Kaka zangu Maggid Mjengwa na Ansbert Ngurumo, mimi pia huandika mara
chache tu, nyinyi ni kati ya waandishi ambao mimi huwasoma sana.
Binafsi nakubaliana na Maggid na sitatofautiana sana na Ansbert. Kuwa,
wanasiasa tusiwatumie vijana vibaya, wengi hawana elimu, hawajui lolote
na wanaburuzika kirahisi.
Tufungue njia za “dialogue” zaidi kuliko mapambano ambayo hayana mwisho mwema.
Pamoja na CCM kuishika pabaya nchi hii, pana haja tunaopambana CCM
iondoke tuwe “very tactical". Mara nyingi tuwekeze nguvu kubwa katika
kutafuta masuluhisho ya kudumu.
Hivi karibuni nilikuwa LIWALE
na Ruangwa, sikuona aibu, niliwaeleza wananchi kuwa kudai haki zao ni
muhimu, lakini isifikie kuanza kuchoma majumba na magari ya
walioshikilia haki zao.Tukianza hiyo michezo ya kuchomeana itapasa
visasi vianze, visasi havina macho, vitatupeleka pabaya. Pamoja na
mapambano ya kudai haki,amani haikwepeki kwa sababu ikikosekana ina
maana hata harakati za kudai haki hazina pa kufanyikia.
Leo
Tanzania ikigeuzwa kuwa uwanja wa vita na mapambano kila kona ya nchi,
hatutakuwa na vyama vya siasa tena, tutakuwa na vikundi vya kupigana kwa
kutumia silaha kila kona. Hatutapeperusha bendera za vyama.
Na
jambo tunalosahau ni kuwa,hivi sasa tukiwafanya vijana wetu wawe
"rude", "bully" and "cruel" kwa kisingizio cha kudai haki, Siku CCM
itakapoondoka na ikaingia CUF, CHADEMA au mwingine, vyama hivi vipya
vitarithi madaraka ya nchi na vijana hao hao RUDE,BULLY and CRUEL. Hivi
sasa ndo tukijifanya machampioni wa kuwaeleza vijana kuwa ajira
zinapatikana “after 3 days”. NCHI HII TUTAIPIGA KIBERITI WENYEWE....
Sera za vyama vitakavyoongoza dola zijikite katika kuwaelimisha
wananchi, wajue kuwa nchi imefikishwa pabaya sana na CCM. Vijana
wajipange wapambane kupiga kura na kulinda kura nchi nzima hadi CCM
iondoke. Vijana wasishauriwe eti wakapambane na bunduki za CCM na kwamba
liwalo na liwe! Pasiwe na liwalo kwenye maisha ya vijana wetu.
WIKI tatu zilizopita nilifika Nanyumbu kufanya mkutano wa hadhara,
polisi waliuzuia kupitia zuio la waziri wa mambo ya ndani na jeshi la
polisi makao makuu kuwa mikutano ya vyama isifanywe mkoa wa Mtwara
isipokuwa na wabunge na madiwani tu.
Kufika Nanyumbu nikakuta vijana
wapatao 1000 wakanipokea, wao na kina mama wakasema mkutano lazima
ufanyike. Polisi nao walikuwa ‘Standby’ na mabomu yao na bunduki zao na
vitambaa vyekundu na kabla ya hapo walishatangaza kwa vipaza sauti kuwa
nisifanye mkutano.
Pamoja na presha kubwa ya umma uliokusanyika
MJINI na ile presha ya viongozi wangu wa wilaya kuwa nisipolazimisha
kufanya mkutano ATI tutaua chama Nanyumbu niliweka msimamo. Ukweli ni
mchungu, sikuwa hata na mshauri, ilinipasa kutangaza kuwa hakuna
mkutano. Niliwakumbusha wananchi kuwa pale hapatakuwa na mkutano bali
mapambano ya polisi na wananchi.
Nilipowauliza wangapi wako tayari
kwa mapambano wote wakanyoosha mikono hadi watoto, tena wakiwa na hasira
KUU. Niliwaeleza kuwa nilikuja kwa ajili ya mkutano tu na siyo
mapambano.
Nikawataka watawanyike kimyakimya kurudi majumbani.
Nilizomewa sana lakini nilikubali gharama hizo, sikuwa tayari kuacha
vilema na majeruhi na hata maiti za watu “just because” ntalaumiwa na
viongozi na wananchi na wanachama. Nilitambua kuwa mara kadhaa nimewahi
kuhutubia mahali pale na nikajua kuwa nitakuwa na fursa nyingine siku za
usoni. Hasira zote zilikuwa juu yangu...kelele za msaliti nikapigiwa,
nikakubali. Kazi ya kiongozi ni kuongoza na si kufuata.
Nakubaliana na Maggid Mjengwa, kuwa viongozi wa vyama vyote tujipange.
CCM haitaondolewa madarakani kwa mapambano ya vijana wetu na polisi na
mabomu na risasi. Tuwaandae vijana nchi nzima, tuwaandae bodaboda na
wamachinga wasimamie mabadiliko makubwa ya elimu ya fikra na demokrasia
pana. Tuwaeleze vijana ukweli, kwamba nchi imeharibiwa sana, kwamba
tunahitaji CCM iondoke ili kiingie chama imara, kipewe muda wa kutosha
wa kusimamia mabadiliko na kupanua wigo wa ajira n.k.
Kamwe
wanasiasa tusizunguke nchi kuwadanganya vijana ATI wakituchagua tu, wote
watakuwa na ajira. Tusiwadanganye wamachinga ATI wakituchagua tu
tutawapa mikopo ya mamilioni, tusiwadanganye vijana ATI watuchague ili
keshoye tuwajengee majumba ya biashara. Tuwaeleze vijana ukweli,
tuwaeleze kuwa tukishaiondoa CCM tutaweka msingi mkubwa wa kuibadili
nchi na kwamba mabadiliko yatakuja hatua kwa hatua yakiwa na tija.
Tuwajulishe kuwa tunahitaji muda. Nchi iliyoharibiwa kwa miaka hamsini
hatutaijenga kwa siku 3 au mwaka mmoja, inahitaji muda uliopimwa na
ukapimika na lazima tuwaandae vijana wafahamu jambo hilo, wasije kudhani
kuwa patakuwa na “miracles”!.
Tusiwadanganye ATI tuna uwezo wa
kubadili nchi KUFUMBA na KUFUMBUA. Tukishashindwa kutekeleza, lazima
APPROACH yetu itakuwa ni kuwafanyisha vurugu, ili waone kuwa tunawatetea
na kwamba VURUGU HIZO ndiyo zitaleta SULUHU ya matatizo yao. Hakuna
mahali ambapo vurugu zimewahi kuwa suluhu ya matatizo ya wananchi.
Kuibadili nchi iliyoharibiwa na CCM kwa nusu karne inahitaji utulivu
mkubwa na kuwaelimisha sana vijana, vinginevyo ni kweli tutaanza
kuchimbiana makaburi.
Julius Mtatiro,
+255717536759, +255787536759,
juliusmtatiro@yahoo.com.
This post was written by: Author Name
Your description comes here!
Get Free Email Updates to your Inbox!
Filed Under:
Siasa
on Wednesday, May 22, 2013
Post a Comment