Featured

    Featured Posts

    Social Icons

Loading...

JANUARY MAKAMBA ATAKA ELIMU BURE

*Asema kinachotakiwa ni kujipanga
*Asema vijana wataamua urais 2015

NAIBU Waziri wa Sayansi, Mawasiliano na Teknolojia, January Makamba, ametofautiana na sera ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), kuhusu suala la elimu kutolewa bure.

Alisema inawezekana Serikali kutoa elimu bure kuanzia elimu ya msingi hadi chuo kikuu, kwani kinachotakiwa ni uamuzi tu.

Mbali na hayo, alisema vijana ndio watakaoamua utawala mpya mwaka 2015, kama watajitokeza kupiga kura kwa sababu wao ni kundi kubwa.

January, ambaye pia ni Mbunge wa Bumbuli (CCM) mkoani Tanga, aliyasema hayo juzi, katika sherehe ya kumbukumbu ya aliyekuwa Mbunge wa Viti Maalumu, marehemu Regia Mtema (CHADEMA), mjini Dar es Salaam.

Marehemu Regia alifariki dunia Januari 14, 2012, kwa ajali ya gari katika eneo la Ruvu, mkoani Pwani.

Akitoa mada kuhusu nafasi ya vijana katika kuchochea maendeleo, alisema kama wakipata elimu, wana nafasi kubwa ya kufanya mabadiliko kwa sababu wana uthubutu.

Alisema, Tanzania inaweza kutoa elimu bure kuanzia shule ya msingi hadi chuo kikuu, kinachotakiwa ni kujipanga.

“Kulikuwa na mjadala mkubwa mwaka 2010 kuhusu elimu kutolewa bure au hapana, kwangu mimi ilikuwa ni kupoteza muda, elimu bure inawezekana Tanzania, ni suala la kujipanga na kuamua.

“Mtu yeyote mwenye elimu ya kiwango cha NBAA, anaweza kukutengenezea huo mpango na ikawezekana,” alisema January na kushangiliwa mno ukumbini.

Kuhusu nafasi ya vijana katika uchaguzi mkuu ujao 2015, alisema hatma ya chama chochote kuchukua madaraka iko mikononi mwa vijana.

Alisema wapiga kura wote, wanaotarajiwa kuandikishwa katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura ni vijana, hivyo wanayo nafasi ya kuamua kiongozi wa nchi.

“Tuliona mwaka 2005, watu wengi walijitokeza kupiga kura tofauti na 2010 ambapo kati ya watu milioni 20 waliojiandikisha, waliopiga kura ni milioni 8 tu, hii maana yake vijana wengi hawakupiga kura, licha ya uchaguzi huo kuwa na hamasa kubwa, lazima turudi nyuma tujiulize, labda demokrasia inahitaji nyanja mpya.

“Mimi ni shabiki mkubwa wa viongozi vijana, najua vijana ni rasilimali namba moja ya taifa, nilipozungumzia umri wa kugombea yalizuka maneno, tunajipigia debe, sikumaanisha kwamba ujana ndiyo sifa pekee ya kuwa kiongozi, lakini pia uzee siyo kashfa ya kuwa kiongozi.

“Tunaambiwa ninyi vijana bado, lakini tukumbuke nafasi nzuri ya kuongoza ni kuongoza, si vinginevyo, ni vema vijana tujitambue sisi ni kundi maalum na nchi hii ni ya kwetu,” alisema Makamba.

Akielezea jinsi alivyomfahamu Regia, alisema ni ukweli ulio wazi marehemu katika uhai wake aliwatendea haki vijana, walemavu na wanawake kwa kuonyesha aina ya uongozi wa kuthubutu.
OHN MNYIKA
Naibu Katibu Mkuu CHADEMA, John Mnyika, alisema chama hicho, kitaendelea kumkumbuka marehemu Regia kama mmoja wa waanzilishi wa falsafa ya Vuguvugu la Mabadiliko (M4C) pamoja na harakati za kudai kuandikwa kwa Katiba mpya.

Alisema miaka ya 2007/08, uongozi wa vijana wa chama hicho ulikuwa ukitafuta mbinu mbalimbali za kuwavuta vijana kupitia taasisi mbalimbali hivyo, walibuni jina la Youth for Change (Y4C).

Mnyika ambaye pia ni Mbunge wa Ubungo, alisema aliyepewa kazi hiyo ni marehemu Regia, ambaye aliifanya kwa ufanisi mkubwa na vijana wenye taaluma mbalimbali walijiunga kwa wingi katika chama hicho.

“Kumbukumbu ya utendaji wa Regia, haitafutika milele, M4C mnayoiona leo ina mkono wake na tayari alikwisha kuanzisha nyingine ya Kilombero (K4C).

“Mchakato wa kudai mabadiliko ya Katiba Mpya una mkono wake, ni mmoja wa walioshauri chama kiende kuzungumza na Rais Kikwete Ikulu badala ya kufanya maandamano.
WAZIRI KAIRUKI
Kwa upande wake, mgeni rasmi, Naibu Waziri wa Sheria na Katiba, Anjela Kairuki, alisema Regia alikuwa mwanaharakati na mbunge mwanamke ambaye atakumbukwa na vizazi vijavyo.

Alisema, Regia alijiamini na hakuwa mwoga, alijitambulisha kwa jina lake halisi katika mitandao ya kijamii, tofauti na viongozi wengine ambao wanatumia majina ya bandia ili wasijulikane.

“Licha ya uwezo wake mkubwa, Regia hakutoka katika familia ya kitajiri wala hakusoma katika shule kubwa za mabwanyeye, ni mfano wa kuigwa na kila mmoja wetu,” alisema Kairuki.

Ili kuendeleza ndoto za marehemu, marafiki wa Regia kupitia mtandao wa Jamii Forum na wengine wameanzisha Taasisi ya Regia Mtema Foundation, ili kuendeleza yote aliyokuwa akiyasimamia marehemu.

Kitabu cha ‘Kero za Wananchi’ kitachapishwa na kusambazwa hivi karibuni, ambapo Kairuki ameahidi kuchangia Sh milioni moja.

CHANZO:MTANZANIA
author

This post was written by: Author Name

Your description comes here!

Get Free Email Updates to your Inbox!

Post a Comment

CodeNirvana
Chediel . Powered by Blogger.
© Copyright Rundugai Blog
Back To Top