiyo itapelekwa kwa wananchi kwa uamuzi wa mwisho kupitia kura ya maoni,” alisema.


Alisema ni matumaini ya serikali kuwa kama kila kitu kitakwenda kama inavyotarajiwa, tanzania itakuwa na Katiba Mpya iliyotokana na maoni na matakwa ya wananchi ifikapo mwaka 2014. 


“Tukifanikiwa kupata Katiba mpya wakati huo, tutafanya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 kwa kutumia Katiba hiyo. 


Inshallah, Mwenyezi Mungu atajaalia baraka zake, nia yetu njema itatimia.  Pamoja na hayo, natoa wito kwenu wananchi wenzangu kushiriki kwa ukamilifu katika hatua zote za mchakato ili tuweze kujenga muafaka kuhusu Katiba tunayoitaka,’ alisema.


MAREKEBISHO YA SHERIA

Akizungumzia marekebisho ya sheria, Rais alisema katika hotuba yake ya  mwisho wa mwezi wa Februari, 2012, alieleza kwamba mazungumzo baina ya Serikali na  vyama vya siasa na wadau wengine juu ya marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba.

“Tulikubaliana tushughulikie marekebisho ya Sheria hiyo hatua kwa hatua.   Tulikubaliana kuanza na mambo yanayohusu Tume ya Kuratibu na Kukusanya Maoni ya Wananchi ili Tume iundwe na ianze kazi.  Baada ya hapo tuangalie vipengele vinavyohusu Bunge Maalum na Kura ya Maoni,” alisema.  


Alisema kuwa walifanya hivyo kuhusu Tume ya Katiba na sasa wanajiandaa kuanza mazungumzo kuhusu ngwe iliyobaki yaani, Bunge Maalum na Kura ya Maoni.  “Kama mazungumzo yatakamilika mapema kunako Januari, 2013 mapendekezo hayo yatafikishwa katika Bunge la Jamhuri ya Muungano katika kikao cha Februari   kwa uamuzi.  Vinginevyo itakuwa  katika  Bunge  la  Aprili, 2013.


Kuhusu Kura ya Maoni, alisema Sheria ya Mabadiliko ya Katiba inaelekeza kuwa Kura ya Maoni itatungiwa Sheria yake maalum. “Ni matumaini yangu kuwa matayarisho yake yataanza mapema iwezekanavyo.  Nawasihi wananchi wenzangu, viongozi wa vyama vya siasa na asasi za kijamii tuwe watulivu, tuendelee kushirikiana katika mchakato huu wa Katiba mpaka tulifikishe jahazi ufukweni salama kwa mustakabali mwema wa nchi yetu na watu wake.,” alisema.


UHUSIANO NA WASHIRIKA

Kuhusu ushirikiano na washirika, Rais Kikwete alisema kuwa Katika mwaka 2012, uhusiano wa Tanzania na washirika wake wa maendeleo ulikuwa mzuri na uliendelea kuimarika. 

“Wote wanaridhika na kusifu kazi nzuri inayofanywa na Serikali yetu na ndiyo maana wanaendelea kushirikiana nasi na kutoa misaada ya maendeleo.  Aidha, wameonesha nia thabiti ya kuendelea kushirikiana nasi na kutusaidia katika harakati zetu za kujiletea maendeleo.,” alisema.


Aliwashukuru washirika wa maendeleo kwa mchango mkubwa wanaoendelea kutoa kwa maendeleo ya nchi.  Aidha, aliwahakikishia kuwa serikali inathamini sana ushirikiano wao na misaada yao na kuwahakikishia kuwa serikali itafanya kila iwezalo kudumisha ushirikiano huo. 


MATARAJIO YA 2013

Kuhusu matarajio ya mwaka 2013, alisema: “Tunatarajia kuwa mwaka 2013 utakuwa mwaka wa mafanikio makubwa zaidi katika nyanja zote kuzidi mwaka 2012.  Mambo yaliyokwama mwaka 2012 yatakwamuliwa. Ajira zitaongezeka kwa uwekezaji vitega uchumi kuongezeka na kuwajengea uwezo wajasiriamali wazalendo, ili waweze kujiajiri wenyewe na kuajiri wengine. 

Kwa ajili hiyo, Mifuko ya kusaidia wajasiriamali wadogo, wanawake na vijana itafufuliwa na kutengewa fedha nyingi katika bajeti ya Serikali.”


Alisema mwaka 2013 ni mwaka wa matumaini, hivyo kila mmoja anatakiwa kujituma na kutimiza wajibu wake na kuongeza kuwa maisha bora yatakuja kwa kila mmoja kutimiza wajibu wake ipasavyo.


“Kama kila mtu atafanya kazi kwa bidii na maarifa, na, kama kila mmoja wetu atajivunia matokeo ya kazi yake na siyo uhodari wa maneno yake ya uchambuzi wa hali.  Kila mtu achukie uvivu na tabia ya kulalamika pasipo kufanya kazi,” alisema rais Kikwete.

 
CHANZO: NIPASHE

author

This post was written by: Author Name

Your description comes here!

Get Free Email Updates to your Inbox!

Post a Comment

CodeNirvana
Chediel . Powered by Blogger.
© Copyright Rundugai Blog
Back To Top