Mkurugenzi wa Oganaizesheni na mafunzo wa Chadema, Benson Kigaila
(Kushoto) akizungumza kuhusu chama hicho kugomea kungamano la Amani,
lililoandaliwa na kijtuo cha demokrasia Tanzania (TCD) Mwingine ni
mratibu wa kanda ya Ziwa Mashariki Renatus Nzemo.Picha na Michael
Matemange
Dar es Salaam. Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), jana
kilitangaza kwamba hakitashiriki kongamano la amani linalotarajiwa
kufanyika kwa siku mbili kuanzia leo baada ya kuitishwa na Kituo cha
Demokrasia Tanzania (TCD) jijini Dar es Salaam.
Kongamano hilo linatarajiwa kujadili na
kutafakari amani ya taifa, lakini chama hicho kimesema hakitahudhuria
kwa sababu kongamano lina mkono wa Serikali.
Mkurugenzi wa Oganaizesheni na Mafunzo wa Chadema,
Benson Kigaila, alisema amani haijadiliwi kwenye kufanya makongamano ya
hotelini bali mazingira ya amani yanawekwa na Serikali kwa kutenda
haki.
Akifafanua jana, Kigaila alisema Chadema inaamini
kwamba Serikali ni mfadhili wa kongamano hilo na kwamba haitashiriki
kwa kuwa amani haijadiliwi bali inatengenezwa na kuwapo kwa mazingira ya
haki na usawa.
‘’Chadema haitashiriki mkutano huo kwa kuwa
aliyepanga, aliyefadhili na aliyeitisha mkutano huo kwa mgongo wa TCD,
ni Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, ambaye ndani ya nafasi yake, haonekani
kuwa na dhamira ya dhati ya kuwapo amani katika taifa letu,’’
alisisitiza.
Pia alisema Chadema haitashiriki katika mkutano
huo akisema Serikali ya CCM, imejaa unafiki kwa kuhubiri amani mchana,
wakati usiku inachochea uhasama wa kidini, kisiasa na inawagawa
Watanzania kwa misingi ya imani za kidini na vyama.
Mwenyekiti wa TCD, James Mbatia alipoulizwa juu
ya madai ya Chadema kwa njia ya simu jana jioni alisikitishwa na madai
hayo akisema kongamano hilo limeitishwa kutekeleza uamuzi wa kikao cha
vyama vya upinzani kilichofanyika Februari 9, mjini Dodoma baada ya
kufukuzwa ndani ya Bunge, John Mnyika ambaye ni Mbunge wa Ubungo
kupitia Chadema.Alisema gharama za kongamano hilo hazizidi Sh100 milioni
na kwamba fedha hizo zinatoka kwa wafadhili wa TCD na Serikali
imechangia kidogo.Mbatia alisisitiza kwamba wakiwa Dodoma kipindi hicho
walikubaliana kuitisha makongamano ya aina hiyo yakiwashirikisha wadau
mbalimbali kwa awamu tofauti na kwamba kwa sasa vimealikwa vyama vyenye
wabunge bungeni na Chama cha UPDP ambacho kitawakilisha vyama ambavyo
havina wabunge. ‘’Sasa ni mwanzo, makongamano mengine yataitishwa
yakiwashirikisha wadau mbalimbali,’’ alisema.
Alisema Waziri Mkuu Pinda hahusiki kwenye
kongamano hilo, bali Serikali itawakilishwa na wawakilishi 20 wakiwamo
wa kutoka Zanzibar. Mbatia ambaye ni Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi
aliwashangaa Chadema kwa kugeuka ghafla akisema hata ratiba walishiriki.
CHANZO:MWANANCHI
CHANZO:MWANANCHI

Post a Comment