Ndugu zangu,kupitia vyombo vyenu vya habari ninaomba
niueleze umma wa watanzania,hususani wadau wa mpira wa miguu,yafuatayo kuhusu
kuenguliwa kwangu.
Awali ya yote nieleze kusikitishwa kwangu na maamuzi
yaliyotolewa na kamati ya rufaa ya TFF ya kuniengua kugombea urais wa
TFF.Sikubaliani na maamuzi haya .
Katika kuniengua kamati ya rufaa ya uchaguzi ya TFF imetoa
sababu mbili (nanukuu magazeti ya jana tarehe 12/02/2013 maana hadi leo
sijakabidhiwa barua ya kuenguliwa).
1.
Kukosa uadilifu kwa kupinga waraka uliotolewa na TFF wa kubadili Katiba ya TFF
mwezi Desemba 2012.
2.
Kukosa uzoefu wa miaka mitano ya uongozi.
Ndugu zangu,kiini cha maamuzi ya Kamati ya rufaa dhidi yangu
ni pingamizi lililowekwa na mtu mmoja anayeitwa AGAPE FUE.Bwana Agape Fue
aliniwekea pingamizi katika kamati ya uchaguzi
akidai mimi nilipinga waraka wa kubadili katiba ya TFF na pia sina
uzoefu wa miaka mitano ya uongozi wa mpira.Kinyume na matakwa ya kamati ya
uchaguzi kama yalivyotangazwa kuwa mtoa pingamizi aje mwenyewe kutetea
pingamizi lake ,Bwana Agape Fue hakutokea mbele ya Kamati ya Bwana
Lyatto.Matokeo yake tarehe 31/01/2012
kamati ya uchaguzi ya TFF ilitoa maamuzi
ya ya kutupilia mbali pingamizi hili.
Bwana Agape Fue
hakuishia hapo kwa mara nyingine tarehe
06/02/2013 alikata rufaa kwenye kamati ya rufaa ya uchaguzi akidai kamati ya
uchaguzi haikumtendea haki. Rufaa hii haikuwa na anwani wala namba ya simu ya Bw.Agape Fue.Rufaa ilisikilizwa tarehe
10/02/2013 na maamuzi ya kukata jina langu yakatangazwa jioni ya tarehe
11/02/2013.
Mpaka leo najiuliza hivi huyu Bw. Agape Fue ni mwanaume
au ni mwanamke?(hakueleza kama ni Bwana
au Bibi Agape Fue). Agape Fue ni nani hasa? Anaishi wapi?Je ni Mtanzania au sio
Mtanzania maana kikanuni wasio
watanzania hawaruhusiwi kujihusisha na uchaguzi wa TFF (rejea kifungu cha 9 cha
kanuni za uchaguzi),pingamizi lake halikuambatana na udhibitisha wa uraia. Kwa
nini alichukua maamuzi haya? Sipati jibu. Iweje mtu achukue maamuzi mazito ya kumkatia mtu
rufaa kisha uishie kusaini karatasi na kuwaachia wengine wakusemee na usije
hata kushuhudia kinachoendelea kama kweli una maslahi na madai yako? Waandishi
wa habari mnisaidie kupata majibu.
Ndugu zangu ,mtoa pingamizi alidai haikuwa sahihi kupinga
azimio la kubadili katiba ya TFF kwa njia ya waraka.Naomba nisistize mambo
matatu:
1.
Wajumbe wa mkutano mkuu wa TFF wanawakilisha
matakwa ya vyama vilivyowatuma kwenda kwenye mkutano
mkuu wa TFF,na ndio maana chama cha mpira cha mkoa wa Kagera (KRFA)
kiliitisha kikao cha kamati ya utendaji
ili kamati iweze kutoa mwongozo
kwa wajumbe wake kuhusu nini kifanyike kuhusu waraka ulioletwa na
TFF,hivyo maamuzi yaliyotolewa ya kuukataa waraka huu yalikuwa ni maamuzi ya
chama cha mpira mkoa wa Kagera na wala hayakuwa ni maamuzi ya Jamal Malinzi,iweje
malinzi niadhibiwe kwa maamuzi haya,kwa nini usiadhibiwe mkoa mzima na mikoa
yote iliyopinga waraka?hii ni haki kweli? Siamini kama kuna mjumbe wa mkutano
mkuu aliyekiuka maamuzi ya kamati yake ya utendaji.
2.
