Featured

    Featured Posts

    Social Icons

Loading...

BUNGE LAMPUUZA CAG

*Lapinga hoja zake kuvunjwa kamati ya POAC
*Wabunge wachachamaa, wamuunga mkono
Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Ludovick Utou
OFISI ya Bunge imetetea uamuzi uliofanywa na Spika, Anne Makinda wa kuivunja Kamati ya Bunge ya Mashirika ya Umma (POAC). Taarifa hiyo imekuja siku mbili baada ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Ludovick Utouh, kukosoa uamuzi huo.
Utouh alitoa shutuma hizo mara baada ya kuwasilisha taarifa yake bungeni, akisema kuwa spika alifanya makosa kuivunja kamati hiyo.

Akizungumza na MTANZANIA mjini hapa jana, Mkurugenzi wa Shughuli za Bunge, John Joel alisema uamuzi wa kuivunja kamati hiyo ni sahihi na wala hakuna makosa yoyote.

Hata hivyo, Joel alimtaka CAG kuelewa kwamba, mambo yaliyopo katika ripoti yake hayawezi kufanyiwa kazi yote kama anavyofikiri.

“Uamuzi uliofanywa na Kamati ya Kanuni ni sahihi kabisa na wala hakuna kosa lililofanyika kuhamisha kazi za POAC kwenda PAC.

“Haina maana kwamba, kila kitu kilichomo katika ripoti ya CAG lazima kifanyiwe kazi, hapana. Kinachofanyika ni Bunge kujielekeza katika mambo muhimu, utaratibu huu ndio unaofanyika duniani kote.

“Bunge lazima lifanye kazi kisayansi na si kwa mazoea, kwani tabia ya kufanya mambo kwa mazoea ndiyo imekuwa ikisababisha baadhi ya mambo kutokwenda vizuri.

“Alichosema CAG ni mtazamo wake, yeye ndivyo anavyoona hivyo, ingawa bado nasema hakuna makosa katika kufanya mabadiliko hayo,” alisema Joel.
 Msimamo wa CAG
Utouh alimshutumu spika wakati akizungumza na waandishi wa habari, mara baada ya ripoti ya mwaka unaoishia Juni, 2012 kuwasilishwa bungeni mwishoni mwa wiki.

Utouh alisema, shughuli za kamati hiyo ambazo kwa sasa zimehamishiwa kamati ya PAC, hazitatekelezwa hadi Mungu atakaporudi.

CAG alisema, sababu zilizofanya kamati ya POAC kuundwa wakati huo bado zipo, hivyo kwa sasa inatakiwa miujiza ili PAC iweze kufanya kazi kwa ufanisi.

“Utaratibu wa kuunganisha kazi za kamati ya PAC hautakidhi matarajio ya wadau ya uwajibikaji kwa kuwa kamati hii itazidiwa na ukubwa wa majukumu.

“Hivyo basi, ofisi yangu bado inashauri kuona uwezekano wa kurudisha kamati hii hata kama kutakuwa na haja ya kuibadilisha jina,” alisema CAG.
 Wabunge wamuunga mkono CAG
Baadhi ya wabunge waliozungumza na MTANZANIA, nao walikosoa hatua ya kamati hiyo kuvunjwa huku wakimuunga mkono CAG.

Mbunge wa Mpanda Mjini, Said Amour Arfi (Chadema), alisema kutokana na mabadiliko hayo ni wazi kuwa kamati ya PAC itaelemewa na majukumu.

Arfi alisema yalifanyika makosa kuivunja kamati hiyo kwani kamati ya PAC haina uwezo wa kufanya kazi zake za msingi kisha kufanya kazi za kamati nyingine iliyovunjwa.

“Mimi nakubaliana na CAG, kwamba ile kamati ya POAC iliondolewa kimakosa kwa sababu kanuni hazikufuatwa.

“Kwa maana hiyo, kamati hiyo irudishwe japokuwa kikanuni bado ipo kwani iliondolewa bila kufuata utaratibu,” alisema Arfi.

Mbunge wa Sikonge, Said Mkumba (CCM), alipinga kamati hiyo kuvunjwa na kusema kuwa kamati hiyo inatakiwa irudishwe kutokana na sababu zilizoiunda.

“Ile ni kamati muhimu sana, kwani nchi hii ina mashirika mengi ambayo yanatakiwa yakaguliwe kwa umakini wa hali ya juu vinginevyo ipo siku yatakufa.

“Kwa hiyo, naungana na CAG ile kamati irudishwe vinginevyo ipo siku tutalaumiana baada ya mashirika kufa,” alisema Mkumba
NA MTANZANIA

author

This post was written by: Author Name

Your description comes here!

Get Free Email Updates to your Inbox!

Post a Comment

CodeNirvana
Chediel . Powered by Blogger.
© Copyright Rundugai Blog
Back To Top