Ndugu Mwenyekiti wa Umoja wa Wakuu wa shule za sekondari Tanzania[TAHOSSA] wilayani Hai,
· Ndugu Viongozi wa TAHOSSA,
· Ndugu Afisa Elimu wa wilaya,
· Wakuu wote wa Shule za sekondari wilayani Hai.
Awali
ya yote nianze kwa kumshukuru mwenyezi Mungu kwa kutupa uzima na
kutukutanisha hapa leo lakini pili kutuwezesha kuendelea na kazi katika
mwaka mpya wa 2013.
Kwa wale ambao hatujakutana pamoja na kwamba
huu ni mwezi Machi lakini kuna msemo wa kiingereza “Late better than
never”,hivyo basi nitumie fursa hii kuwatakia mwaka mpya mwema wenye
upendo na uwajibikaji.
Lakini jambo la pili nichukuwe fursa hii
kuwashukuru kwa kunialika kuzungumza machache kwenye Mkutano huu na
niwapongeze waandaaji kwa kuweza kuwakutanisha wakuu wa shule za
sekondari katika wilaya ya Hai.
Ingawa ni jumuiko la kawaida kwa kila mwaka lakini kupata idadi kubwa ni mafanikio makubwa hongereni sana.
Ndugu
Mwenyekiti, Mkutano huu unafanyika katika kipindi hiki ambacho mjadala
mkubwa hapa nchini ni matokeo ya kidato cha nne.Lakini Matokeo hayo ni
hitimisho tu ya matokeo mengine ya darasa la saba na yale ya kidato cha
pili.
Mnamo tarehe 18 Februari, 2013 Baraza la Mitihani la Taifa
lilitangaza matokeo ya Mtihani wa Taifa wa Kidato cha Nne ya mwaka
2012. Wanafunzi 397,132 walifanya mtihani huo na kati ya hao,
waliofaulu ni 126,851 yaani sawa na asilimia 34.5. Wanafunzi 240,903
ambao ni sawa na asilimia 65.5 hawakufaulu mtihani huo.
Matokeo
ya mitihani ya huo, yameshtua na kufadhaisha watu wengi nchini kwani
hata shule zinazofahamika kuwa na historia ya kufaulisha vizuri kama
vile seminari, shule za watu binafsi, za mashirika ya dini na sekondari
kongwe za Serikali ambazo hazina matatizo kama ilivyo kwa zile sekondari
za Kata, nazo safari hii hazikupata mafanikio kama ilivyo kawaida yao
Kwa
upande wa wilaya ya Hai katika shule za serikali watahiniwa 1,688
wamefeli kabisa kwa kupata sifuri.Kwa upande wa ufaulu,wanafunzi wawili
walifanikiwa kupata daraja la kwanza,wanafunzi watano daraja la
pili,wanafunzi 44 daraja la tatu na wanafnzi 555 daraja la nne.
Kwa
upande wa shule za binafsi,wao wamepata daraja la kwanza wanafunz
11,daraja la pili wanafunzi 44,daraja la tatu wanafunzi 111 na daraja la
nne wanafunzi 405 ilhali waliofeli ni wanafunzi 145.
Kwa upande
wa kidato cha pili ni vivyo hivyo,Wilaya ya Hai imefanya vibaya kwa
kupata wastani wa ufaulu wa asilimia 35 huku kiasi cha wanafunzi 940
wanalazimika kubakia katika kidato cha pili wakiwa miongoni mwa
wanafunzi 2,959 walifanya mtihani huo.
Ndugu mwenyekiti,Nyinyi
mliopo hapa ni wadau nambari moja wa elimu katika wilaya yetu ya Hai na
bahati nzuri mmekutana wakati hivi sasa kila mmoja wetu yuko katika
kuangalia tunafanya nini kuinusuru elimu yetu.
Uongozi wa
serikali katika wilaya umeshapanga kuwa na mkutano na wadau wa
elimukuzungumzia mikakati inayolenga kuinua hali ya elimu na kukomesha
kabisa dosari zote ambazo zinasababisha elimu yetu kwenda chini ama
kuzorota.
