Featured

    Featured Posts

    Social Icons

Loading...

KILA MTANZANIA SASA ANADAIWA SH.450,000

WATANZANIA wametumbukia katika mtego mpya katika deni ambalo limezidi kuongezeka kwa kiwango cha kutisha, licha ya ukali wa maisha wanaokabiliana nao.

Hali hiyo imetokana na kuongezeka kwa deni la taifa kutoka Sh trilioni 6.4 mwaka 2007/ 2008, hadi kufikia Sh trilioni 21 ambalo ni ongezeko la kiasi cha trilioni 15 kwa kipindi cha miaka mitano.


Taarifa ya Mtandao wa Madeni na Maendeleo Tanzania (TCDD), imeeleza kuwa deni hilo likigawanywa kwa idadi ya Watanzania milioni 45.9, inamaana kila Mtanzania anadaiwa Sh 450, 000.

Mkurugenzi Mtendaji wa TCDD, Hebron Mwakagenda, alisema Dar es Salaam jana kuwa, ongezeko hilo la deni ni kwa kipindi cha miaka mitano tu, jambo ambalo ni hatari kwa uchumi wa taifa.

Alisema kutokana na takwimu za Sensa ya watu na makazi iliyotangazwa na Rais Jakaya Kikwete Desemba mwaka jana, kiasi cha deni kinachodaiwa na taasisi za nje na ndani kinafanya kila Mtanzania kuwa na deni hilo.

“Takwimu za Sensa tulizotangaziwa na Rais mwaka jana, ni kwamba hivi sasa tuko Watanzania zaidi ya milioni 45, maana yake ni kwamba tukigawanya trilioni 21 kila mmoja atadaiwa Sh 450,000.

“Hebu fikiria Mtanzania anayeishi chini ya dola moja kwa siku, tunaambiwa anadaiwa Sh 450,000, fedha ambazo zilikopwa kwa niaba yake na waziri mwenye dhamana,” alisema.

Alisema TCDD ambayo kazi yake ni kufanya tafiti na kampeni dhidi ya madeni, imepeleka mapendekezo yake kwa Tume ya Katiba mpya ili taifa liwe na utaratibu wa kukopa tofauti na sasa, ambapo waziri wa Fedha ndiye mwenye dhamana ya kukopa kwa niaba ya Watanzania wote.


Maoni ya TCDD ambayo yalipelekwa kwa Tume ya Jaji Warioba ni pamoja na mpango wa Serikali kuhusu madeni kuwa wazi kwa wawakilishi wa wananchi, yaani wabunge na wawakilishi ili suala la kukopa liwe kwa niaba ya taifa na si jambo la siri.

Hoja nyingine ni kuwa Serikali iwajibike kutoa taarifa kwa Bunge kila baada ya miezi sita, kuhusu maendeleo ya deni pamoja na kuweka ukomo wa kukopa ili kuondoa uwezekano wa malimbikizo ya madeni yasiyokuwa na tija.

“TCDD haipingi taifa kukopa, isipokuwa si kila tatizo Serikali inakimbilia kukopa katika taasisi za nje na ndani, kwamba athari ya madeni ya ndani ni mbaya kuliko madeni ya nje.

“Deni la ndani hususan katika mabenki linapaswa kulipwa katika kipindi kifupi tofauti na madeni ya nje, ambapo ulipaji wake unachukua muda mrefu na nchi inaweza kujipanga kuyalipa,” alisema.

author

This post was written by: Author Name

Your description comes here!

Get Free Email Updates to your Inbox!

Post a Comment

CodeNirvana
Chediel . Powered by Blogger.
© Copyright Rundugai Blog
Back To Top