Kiongozi wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu
Tanzania Sheikh Ponda Issa Ponda akiwa amelazwa kwenye chumba maalumu
katika taasisi ya mifupa Muhimbili (MOI), muda mfupi baada ya kufikishwa
hospitalini hapojana. Picha na Venance Nestory
Sheikh Ponda alisafirishwa usiku wa manane kutoka Morogoro baada ya juzi
kupigwa na kitu kinachodaiwa kuwa ni mtutu wa bomu saa 12:25 jioni
alipokuwa akisindikizwa na wafuasi wake kwenda katika Msikiti wa Mungu
Mmoja Dini Moja mara baada ya kumaliza kutoa mhadhara katika kongamano
mjini hapo.
Hata hivyo, Mwenyekiti wa Kongamano hilo, Sheikh Idd Mussa Msema, alidai kuwa Sheikh Ponda alipigwa risasi tatu begani.
Taarifa kutoka ndani ya familia ya Ponda zilisema kwamba baada ya kupata
taarifa za kupigwa risasi, baadhi ya masheikh walifunga safari kwenda
Morogoro na kumrejesha Dar es Salaam usiku huohuo. Kabla ya kurudishwa
Dar es Salaam, imeelezwa kuwa Sheikh Ponda alipelekwa katika Zahanati ya
Islamic Foundation.
Mmoja wa wanafamilia alidokeza kwamba Sheikh Ponda alifichwa na alikuwa
chini ya ulinzi mkali wa wafuasi wake na hakuna aliyeruhusiwa
kumsogelea.
Muhimbili
Hata hivyo, habari zilizopatikana baadaye jana zilisema kuwa alifikishwa
Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kwa ajili ya kupatiwa matibabu.
Sheikh Ponda alifikishwa Muhimbili jana saa 7:18 mchana na alipelekwa
kwenye chumba cha wagonjwa wa dharura na baadaye alitolewa na kupelekwa
kwenye chumba cha x-ray kwa ajili ya vipimo. Baadaye alipelekwa chumba
cha upasuaji.
Eneo kubwa la hospitali hiyo lilikuwa na idadi kubwa ya askari na mmoja
wa askari waliokuwa doria hospitalini hapo alisema walitawanywa kwenye
hospitali mbalimbali za Dar es Salaam baada ya kupata taarifa kuwa
angeletwa kwa matibabu.
“Nakuambia tuko hapa tangu saa kumi na moja asubuhi, tumetawanywa
hospitali mbalimbali baada ya kupata taarifa kuwa analetwa Dar. Bahati
nzuri kaletwa hapa Muhimbili... tunasubiri apate matibabu na tutamtia
mbaroni,” alisema askari huyo.
Taarifa ya poli
Msemaji wa Polisi, Advera Senso alisema jana katika taarifa yake kuwa
Sheikh Ponda yuko Hospitali ya Muhimbili akitibiwa baada ya kupata
majeraha yaliyotokana na purukushani na polisi wakati wafuasi wake
walipokuwa wanataka kumtorosha.
“Kutokana na tukio hilo, timu inayoshirikisha wajumbe kutoka Jukwaa la
Haki Jinai likiongozwa na Kamishna wa Polisi Isaya Mungulu imeanza
uchunguzi wa tukio hilo na Polisi inawataka wananchi kuwa watulivu
wakati wanashughulikia suala hilo kisheria.”
Polisi Morogoro wapigwa chenga
Wakati akiwa Muhimbili, Polisi mkoani Morogoro, lilisema bado linamtafuta Sheikh Ponda.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Faustine Shilogile alisema jana kuwa
kwa taarifa zilizopo, bado Sheikh Ponda amefichwa mkoani Morogoro na
kwamba anaendelea kutafutwa.
“Tamko la Serikali mpaka sasa hatujathibitisha kwamba Sheikh Ponda
amejeruhiwa na risasi na tunamtaka mtu yeyote awe yeye au ndugu yake aje
kuthibitisha kwamba amepigwa risasi,” alisema.
