Askari wa jeshi la polisi wakiwa wanashusha magunia ya madawa ya
kulevya aina ya bangi mara baada ya kukamatwa eneo la Usa River wilayani
Arumeru yakiwa yanasafirishwa kwenye gari aina ya Fuso lenye namba za
usajili T.282 AAJ kuelekea Moshi

Kamanda
wa Polisi Mkoa wa Arusha Kamishna Msaidizi wa Polisi Liberatus Sabas
akiwaonyesha waandishi wa habari madawa ya kulevya aina ya bangi ambayo
yalikuwa kwenye magunia 97 yaliyokamatwa na askari wa jeshi hilo katika
eneo la Usa river wilayani Arumeru -Picha na Rashid Nchimbi wa Jeshi la
Polisi
---
Jeshi la Polisi mkoani hapa limemkamata mtu
mmoja akiwa na magunia 97 ya madawa ya kulevya aina ya bangi ambayo
yalikuwa yanasafirishwa toka mkoani hapa kuelekea Moshi. Akithibitisha
kutokea kwa tukio hilo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha Kamishna
Msaidizi wa Polisi Liberatus Sabas amesema kwamba, tukio hilo lilitokea
muda wa saa 10:00 alfajiri eneo la Usa River wilayani Arumeru.
Alisema
mafanikio hayo yametokana na ushirikiano mzuri kati ya jeshi hilo na
wananchi ambapo taarifa za tukio hilo zilitolewa na raia wema ambapo
askari wa jeshi hilo waliweka mtego eneo hilo na kufanikiwa kulikamata
gari aina ya Fuso lenye namba za usajili T. 282 AAJ.
Kamanda
Sabas aliongeza kwa kusema kwamba, ndani ya bodi ya gari hilo kulikuwa
na mboga aina ya kabeji iliyosambazwa vizuri huku chini ya mboga hiyo
kukiwa na madawa hayo yaliyokuwa kwenye magunia huku yakivingirishwa
kwenye mifuko ya “plastiki” kwa ndani.
Alisema katika gari hilo
kulikuwa na watu watatu na mara baada ya askari hao kulisimamisha dereva
pamoja na msaidizi wake walifanikiwa kukimbia huku mtu mmoja
aliyejulikana kwa jina la Praygod Marick (22) Mkazi wa Dar esalaam
akikamatwa.
Jeshi la polisi Mkoani hapa linaendelea kumhoji
mtuhumiwa huyo huku watuhumiwa wengine wakiendelea kutafutwa. Kwa mara
nyingine tena Kamanda huyo aliendelea kuwashukuru wananchi wa Mkoa huu
kutokana na ushirikiano wao mkubwa wanaoutoa kwa jeshi hilo na kuendelea
kuwasisitizia kuimarisha mahusiano na jeshi hilo.
Kwa muda wa
kipindi cha mwezi mmoja toka januari 07, 2013 mpaka hivi leo jeshi hilo
limeshakamata madawa ya kulevya aina ya mirungi magunia 372 katika
magari mawili tofauti na pia limeshakamata jumla ya magunia 117 ya
madawa ya kulevya aina ya bangi ambapo mwanzoni mwa wiki hii jumla ya
magunia 20 yalikamatwa yakiwa yanasafirishwa kwa kutumia wanyama aina ya
Punda maeneo ya Losoiti wilayani Longido.
Na
Rashid Nchimbi
Jeshi la Polisi- Arusha
Post a Comment