Ndugu mwenyekiti,mwezi uliopita nilikuwa na kundi la
wanafunzi wa vyuo vikuu mbalimbali wanaotoka wilaya ya Hai kupitia Umoja
wa wanafunzi wanaosoma vyuo vikuu kutoka wilayani Hai[HAUSO] niliwaomba
kwa kuwa wapo likizo basi wajitolee kufanyakazi za kuwafundisha wadogo
zao walioko katika sekondari mbalimbali,hivyo walikubali na vijana kumi
na tano walikuwa huko katika shule.
Lakini mbali ya kufundisha
niliwaomba wanafanyiye tathimini ya nini tunaweza kufanya katika
kuhakikisha kuwa tunainua hali ya elimu katika wilaya yetu ya Hai.
Kwa
sasa wote wamesharejea vyuoni lakini nilibahati kukaa nao na
wamenieleza mengi ambayo wamyabaini katika shule zetu za sekondari na
katika kuyashughulikia nimeona baadhi ni ya kuchukulia mkakati wa muda
mfupi ama wa haraka.
Hivi sasa kuna vijana wetu ambao wana miezi
michache sana kabla ya kuingia katika mitihani ya kumaliza elimu ya
msingi na huu ukiwa ni mwezi machi na niliwauliza hao vijana vipi hali
ipoje ? Nao walinijibu kwamba tusipochukuwa hatua matokeo ya kidato cha
nne kwa mwaka huu yanaweza kuwa mabaya maradufu ya matokeo ya mwaka
jana.
Hivyo nyinyi mkiwa wakuu wa shule kwa taratibu za halali
kabisa tuunganishe nguvu zetu katika kuchukuwa hatua za muda mfupi
ambazo zitawasaidia vijana ambao wanajiandaa kufany mitihani ya kumaliza
kidato cha nne wanafanya vizuri.
Kuna baadhi ya maeneo ambayo
waliyaona na mengine pia yamo katika taarifa mbalimbali za wakaguzi wa
elimu zinazofanyika kwa nyakati tofauti ambapo sisi kama wakuu wa shule
tunaweza kujadiliana hapa na kuweka mkakati wa kuchukuwa hatua kwa lengo
la kuwasaidia vijana wetu katika kujenga maisha.
Baadhi waliyoyaona vijana wetu wa vyuo vikuu ni pamoja na;
1. Migogoro ndani ya ofisi za shule yaani Staff Room.
Katika
mwezi mmoja wa kufanya kazi wamebaini kwamba katika baadhi ya shule
kuna maelewano madogo ama hakuna kabisa kati ya mkuu wa shule na makamu
mkuu wa shule pamoja na mwalimu wa taaluma.
2. Nidhamu ya mavazi kwa baadhi ya walimu.
Baadhi
ya walimu wameondoka kabisa katika mazoea ambayo tuliyajenga miaka ya
nyuma kwa katika jamii zetu walimu ni mfano wa kuigwa kwa kuingia katika
mavazi yasiyokuwa ya staa yakiwemo ya kushusha suruali chini maarufu
kama kata K na kuteremsha sketi chini.
3. Mtihani wa Mock kutokuwa na mfumo wa kuupima.
Mtihani
huu haufanyiwi tathimini nzuri katika ngazi ya wilaya ili uweze
kutumika katika kuwaandaa watahiniwa wanaotarajiwa kufanya mitihani ya
kitaifa baada ya miezi michache mbeleni
4. Wanafunzi kushindwa kuelewa Lugha ya kufundishia.
Bado
kuna tatizo kubwa kwa idadi kubwa ya wanafunzi wanaoanza kidato cha
kwanza kuelewa vizuri lugha ya kujifunzia ya kiingereza kutokana na
kutumia lugha ya Kiswahili kwa muda ya miaka saba katika shule za
msingi.
5. Wanafunzi kuingia katika mahusiano ya Kimapenzi.
Imebainika kuwa baadhi ya wanafuni wanaingia katika uhusiano wa kimapenzi na hivyo kushindwa kujikitia katika masomo.
