SERIKALI imesema mabadiliko ya utangazaji kutoka analojia kwenda dijitali hayaepukiki.
Kutokana na hali hiyo imewataka wadau wote kushirikiana katika
mchakato mzima kama ilivyokubalika kupitia vikao mbalimbali
vilivyofanyika tangu mwaka 2005.
Akitoa tamko la serikali kuhusiana na uhamaji huo jana, Waziri wa
Sayansi, Mawasiliano na Teknolojia, Profesa Makame Mbarawa alisema
serikali imejiridhisha kuwa mchakato wote wa kuelekea mfumo huo wa
utangazaji ulifanywa kwa umakini mkubwa na kwa muda wa kutosha na kuwa
elimu imetolewa na inaendelea kutolewa.
“Ni dhahiri kuwa watoa huduma za miundombinu ya dijitali waliopewa
leseni tangu 2010 wameendelea na wajibu wa kuweka mitambo ya digitali
sehemu mbalimbali nchini na zoezi linaendelea vizuri,” alisema Profesa
Mbarawa.
Alisema serikali haitavumilia kikundi au mtu yeyote atakayeonekana
kupotosha au kufifisha mchakato wa kuhamia katika mfumo wa utangazaji wa
dijitali.
Aidha, alisema serikali imeiagiza Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania
(TCRA) kuendelea na utaratibu, ratiba ya uzimaji wa mitambo ya analojia
kama ilivyotolewa na serikali.
Pia serikali imeiagiza mamlaka hiyo kupitia kamati ya maudhui
kuchunguza endapo kauli zilizotolewa na baadhi ya wamiliki wa vyombo vya
habari kwa kutumia muda mrefu kuelezea kauli zao katika vyombo vyao vya
habari kama hawakukiuka sheria na kanuni za Utangazaji kwa nia ya
kupotosha umma kwa kusudio la kudhoofisha maamuzi hayo ya serikali.
Katika siku za hivi karibuni, kumekuwapo na kauli mbalimbali
zinazotolewa na baadhi ya wamiliki wa vyombo vya habari na hasa wa
utangazaji wakiilaumu na kuishutumu serikali kuhusu uamuzi wa kuhamia
katika mfumo wa dijitali.
Waziri Mbarawa alisema kauli hizi sio za kweli, zinapotosha ukweli na
hali halisi na pia zinalenga kuchochea wananchi kutokubaliana na uamuzi
wa serikali.
Waziri Mbarawa aliwaomba wananchi kupuuza upotoshaji unaofanywa kuhusu
ukweli wa mabadiliko ya mfumo wa utangazaji wa kutoka analojia kwenda
dijitali.
Post a Comment