Moshi. Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) mkoani
Kilimanjaro umesema hautafanya maandamano yoyote yasiyo na tija na
badala yake wataweka mikakati ya kukabiliana na changamoto
zinazowakabili ikiwamo ya ukosefu wa ajira.
Mwenyekiti wa UVCCM Mkoa wa Kilimanjaro, Frederick
Mushi alitoa ahadi hiyo juzi wakati akihutubia mkutano wa hadhara
katika Viwanja vya Mawazo mjini Moshi baada ya kuzindua tawi jipya la
vijana wa eneo hilo.
Mushi alielezea kusikitishwa kwake na baadhi ya
wanasiasa wanaowatumia vijana kufanya maandamano ili kutimiza malengo
yao ya kisiasa huku vijana wakipata shida.
Alisema vijana hao wa mawazo ni mfano wa kuigwa na uamuzi wao utawafungulia milango ya kujiletea maendeleo hapo baadaye.
Kwa upande wake, Kamanda wa Vijana UVCCM Wilaya ya
Moshi mjini, ambaye pia ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM (NEC)
kupitia Moshi mjini, Aggrey Marealle alishauri vijana hao kuanzisha
Chama cha Kuweka na Kukopa (Saccos).
Shambe Sagaf, ambaye alimwakilisha Marealle
alisema kuwa njia ya pekee ya vijana kupambana na tatizo la ajira ni
kujiunga na kuanzisha vikundi vya maendeleo ambapo aliahidi kuwaunga
mkono ili waweze kutimiza azma yao.
Mwenyekiti wa UVCCM Moshi Mjini, Abdalla Thabit
alisema mapema kikundi hicho kilianzishwa na vijana hao kikiwa na lengo
la kujitegemea kwa kuanzisha miradi mbalimbali.
NA MWANANCHI
NA MWANANCHI
Post a Comment