Alikanusha madai kwamba jeshi hilo limehusika kumpiga risasi akisema
hakuna ushahidi kwa kuwa hajaonekana ili kuonyesha kuwa amepata majeraha
sehemu yoyote ya mwili wake.
“Siku zote risasi haifichiki, kama amepigwa angejitokeza ili kupewa kibali cha matibabu,” alisema Shilogile.
Alisema polisi inawashikilia watu wawili na inawatafuta viongozi watano
wa Umoja wa Waadhiri wa Kiislamu Mkoa wa Morogoro walioandaa kongamano
hilo.
Kamanda Shilogile alisema waandaaji wa kongamano hilo walipewa kibali na
polisi kufanya kongamano kwa masharti ya kutokutoa matamshi ya
uchochezi ikiwa ni pamoja na Sheikh Ponda kutokuhudhuria.
Alisema hata hivyo, katika kongamano hilo lililofanyika eneo la Kiwanja
cha Ndege kulikuwapo na wageni zaidi ya watano waliohutubia. Kamanda
Shilogile alisema ilipofika saa 12.50 jioni ndipo Sheikh Ponda alipofika
na baadaye kupewa dakika tano kuzungumza na alieleza kuwa yeye si
mzungumzaji kwa siku hiyo na badala yake angezungumza leo katika Viwanja
vya Msikiti wa Jabal Hirra.
Alisema baada ya hapo mkutano ulifungwa na wafuasi wake wakaanza
kusukuma gari alilokuwa amepanda katika Barabara ya Tumbaku karibu na
Kituo cha Mafuta cha El Saedy. Alisema kuwa, polisi walimfuata kutaka
kumtia mbaroni lakini wafuasi wake walianza kurusha mawe na ndipo askari
hao walipofyatua juu risasi tatu za baridi ili kuwatawanya.
Hata hivyo, alisema polisi walizidiwa nguvu na wafuasi hao ambao
walifanikiwa kumtorosha Sheikh huyo kwa pikipiki.Alisema kuwa baadaye
zilizagaa taarifa kuwa amepigwa risasi ya begani na kupelekwa Hospitali
ya Mkoa kisha kutoroshwa kusikojulikana.
Wavamia hospitali
Katika hatua nyingine, watu wanaosadikiwa ni wafuasi wa Sheikh Ponda
wamevamia Hospitali ya Mkoa wa Morogoro na kufanya uharibifu kwa kuvunja
vioo katika wodi namba sita ya watoto wakishinikiza kuonyeshwa Sheikh
huyo alipo.
Baadhi ya wagonjwa waliolazwa na watoto wao katika wodi hiyo, Kibua
Michael na Cecilia Clemence kwa nyakati tofauti walisema kwamba wafuasi
hao walikusanyana nje ya hospitali hiyo na kurusha mawe na kusababisha
taharuki kwa baadhi ya wagonjwa.
Sheikh Kundecha atoa sharti
Taasisi na Jumuiya za Kiislamu Tanzania, imeitaka Serikali kuunda tume
huru ya uchunguzi wa tukio la kujeruhiwa kwa Sheikh Ponda na majibu yake
ndiyo yatakayoamua uhusiano baina ya Waislamu nchini na Serikali
iliyopo madarakani.
Akitoa tamko la Jumuiya hiyo katika Msikiti wa Mtambani, Kinondoni, Dar
es Salaam jana, Amiri wa Jumuiya hiyo, Sheikh Yusufu Mussa Kundecha
alisema pamoja na mambo mengine, pia wanataka kuona askari polisi
aliyemdhuru Sheikh Ponda anachukuliwa hatua za kisheria.
Alisema kitendo alichofanyiwa Sheikh Ponda ni mtiririko wa vitendo vya
uonevu na unyanyasaji na aliishangaa Serikali kumtafuta Sheikh huyo
kupitia vyombo vya habari wakati inafahamu hatua za kuchukua pale
wanapokuwa wanamtafuta mtu.
