Featured

    Featured Posts

    Social Icons

Loading...

CHADEMA WANYESHEWA MABOMU YA MACHOZI


Askari wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) wakiwatawanya kwa mabomu ya kutoa machozi wafuasi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) waliokuwa wakiandamana kuelekea ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza jana.
...........
Jiji la Mwanza jana lilirindima mabomu ya kutoa machozi kwa takribani saa mbili wakati polisi wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) walipokuwa wakiwatawanya wafuasi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) waliokuwa wakiandamana kuelekea ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza.

Hatua ya wafuasi wa Chadema kuandamana kuelekea ofisini kwa Mkuu wa Mkoa, Evarist Ndikilo, ilitokana na kiongozi huyo kushindwa kutokea katika uwanja wa Furahisha kwa ajili ya kupokea maandamano hayo kama ilivyotarajiwa.

Maandamano hayo ambayo yalipangwa na wafuasi wa Chadema kwa kushirikiana na wabunge wa Ilemela, Highness Kiwia na Nyamagana, Hezekiel Wenje yalikuwa na lengo la kumshinikiza mkuu huyo wa mkoa kutoa tamko au kuwakabidhi barua wanayodai aliandikiwa na Waziri Mkuu akielekeza kurejeshwa madarakani madiwani watatu wa chama hicho, waliotimuliwa na Meya wa Manispaa ya Ilemela kinyume cha utaratibu.

Madiwani hao ni Marietha Chenyenge wa Kata ya Ilemela, Abubakar Kapera wa Kata ya Nyamanoro na Dani Kahungu wa Kata ya Kirumba, ambao walitimuliwa na Meya Henry Matata, ambaye hata hivyo, Chadema hawamtambui kama Meya halali kwa kile wanachodai alichaguliwa kinyume cha taratibu.

Ingawa maandamano hayo yalikuwa yameruhusiwa na kupewa ulinzi, lakini polisi walilazimika kuwatawanya wafuasi wa Chadema kwa kufyatua mabomu ya machozi baada ya wafuasi hao kwenda kinyume cha maelekezo waliyokuwa wamepewa.

Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi Mkoani Mwanza Ernest Mangu, maandamano hayo yaliyoanza majira ya saa 4:30 asubuhi yalipangwa kuanzia Buzuruga hadi katika uwanja wa Furahisha.

Hata hivyo, baada ya kufika katika uwanja huo wafuasi wa Chadema hawakumkuta mkuu wa mkoa ambaye waliatarajia ayapokee na kuwapa majibu ya madai yao.

Baada ya kutomkuta mkuu wa mkoa wafuasi hao waliwataka wabunge wao (Kiwia na Wenje), kwenda ofisini kwa mkuu wa mkoa na wawaletee majibu ya kuridhisha.

Mbunge Kiwia ndiye aliyelazimika kwenda kwa mkuu wa mkoa huku Wenje akibaki uwanjani hapo kuwatuliza wafuasi wao wasilete matata.

Hata hivyo, wafuasi hao walionekana kukosa uvumilivu ndipo ilipowadia majira ya saa 7:45 waliamua kuandamana kuekelea ofisini kwa mkuu wa mkoa kufuata majibu wao wenyewe na ndipo walipokutana na mkono wa chuma mara tu walipofika katika maeneo ya Nela kwenye barabara ya Makongoro.

Kabla ya kuanza maandamano hayo kuekelea kwa mkuu wa mkoa huku wakiwa na mabango yenye ujumbe kama vile “Meya wa mahakama tuachie jiji letu’, ‘Hatumtaki Matata siyo Meya halali’ wafuasi hao hawakusita kuonyesha hasira zao na kumweleza Mbunge Wenje aliyebaki kuwatuliza kuwa wanampa dakika 10 majibu yawe yamekuja la sivyo wataandamana kuelekea kwa mkuu wa mkoa.

Wenje aliwatuliza wafuasia hao kwa kuwaeleza kuwa hataki damu imwagike mahala pale na hivyo wawe watulivu kwa kusubiri majibu kutoka kwa Mbunge wa Ilemela.

Ili kutaka kuwaridhisha zaidi, Wenje alilazimika kumpigia simu Mbunge Kiwia na kuweka simu kwenye kipaza sauti ili wafuasi hao waweze kusikia kama tayari amefika kwa mkuu wa mkoa na amesema nini.

Baada ya kuchoshwa kusubiri ndipo wafuasia hao walipoanza kuandamana tena kutoka uwanja wa Furahisha kuelekea kwa mkuu wa mkoa na kuwafanya polisi waliokuwapo katika maeneo mbalimbali kurusha mabomu ya machozi ili kuwatawanya.

Hali hiyo ilisababisha kufungwa kwa barabara kwa takribani saa mbili na kusababisha kukosekana kwa huduma ya usafiri huku baadhi ya wanafunzi katika Shule ya Msingi ya Makongoro wakidaiwa kuzimia kutokana na milio ya mabomu.

Akizungumza hali hiyo, Mkuu wa Mkoa Ndikilo alisema suala la Meya wa Manispaa ya Ilemela lipo mahakamani na kwamba serikali inaheshimu uhuru wa mahakama na wala siyo suala la mkuu wa mkoa wala maandamano.

“Huenda viongozi wa Chadema hawakuwaelewesha vizuri wafuasi wao kuhusu jambo hili kwa sababu suala la meya siyo la mkuu wa mkoa ni la Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela na lipo mahakamani,” alisema.

Kuhusu suala la madiwani watatu waliotimuliwa na Matata, alisema Chadema walikata rufaa kwa Waziri Mkuu na siyo kwake kwani yeye alipewa nakala tu ya barua hivyo anayetakiwa kuwapa majibu ni Waziri Mkuu.

“Sina uwezo wa kuwarudisha madiwani waliofukuzwa kwani hawakukata rufaa kwangu,” alisema.

Aidha, aliporejea uwanjani hapo, Kiwia aliitaka serikali kutopuuza madai ya wananchi hao.
 
Awali Mbunge wa Nyamagana, Wenje alisema wameandamana kutafuta haki na sababu ya maandamano hayo yalijulikana, lakini kwa hofu mkuu wa mkoa ameshindwa kutokea kuwapa wananchi majibu wanayostahili.

Kamanda Mangu alisema maandamano hayo yaliruhusiwa kutoka Buzuruga hadi Furahisha na baada ya pale ujumbe wa viongozi ulielekea kwa mkuu wa mkoa.

Alisema baadhi ya wafuasi wa Chadema walikosa uvumilivu na kuanzisha maandamano mengine kwenda kwa mkuu wa mkoa hali ambayo iliwalazimu kutumia mabomu ya machozi kuwatawanya na kwamba hakuna aliyejeruhiwa.
CHANZO: NIPASHE
author

This post was written by: Author Name

Your description comes here!

Get Free Email Updates to your Inbox!
Chediel . Powered by Blogger.
© Copyright Rundugai Blog
Back To Top