Featured

    Featured Posts

    Social Icons

Loading...

SUGU ALICHAFUA BUNGE

*Hotuba yake yang’ata, yadaiwa kujaa uchochezi
*Spika aliahirisha Bunge, waandishi wamshangaa waziri
* Tundu Lissu, Anne Kilango nusura wazichape nje ya Bunge
Mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi (Sugu)
HOTUBA ya Kambi rasmi ya Upinzani jana ilichafua hali ya hewa bungeni, hatua iliyomlazimu Spika, Anne Makinda kuahirisha kikao cha Bunge asubuhi kabla ya muda rasmi.

Hatua hiyo ilikuja wakati msemaji wa kambi hiyo wa Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Joseph Mbilinyi maarufu kama Sugu alipokuwa akisoma hotuba hiyo iliyodaiwa kujaa lugha ya uchochezi. Hotuba hiyo ilisomwa muda mfupi baada ya Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Dk. Fenella Mukangara kuwasilisha makadirio ya bajeti ya wizara yake.

Spika aliahirisha kikao cha Bunge saa 5: 30 asubuhi tofauti na muda wa kawaida wa Bunge kuahirishwa saa 7: 00 mchana hadi saa 11:00 jioni.
Dalili za kuchafuka kwa hali ya hewa zilianza kujionyesha mapema wakati Makamu Mweyekiti wa Kamati ya Bunge ya Maendeleo ya Jamii, Said Mtanda aliposoma maoni ya kamati yake.

Wakati Mtanda akiwasilisha maoni ya kamati yake, muda wote Kaimu Mnadhimu upande wa Serikali, Dk. Mary Nagu na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Frederick Werema walijikita katika hotuba ya kambi ya upinzani.

Spika Makinda aliliahirisha Bunge baada ya kupokea mwongozo ulioombwa na Mbunge wa Mbozi Mashariki, Godfrey Zambi (CCM) akilalamikia hotuba hiyo.

Zambi alisimama baada ya Dk. Nagu kushindwa kufanikisha mpango wa kumzuia Sugu aliposimama mara mbili, huku Mnadhimu wa Kambi ya Upinzani, Tundu Lissu akimvunja nguvu kwa kusimama sambamba na Dk. Nagu. 
 Mwongozo wa Spika
Akiomba mwongozo huo, Zambi alitaka kujua iwapo ni halali kwa hotuba hiyo kuendelea kusomwa wakati imejaa maneno ya uwongo na mengine ya uchochezi.

“Nimesimama kwa mujibu wa kanuni namba 68 (1) na kanuni nyingine ya 64 (A). Hotuba hii ina taarifa ambazo hazina ukweli.

“Kuanzia ukurasa wa 1 hadi wa 14, hotuba hii imejaa uchochezi. Katika ukurasa wa pili, hotuba inasema hivi, alisema Zambi huku akinukuu hotuba hiyo:

“Tanzania imegeuka chini ya usimamizi wa wizara na Serikali hii ya CCM kuwa taifa linaloteka nyara wanahabari, kuwatesa kwa kuwang’oa kucha na meno. Kuwatoboa macho, kuwamwangia tindikali na hata kuwaua,” mwisho wa kunukuu.

Zambi aliendelea kusema: “Kauli hii ni nzito dhidi ya Serikali ya CCM, hatuwezi kunyamazia hotuba hii yenye uchochezi na watu wanaendelea kuisikiliza.” 
Spika aliahirisha Bunge
Spika Makinda aliikubali hoja hiyo na aliahirisha Bunge hadi saa 11 jioni i kutoa fursa kwa Kamati ya Kanuni kupitia hotuba hiyo kuona iwapo inafaa kuendelea kusomwa au ifutwe.

“Waheshimiwa wabunge sisi wenyewe juzi hapa tumepitisha Azimio la Bunge kupinga lugha za uchochezi zinazofanywa humu ndani… naahirisha Bunge hadi jioni ili Kamati ya Kanuni ikapitie hotuba hii,” alisema.
 Lissu, Kilango nusura wazichape
Baada ya Bunge kuahirishwa, nje ya ukumbi hali haikuwa nzuri baina ya Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu na Mbunge wa Same Mashariki (CCM), Anne Kilango Malecela.

Mtafaruku huo uliibuka baada ya Kilango kusikika akimtuhumu Lissu kwa uchochezi, akisema kwamba amekuwa mbunge pekee anayeongoza kwa vurugu.

Maneno hayo hayakumfurahisha Lissu ambaye alishindwa kuvumilia na kumgeukia Kilango kwa nguvu huku baadhi ya wabunge wakishuhudia na wengine wakimzuia Lissu.
 Waziri awatibua waandishi wa habari
Wakati huohuo, waandishi wa habari wamemlalamikia Dk. Mukangara kwa hotuba yake kujikitaza zaidi kuzungumzia vyombo vya habari vya Serikali na kusahau kundi la waandishi katika sekta binafsi.