Katika mchakato wa kubadili katiba kwa njia ya
waraka kilichokuwa kinagomba sio maudhui (content) ya mabadiliko ya Katiba bali
utaratibu uliotumika kubadili Katiba. Swali la msingi tulilojiuliza wajumbe wa
kamati ya utendaji KRFA ni kwamba je kwa
mujibu wa Katiba ya TFF kifungu 22 na kifungu 30 wapi katiba inatamka kuwa
inaweza kubadilishwa kwa njia ya waraka? Mpaka leo hilo jibu hakuna,labda
aliyeniwekea pingamizi atusaidie kupata jibu la swali hili. Katiba ya TFF iko
wazi kabisa inatamka kuwa Katiba
itabadilishwa kwa njia ya Mkutano Mkuu tu (General Assembly).
3.
Ni kweli FIFA iliagiza yafanyike mabadiliko ya
Katiba ya kuingiza kipendele cha ‘club licencing’ katika Katiba ,lakini je FIFA
katika agizo hilo ilisema Katiba ya TFF ivunjwe ili kutimiza azma hiyo?
Ikumbukwe kuwa mwaka 2004 FIFA iliagiza TFF iingize kwenye Katiba kipengele cha
Katibu Mkuu awe wa kuajiriwa badala ya kuchaguliwa,agizo hili lilitekelezwa kwa
kupitishwa na Mktano Mkuu wa TFF,iweje leo utaratibu huu ukiukwe? Hata majuzi
CAF walipotaka kubadili katiba ili Rais wa CAF atokane na wajumbe wa Kamati ya
Utendaji jambo hili lilitekelezwa kwa kuitisha mkutano mkuu wa dharura uliofanyika Seychelles majuzi. Katiba ndio
msingi mkuu wa uendeshajiwa TFF,nitaipigania siku zote.Huo ndio utaratibu,si
CAF si FIFA si Vyama vya mpira vya nchi,hakuna anayebadili Katiba kwa njia ya waraka,kama kuna mwenye
ushahidi aulete.
Kuengua jina langu eti kwa kuwa nilipinga
waraka wa kubadili Katiba sio uamuzi sahihi.
Kuhusu uzoefu wa miaka mitano katika
Uongozi:
Ikumbukwe kuwa katika uchaguzi mkuu wa TFF
mwaka 2008 niligombea na jina langu lilikatwa na kamati ya uchaguzi ya TFF.Nilikata rufaa katika
Kamati ya Rufaa ya TFF na kushinda . Hukumu hii ni halali hadi leo.Iweje leo
hii miaka minne baadae Kamati hiyo hiyo ya rufaa (kubadili majina ya wajumbe
sio kubadili taasisi) inione sina uzoefu?.Si hilo tu ,hata katika kujaza fomu
namba moja ya kugombea niliambatanisha vielelezo vyote vya uzoefu wangu ikiwa
ni pamoja na kudhibitisha kuwa katika kipindi cha miaka mine iliyopita nimekuwa:
-Mjumbe wa Baraza la michezo mkoa wa Dar es
salaam.
-Mwenyekiti wa kamati ya mashindano chama
cha mpira mkoa wa Pwani COREFA.
-Mjumbe wa mkutano mkuu wa mkoa wa Kagera
-Mwenyekiti wa chama cha mpira mkoa wa
Kagera
Hii ni pamoja na kuongoza Yanga 2002-2005.
Hivi katika nafasi hizi za uongozi ipi ni
ya kuongoza ‘bonanza’? Nimedhalilishwa sana.
HITIMISHO
Vyombo vya habari kupitia makala,tahariri
na maoni ya wasikilizaji/wasomaji/watazamaji vimesifia sana awamu mbili za
uongozi wa Bwana Leodeger Tenga.Bwana Tenga amesifiwa kwa umahiri wake wa
kuleta utulivu katika sekta ya mpira wa miguu Tanzania.Amesifiwa kwa kujenga
taasisi imara ambayo mhimili wake mkuu ni sekretarieti makini na kamati mbali
mbali zilizo imara .Let him rise to the occasion,muda wa kuonyesha uongozi
imara ni huu,historia itamhukumu kwa jinsi gani atasimamia suala hili,haki sio
lazima itendeke lakini pia inatakiwa ionekane inatendeka.
Kamati ya utendaji ya TFF inayo mamlaka ya
kubatilisha maamuzi haya kwa maslahi ya mpira wa Tanzania.Ninamshauri Rais wa
TFF aitishe kikao cha dharura cha kamati ya utendaji ili kijadili hali hii na
kunirudishia haki yangu ya kugombea urais wa TFF.
Nihitimishe kwa kuwaomba wadau wa mpira wa
miguu Tanzania wawe watulivu wakati
tukisubiri kupata ufumbuzi wa suala hili.
Mungu ibariki Afrika,
Mungu ibariki Tanzania.
Ahsanteni sana,
Jamal Emil Malinzi
Dar es salaam
13/02/2013
Post a Comment