6. Wazazi kushindwa kutoa ushirikiano kwa walimu.
Baadhi
ya wazazi wamekuwa na tabia ya kwenda shule kugombana na walimu mara
walimu wanapochukuwa hatua za kuwarekebisha wanafunzi wanaopooka.
7. Baadhi ya mada za masomo hazifundishwi kabisa.
Imebainika
kwamba baadhi ya topic katika masomo na hasa hisababti pamoja na masomo
ya sayansi hazifundishwi kabisa mpaka wanafunzi wanamaliza elimu ya
msingi
8. Kuingia kwa utandawazi na teknolojia ya kisasa.
Baadhi
ya wanafunzi kutumia vibaya teknolojia ya kisasa hususani simu za
mikononi na hivyo kujikita zaidi huko huku wakisahau jukumu lao kubwa
ambalo ni kujifunza na kuelewa kile wanachojifunza.
Vijana hao
walitoa baadhi ya mapendekezo yakiwemo ya mkakati wa muda mfupi wa
kuwasaidia vijana wetu ambao wanatarajia kufanya mitihani yao mwaka huu
ambayo ni pamoja na;
1. Kuwepo na utaratibu wa kubadilishana kufundisha baadhi ya
Topic
miongoni mwa walimu kwa walimu wa shule za jirani kwa maana wa shule
moja kwenda shule nyingine kutegemeana na umahiri wake katika topic
husika.
2. Kuongeza saa za kuwafundisha kidato cha nne.
Wanafunzi
wote wanaotarajia kufanya mitihani ya kidato cha nne waweze kuwahi
kufika shuleni saa moja asubuhi na baadaye warudi tena jioni baada ya
kutoka shule saa nane na nusu mchana
3. Kuandaliwa kisaikolojia.
Kutokana
na matokeo ya mitihani iliyopita kuwa mabaya basi kwa vyovyote vile
hali hiyo inaweza kuwaathiri baadhi ya watahiniwa watarajiwa na hivyo ni
vyema ukaandaliwa mfumo wa kuwajenga kisaikolojia.
4. Mkazo katika kufundishwa mbinu za kufanya mitihani.
Ratiba
ya kufundishwa jinsi ya mbinu za kufanya mitihani imekuwa fupi na hivyo
ni vyema walimu katika shule wakaangalia mkakati wa kuwafundisha
wanafunzi mbinu za kufanya mitihani
5. Uimarisha wa bodi za shule.
Kuimarisha
ama kufufua bdi za shule baada ya kubainika kwamba shule nyingi katika
wilaya ya Hai hazina kabisa bodi za shule ama zilizopo zinashindwa
kuwajibika.Kuwepo kwa bodi hizo kutaimarisha mahusiano kati walimu na
wazazi na kuweka mkakati wa pamoja na kuwasaidia wanafunzi.
6. Mpango wa kuwapa motisha walimu wanaofanya vizuri.
Kwa
walimu ambao watafanikiwa kuwezesha idadi kubwa ya wanafunzi kufanya
vizuri kwa kupata alama za juu za A ama B,basi kuwe na utaratibu wa
kuwazawadia na kutambua mchango wao katika elimu.
Ndugu
mwenyekiti,Haya ni baadhi tu ya mapendekezo ya muda mfupi ambayo nyinyi
kama wana taaluma na wadau namba moja mnaweza kuyajadili na
kuyatengenezea mapendekezo kwa ajili ya kuchukuwa hatua katika muda
muafaka.
Mapendekezo mengine ni ya muda wa kati na mrefu ambayo
tutayatengezea utaratibu baada ya kumaliza mchakato wa kukutana na wadau
pamoja na makundi mbalimbali ambayo kwa namna moja yanahusika katika
masuala ya elimu.
Wilaya inawategemea sana katika kuirejesha
katika hadhi ya miaka ya nyuma kama miongoni mwa wilaya ambazo zilikuwa
na wasomi katika miaka ya awali mara tua baada ya uhuru mwaka 1961
Ndugu
mwenyekiti baada ya masuala ya elimu ambayo hasa ndiyo jukumu lenu
kubwa kama wakuu wa shule za sekondari,naomba mniruhusu kuongelea baadhi
ya masuala ya kijamii kutokana na nyinyi mbali ya kuwa wakuu wa shule
lakini pia ni sehemu ya jamii na pia wengi wenu katika jamii mnanafasi
kubwa ya kukubaliwa na kuheshimika sana.