Mbali na hilo, nyongo ya waandishi hao ilitibuka zaidi kutokana na hotuba hiyo kushindwa kutambua changamoto mbalimbali ambazo waandishi wa habari wanakumbana nazo katika utendaji wao kazi.

Wakati hotuba hiyo imejaa simulizi za miradi ya mwenge, vyombo vya habari vya Serikali na mabaraza ya vijana, waziri ameshindwa kutambua vitendo vya kinyama wanavyofanyiwa waandishi ikiwamo kuuawa, kutekwa na kuteswa.

Miongoni mwa matukio mabaya ni tukio la kuuawa kwa aliyekuwa mwandishi wa habari wa Channel Ten mkoani Iringa, Daus Mwangosi.

Mengine ni kutekwa na kuteswa kwa Mhariri Mtendaji wa Kampuni ya New Habari (2006) Ltd na Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Absalom Kibanda.

Waandishi wa habari walitoka ukumbini wakiwa na hasira kutokana na hotuba hiyo kuonyesha ubaguzi wa dhahiri na kushindwa kutambua matukio mabaya wanaofanyiwa waandishi.

Baadhi ya waandishi walishangaa hotuba hiyo kwa jinsi ilivyoandaliwa ambako baadhi yao walisikika wakisema:

“Kwa mtindo huu ni bora tuhamishiwe wizara ya mifugo tunaweza kutendewa haki kuliko wizara hii ya habari.”

Akizungumza nje ya ukumbi wa Bunge, Katibu wa Jukwaa la Wahariri wa Habari (TEF), Nevile Meena, alisema waziri amekwepa wajibu wake kwa kushindwa kutambua changamoto za waandishi wa habari.

“Waziri amekwepa wajibu wake, ukiangalia hotuba nzima ina chembechembe za kuwabagua waandishi wa habari, nchi yetu hivi sasa imebadilika hatutegemei vyombo vya Serikali peke yake.

“Kuhusu hotuba ya kambi ya upinzani mimi sioni kama kuna uchochezi ndani yake, hotuba ya Sugu imejaribu kutoa taswira kuhusu maisha na usalama wa waandishi wa habari nchini.

“Hivi tunavyozungumza waziri anatambua mwenzetu Kibanda hana jicho, bado yupo nje ya nchi akiendelea na matibabu.

“Suala la Kibanda kutekwa ni fact (ukweli) hakuna jambo la kubuni, suala la kuuawa Mwangosi ni fact (kweli) wengine wamepigwa risasi ingawa bado wanaishi yote haya ni facts.

“Kwa mwandishi makini aliyekuwapo mule ndani ataona kuwa suala la kuzima hotuba ya upinzani lilikuwa ni jambo lililopangwa, sisi wengine ni wazoefu wa kuripoti Bunge tunaelewa, ingawa leo tumekuja kama wageni.

“Waziri kuzungumzi TBC alikuwa na haki ya kufanya hivyo kwa kuwa ni shirika lililopo chini yake, lakini tulitarajia Serikali ingeeleza mikatai yake kuhusu suala la usalama wetu. Hotuba ya waziri ina ukakasi ndani yake,” alisema.
 Hotuba ya Sugu
Awali akisoma hotuba yake, Sugu alisema kutokana na vitendo vya ukatili dhidi ya waandishi wa habari ni wazi kuwa Tanzania imeingia rasmi katika orodha ya fedheha (The list of shame) ya mataifa ambayo taaluma ya habari ni taaluma ya hatari.

“Kwa mujibu wa taarifa ya Kamati ya Kulinda Waandishi wa Habari Duniani (CPJ) iliyotolewa mwaka 1992, Tanzania imeingizwa kwenye orodha ya nchi 20 ambazo ni hatari kwa waandishi wa habari.

“Kwa mujibu wa taarifa hiyo, tishio kubwa kwa waandishi wa habari duniani ni kuuwawa kwa kutekwa, kuteswa na kutishiwa maisha” alisema.

Sugu alisema taarifa hiyo ya CPJ inaungwa mkono na ushahidi wa matukio mengi yanayodhihirisha kwamba maisha ya waandishi wa habari wa Tanzania yapo hatarini kutokana na vitisho kutoka kwa watendaji wa Serikali ambao hawataki kukosolewa.

“Miezi sita baada ya Jeshi la Polisi kumuua Daud Mwangosi, mwandishi mwingine mwandamizi na Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri, Absalom Kibanda alitekwa nyara na kuteswa vibaya nje ya nyumba yake,” alisema.
 NA MTANZANIA
author

This post was written by: Author Name

Your description comes here!

Get Free Email Updates to your Inbox!

Post a Comment

CodeNirvana
Chediel . Powered by Blogger.
© Copyright Rundugai Blog
Back To Top