Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi, Philipo Mulugo
......................
Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi,
Philipo Mulugo, amewataka wadau wa elimu wasiitupie lawama serikali,
kufuatia matokeo mabaya ya kidato cha nne.
Badala yake, Mulugo alisema wadau wanapaswa kuwajibika kwa nafasi
zao, ili kuhakikisha kasoro zilizojitokeza mwaka huu hazitokei tena.
Mulugo alitoa kauli hiyo jana jijini Dar es Salaam, wakati wa
maonyesho ya elimu ya stadi mbalimbali yaliyoandaliwa na Shule ya
Sekondari Shaaban Robert na kuhusisha vyuo vya ndani na nje.
Maonyesho hayo, pamoja na mambo mengine, yamelenga kuwasaidia
wanafunzi wanaomaliza kidato cha sita, kupata uelewa kuhusu stadi
mbalimbali za maisha.
“Wanafunzi, walimu, wazazi na wadau wengine wa elimu, kila mmoja
anatakiwa kuwajibika kwa nafasi yake ili kuinusuru elimu,” alisema.
AWASHUKIA WALIMU WA ‘VODA FASTA’
Mulugo alithibitisha kuwa tatizo jingine linalopaswa kutazamwa ni
walimu wanaozalishwa kwa ajili ya kutoa elimu hiyo kwa wanafunzi, wakiwa
katika viwango kitaaluma.
“Unakuta mwalimu ana alama za chini, kisa tu amepata daraja la nne
akiwa na alama 28, anaenda vyuo vya ualimu kusomea ualimu, hii ni
hatari,” alisema. Mfumo huo ni maarufu nchini kama ‘voda fasta’.
WADAU WAZIDI KUIBUA MAPYA
Wadau kadhaa wameelezea sababu tofauti zinazochangia hali hiyo
inayodhihirisha mwelekeo hasi wa taifa katika nia ya kufuta ujinga na
kukabiliana na mabadiliko ya sayansi na teknolojia.
Mkuu wa Shule ya St Mathew wilayani Mkuranga mkoa wa Pwani, Lucas
Hassan, alisema kitendo cha serikali kubadili mitaala ya elimu wakati
walimu hawana taaluma, ilisababisha muendelezo wa ufaulu hafifu kwa
wanafunzi tangu 2009.
Alisema kutokana na mabadiliko hayo kufanywa ghafla, wakati walimu
hawajaandaliwa kwenye mfumo huo, ufaulu duni utaendelea kuwa janga la
taifa.
“Serikali iangalie eneo la tatizo husika bila kuwahukumu wanafunzi
moja kwa moja kuwa hawana akili, sio rahisi kwa idadi ya wanafunzi
waliofeli kuwa wote hawana akili, tatizo liko katika mfumo wa mitaala na
utaalamu wa walimu husika” alisema.
Aliongeza kuwa wakati serikali inalitafutia ufumbuzi tatizo hilo,
iangalie pia eneo la usahishaji mitihani kwa sababu, pamoja na
mabadiliko hayo bado halina wataalamu wenye sifa.
CHANZO:
NIPASHE
Post a Comment