1. Kukithiri kwa tabia ya unywaji wa pombe ikiwemo pombe haramu ya gongo
Ndugu
Mwenyekiti,sote tunafahamu vijana tunaowafundisha ni sehemu ya kundi
kubwa la vijana katika wilaya yetu ambalo sasa hivi linaendelea
kuangamia kutokana na kukithiri kwa unywaji wa pombe ikiwemo pombe
haramu ya gongo.
Kwa mwananchi yeyote mwenye uchungu na wilaya
yetu ya Hai lazima suala hili litamgusa kwani hivi sasa ni janga la
wilaya na hali hii ikiendelea baada ya miaka mitano mpaka kumi ijayo
hatutakuwa tena na kizazi kilichoandaliwa vyema kupambana na changamoto
za maisha.
Lakini baya zaidi baadhi ya viongozi wenzetu katika
vijiji na vitongoji wamekuwa vinara katika kuhakikisha biashara hii ya
pombe haramu ya gongo inaendelea kudumu.
Rai yangu kwenu ni
kushirikiana katika kuhakikisha kwamba tunaweka mkakati wa kupambana na
watengenezaji,wauzaji na watumiaji wa pombe haramu ya gongo na
kuhakikisha imekwisha kabisa.
Lakini mbali na pombe haramu ya
gongo lakni kuna tatizo kubwa la matumizi ya pombe halali kwa muda kwa
idadi kubwa ya vijana zikiwemo zile zinazobebeka kirahisi ndani ya
mifuko ya plastki pamoja na pombe yetu ya asli ya mbege.
Pamoja
na kuwepo kwa sheria ambayo hivi sasa tumeanza kuitekeleza kwa nguvu
zote lakini nyinyi kwa upande wenu naomba niwaombe kwa nafasi zenu
kuendelea kuelimisha jamii athari za kunywa pombe kwa saa ishirini na
nne ndani ya siku saba za wiki katika siku thelathini za mwezi.
Sisi
kwa upande wetu tutaendelea kusimamia sheria ya saa za unywaji wa pombe
ambapo ni saa tisa jioni mpaka saa tatu usiku kwa siku za katikati ya
wiki na saa nne kwa mwisho wa wiki kwa maana jumamosi na jumapili.
2. Utunzaji wa mazingira
Ndugu
Mwenyekiti,mazingira ndiyo uhai wetu.Kwa kutambua hilo na kasi kubwa
iliyojitokeza ya ukataji wa miti,serikali katika mkoa wa kilimanjaro kwa
nia nzuri kabisa ilisitisha vibali vya ukataji wa miti kwa ajili ya
mbao na magogo.
Maamuzi haya hayakuchukuliwa kwa ajili ya manufaa
ya mtu binafsi au kwa lengo la kuwakomoa wananchi,bali kuthamini ustawi
wa maisha ya jamii yote ya mkoa wa Kilimanjao wakiwemo wakazi wa
wilaya ya Hai.
Babu zetu walifanyakazi kubwa ya kupanda miti kwa
kasi na ndiyo maana wengi wetu wakati tunazaliwa tulikuta wilaya ya Hai
ikiwa na mazingira ya kuvutia yenye mvua za kutosha zilizotusaidia
kuendesha shughuli zetu za kilimo na ufugaji kwa ufanisi mkubwa.
Kibaya
kilichojitokeza hivi sasa bila ya kuthamini jitihada za wazazi wetu za
kupanda miti na kuitunza hivi sasa tumekuwa tukikata miti hii kwa kasi
kubwa sana na kuharibu mazingira hali ambayo imesababisha hata msimu wa
mvua usiwe wa uhakika huku joto likiongezeka maradufu.
Kutokana
na hali hiyo ndipo serikali mkoani Kilimanjaro ikachukuwa maamuzi magumu
ya kusitisha vibali vya ukataji wa miti kwa ajili ya mbao na magogo.