Alisema hata yeye wakati anatafutwa na polisi alipelekewa barua
akitakiwa kuripoti kituoni lakini si kupitia vyombo vya habari na
kitendo hicho kinaonyesha wazi kuwa Serikali imeshindwa kuwahakikishia
raia usalama wao.
“Mbaya zaidi, wao ambao wanataka watu wasichukue sheria mkononi ndiyo
hao wa kwanza kufanya hivyo jambo ambalo sidhani kama litatufikisha
pazuri,” alisema Kundecha.
Aliitaka Serikali kufuata sheria na kufuata taratibu husika katika
kushughulikia masuala yanayowahusu makundi mbalimbali katika jamii
badala ya inavyofanya sasa akisema hiyo inachangia chuki kati ya
Waislamu na Serikali.
Profesa Lipumba atoa tam
Mwenyekiti wa (Cuf), Profesa Ibrahim Lipumba amemtaka Rais Jakaya
Kikwete kuingilia kati suala la kupigwa risasi kwa Sheikh Ponda ili nchi
isije kuingia kwenye machafuko yenye mrengo wa kidini.
Profesa Lipumba aliwaambia waandishi wa habari jana ofisini kwake Dar es
Salaam kuwa chama hicho kinalaani vikali tukio hilo na kutaka polisi
kuwakamata waliompiga risasi.
“Nimetoka kumjulia hali muda mfupi uliopita, nimemkuta akiwa katika hali
mbaya japo anaweza kuzungumza na kutambua watu wanaokwenda kumwona...
kwa kweli tukio la kupigwa risasi kwa Sheikh Ponda linaweza kusababisha
nchi kuingia kwenye machafuko ya kidini kama hatua za haraka
hazitachukuliwa.
“Tukio la Sheikh Ponda kupigwa risasi tena na watu wanaodhaniwa kuwa ni polisi, limeleta sura mbaya kwa taifa,” alisema Lipumba.
Rufaa ya wafuasi wake leo
Wakati hayo yakitokea, rufaa ya wafuasi 52 wa Sheikh Ponda waliohukumiwa
kifungo cha mwaka mmoja jela inatarajiwa kusikilizwa leo katika
Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam.
Wafuasi hao walihukumiwa kifungo hicho, Machi 21, mwaka huu na Mahakama
ya Hakimu Mkazi Kisutu baada ya kutiwa hatiani kwa makosa matatu kati ya
manne yaliyokuwa yakiwakabili.
Walikuwa wakikabiliwa na mashtaka ya kula njama, kutenda makosa, kukaidi
amri ya polisi kabla na baada ya kufanya maandamano yaliyozuiwa na
polisi, kufanya mikusanyiko haramu na kusababisha uvunjifu wa amani na
uchochezi.
Hata hivyo, kupitia kwa Wakili wao, Mohamed Tibanyendera walikata rufaa wakipinga hukumu na adhabu waliyopewa.
Rufaa hiyo itasikilizwa leo na Jaji Salvatory Bongole.
Kwa mujibu wa hati ya rufani waliyoiwasilisha mahakamani hapo, wafuasi
hao, pamoja na mambo mengine, wanadai kuwa hakimu alikosea kisheria
katika kuchambua ushahidi wa pande zote uliowasilishwa mahakamani.
Pia wanadai kuwa katika hukumu hiyo, hakimu alijikanganya kwa kumwachia
huru mmoja wa washtakiwa na kuwatia hatiani washtakiwa wengine.
Watu hao walikamatwa na Polisi Machi 15, mwaka huu, wakiandamana kwenda
Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), kwa lengo la kumshinikiza kumpa
dhamana Sheikh Ponda na mshtakiwa mwenzake Mukadam Swalehe na Machi 18,
mwaka huu walipandishwa kizimbani na kusomewa mashtaka.
Imeandikwa na Lilian Lucas (Morogoro), James Magai, Bakari Kiango, Aziza Masoud, Aidan Mhando na Joseph Zablon (Dar).
Chanzo - Gazeti la Mwananchi