Featured

    Featured Posts

    Social Icons

Loading...

JK AWAPIGA VIJEMBE WANA CCM

Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete
MWENYEKITI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rais Jakaya Kikwete, amewapiga vijembe wajumbe wa Halmashauri Kuu ya chama hicho (NEC), ambao wameanza kampeni za kuwashinikiza wenzao wawakatae baadhi ya wajumbe wa Kamati Kuu watakaopendekezwa.

Akifungua semina ya wajumbe hao mjini Dodoma jana, Rais Kikwete alisema kuna baadhi ya wajumbe wameanza kukaa kwenye magenge kushinikiza wajumbe wengine wawakatae baadhi ya wajumbe watakaoteuliwa katika Kamati Kuu.

Alisema kwamba, ndani ya Halmashauri Kuu, hakuna mjumbe ambaye ni hatari kwa chama kwa kuwa wote wamepewa dhamana ya kuongoza.

Aliwataka wajumbe kutowasikiliza watu hao kwa kuwa orodha ya Kamati Kuu hadi sasa bado haijaandaliwa.

“Niwatahadharishe kwamba, asiwadanganye mtu kwamba orodha ndiyo hii, hawa ndiyo watakaochaguliwa, huyo anawapotezea wakati.

“Kama alikukuta unakunywa bia, mwongezee chupa ili anywe na akimaliza, aondoke kwa sababu orodha hatujaitengeneza bado.

“Rais ndiye nimekuja leo asubuhi, mimi Rais na Makamu Mwenyekiti, tutakaa, tena tutakaa kesho (leo), wala asiamke mtu akasema kwamba usiku huu nimepata orodha ni hii hapa.

“Msisumbuke kufanya mikutano ya kumuunga mkono fulani maana hakuna orodha.

“Wapo wengine wataanza kusema, waungeni mkono hawa, hawa ndiyo wanafaa na hawa ni hatari, inakuwaje wajumbe wa NEC wawe hatari kwa chama chetu”? alihoji Rais Kikwete.

Rais Kikwete aliwataka wajumbe wapya kujishirikisha kwenye mambo ya kujenga na siyo kujiunga kwenye makundi ya kukibomoa chama.

“Msikubali kushirikishwa kwenye mambo ya kubomoa na kutengeneza magenge mahali fulani ili mtu aharibikiwe, hili jambo halina tija, unajipa kihoro hasa pale uliyetaka aharibikiwe asipoharibikiwa.

“Kwa nini mnapenda kufanya biashara isiyo na maana, wekeza kwenye kitu cha maana, hii tabia ya kukaa kwenye vigenge fulani ili tumkatae fulani haifai, mnapanga kumkataa kwani orodha yenyewe iko wapi, lakini akili ni nywele kila mtu ana zake,” alisema.

Akizungumzia mada zilizotarajiwa kuwasilishwa katika semina hiyo, alisema ni pamoja na maadili ili taswira ya kimaadili ya viongozi hao iendane na taswira ya chama.

“Kiongozi unaonyesha taswira ya jamii na chombo unachowakilisha, kama mwenyewe maadili yako ni mabovu unaonyesha hata chombo unachowakilisha kipo hivyo hivyo.

“Siyo mjumbe wa NEC, unalewa mpaka unakuwa wa mwisho kuondoka baa halafu unamalizia na Kidumu Chama Cha Mapinduzi, hapo maana yake CCM itaonekana ni chama cha walevi,” alisema.

Rais Kikwete aliitaja mada nyingine iliyotarajiwa kujadiliwa kuwa ni mkakati wa kukuza ajira, kwamba chama hicho kinahusika na tatizo la ajira nchini kwa kuwa ndicho kinachoongoza nchi.

“Kwa sasa ajira za Serikali hakuna isipokuwa katika sekta ya afya na elimu na eneo pekee la kutoa ajira ni katika sekta binafsi, sasa tunapowaita wezi tutawekezaje katika sekta hii.

“Tunapojadili tatizo hili, tusilalamike badala yake kama viongozi, tutoe suluhisho vinginevyo itakuwa ni maneno ya jukwaani tu,” alisema.

Aliitaja mada nyingine katika semina hiyo kuwa ni nafasi na wajibu wa Mjumbe wa NEC na Mkakati wa kutekeleza maazimio ya mkutano mkuu wa taifa uliofanyika Novemba mwaka jana mjini Dodoma.

Aidha, alisema baada ya mkutano huo wa NEC, vikao vinavyofuata vitaanza kufanyika katika mikoa mbalimbali na kwamba mkoa unaotaka kuwa mwenyeji unaruhusiwa kupeleka maombi yake.

Kwa mujibu wa ratiba, katika semina hiyo ya jana, mada tatu zilitarajiwa kujadiliwa mada nyingine moja ingejadiliwa leo.

Ratiba hiyo inaonyesha kwamba, baada ya semina hiyo kumalizika leo, kikao cha NEC cha kuunda Kamati Kuu kitaanza leo saa kumi jioni.

Watoa mada katika semina hiyo ni pamoja na Makamu Mwenyekiti mstaafu, Pius Msekwa, Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara, Philip Mangula, Katibu Mkuu, Abdulrahman Kinana, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda na Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar, Balozi Seif Ali Idd.

NA MTANZANIA
author

This post was written by: Author Name

Your description comes here!

Get Free Email Updates to your Inbox!

Post a Comment

CodeNirvana
Chediel . Powered by Blogger.
© Copyright Rundugai Blog
Back To Top