Ndugu
mwenyekiti,cha kushangaza katika maeneo mengi ya wilaya ya Hai bado
kuna baadhi ya vinara wa ukataji wa miti miongoni mwao ni viongozi
wenzetu.
Wanaofanya vitendo hivi wanafahamika hivyo ombi langu la
pili kwenu ni kuomba ushirikiano wenu katika kuwafichuwa wanaofanya
hivyo kwa kuwasiliana name moja kwa moja lakini pia kuendelea kutoa
elimu kuhusu umuhimu wa kuendelea kutunza mazingira.
Lakini sanjari na hilo hivi sasa tupo katika kampeni ya upandaji wa miti katika maeneo mbalimbali.
Tumeagiza
na kuwaandikia kama wakuu wa shule kuanzisha kitalu ama bustani ya
miche ili msimu wa mvua utakapoamza basi tusipate tatizo la miche.
Kama
wakuu wa shule hakikisheni mnakwenda kusimamia zoezi la maandalizi ya
upandaji wa miti kwa kuwa na vitalu vya miche vya ya kutosha kwa maana
mvua zitapoanza kunyesha basi tuanze mara moja zoezi la upandaji wa
miti.
1. Utawala bora
Ndugu Mwenyekiti,Changamoto ya
masuala yenye mwelekeo wa utawala bora limekuwa tatizo kubwa sana katika
wilaya yetu kuanzia sisi tulioko ngazi ya wilaya mpaka viongozi wetu
walioko katika ngazi za vijiji.
Aidha Uwajibikaji limekuwa tatizo
kubwa sana likitugusa sisi viongozi wa kisiasa mpaka wataalamu wetu wa
ngazi mbalimbali huku tatizo kubwa likiwa kusahau majukumu yetu.
Kwa
upande wa changamoto hii nitaieleza katika maeneo mawili tu ambayo sisi
kama wakuu wa shule na wanajamii katika maeneo yetu tunaweza kusaidia
kwa kiasi cha juu sana.
Changamoto ya kwanza inahusu ufanyikaji
wa vikao vya kisheria katika ngazi za vijiji na kata.Hilo limekuwa
tatizo kubwa sana katika wilaya yetu.Kila unapita katika vijiji
malalamiko makubwa ni ufanyikaji wa mikutano ya vijiji na hasa ajenda
inayohusu kusomwa kwa taarifa ya mapato na matumizi.
Kwa uchache sana pia tuna tatizo la ufanyikaji wa mikutano ya kamati za maendeleo za kata yaani WDC katika baadhi ya kata.
Changamoto
hizo zote siyo siri zinafahamika vizuri kwa maofisa wetu wa ngazi za
tarafa na kata hususani kwa ufanyikaji wa mikutano mikuu ya kijiji na
kwa ile ya ngazi ya kata zinafahamika katika halmashauri yetu ya wilaya.
Sasa
tunalenga kumaliza tatizo la ufanyikaji wa vikao vya kisheria katika
ngazi ya vijiji.Mkiwa wakuu wa shule mnanafasi kubwa ya kushauri na
kuelimisha pia kama wasomi hivyo nawaombeni ratiba za vikao vya kisheria
katika vijiji vyenu zinafanyika vikiwa na ajenda zote muhimu,mahudhurio
na maamuzi.
Lakini kwa upande wa masuala ya utawala bora
nimalizie kwa kuwataka nyinyi wakuu wa shule kutojitenga na miradi
mbalimbali na badala yake kuhakikisha mnafuatilia kwa ukaribu miradi
yote inayotekelezwa katika maeneo yenu iwe ndani ya shule ama katika
ngazi ya vijiji.
Naomba nimalize kwa kuwashukuru tena kwa kunipa
heshima kubwa ya kunialika katika mkutano wenu huu ambao umenipa fursa
kubwa ya kuzungumza nanyi kwa mapana kuhusiana na masuala ya elimu nnchi
kwa ujumla pamoja na katika wilaya ya Hai
Nawatakia mafanikio katika mkutano wenu,Mungu ibariki wilaya ya Hai,Mungu ibariki Tanzania, asanteni kwa kunisikiliza
Post a Comment