Dar es Salaam. Kamati ya Bunge ya Huduma za Jamii, imevikataa viwango
vipya vya alama za ufaulu kwa elimu ya sekondari vilivyotarajiwa kuanza
kutumika mwaka huu na kutaka utaratibu na alama zilizotumika mwaka jana,
zitumike kupanga matokeo ya Mtihani wa Taifa wa Kidato cha Nne wa mwaka
huu.
Serikali ilitangaza utaratibu mpya wa alama za Mitihani ya Kidato cha
Nne na Sita kwa kufuta Daraja la Sifuri na kuleta Daraja la Tano.
Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Stephen Ngonyani alisema jana kuwa
kamati hiyo ilichukua uamuzi huo kwa kuwa pamoja na udhaifu ulio kwenye
alama hizo, kamati yao haikuhusishwa katika mchakato wa kuandaa alama
hizo.
“Mwenyekiti wangu (Margaret Sitta) alisema kile hakiwezekani, kuna
viwango ambavyo wameleta havipo kwenye nchi nyingine duniani,
tumewaambia wakavifanyie kazi walete tena,” alisema mbunge huyo wa
Korogwe Vijijini, ambaye ni maarufu zaidi kwa jina la Profesa Maji
Marefu.
Ngonyani alisema waliagiza watendaji wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya
Ufundi kuhakikisha wanaishirikisha kamati yao kwani imejaa walimu
wanaoweza kushauri vizuri.
“Hatutaki watuletee mambo ambayo yamewashinda baada ya kuyapeleka kwa wananchi,” alisema Ngonyani.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Sifuni
Mchome akitangaza uamuzi huo mapema mwezi huu, alisema uamuzi wa
kubadilisha mfumo huo umechukuliwa kutokana na changamoto zilizojitokeza
mwaka 2012.
Alama zilizokuwa zikitumiwa awali na Baraza la Mitihani la Taifa
(Necta), katika kupanga matokeo hayo, kwa Kidato cha Nne ni A=80-100,
B=65-79, C=50-64, D=35-49, F 0-34 kwa upande wa Kidato cha Sita,
A=80-100, B=75-79, C=65-74, D=55-64, E=45-54, S=40-44 na F= 0-39.
Alama mpya zilizotangazwa ni A=75-100, B+=60-74, B=50-59, C=40-49,
D=30-39, E=20-29 na F=0-19. Alama hizo ni kwa kidato cha nne na sita.
Kwa utaratibu huo, A ilitafsiriwa kuwa ni ufaulu uliojipambanua, B+ ni
ufaulu bora sana, B ufaulu mzuri sana, C ufaulu mzuri, D ufaulu hafifu, E
ufaulu hafifu sana na F ufaulu usioridhisha.
Katika utaratibu huo, mtihani wa mwisho ulitarajiwa kuwa na alama 60 na
alama 40 zitokane na alama za Maendeleo ya Mwanafunzi Shuleni
(Continuous Assessment-CA).
Mwaka jana baada ya Serikali kufuta matokeo ya mtihani wa Kidato cha
Nne, Necta ilitumia CA ya 30 huku mtihani wa mwisho ukiwa na alama 70.
Wadau wa elimu na wabunge walipinga vikali utaratibu mpya wa alama za
mitihani hali iliyofanya Spika wa Bunge, Anne Makinda kuamuru wizara
husika kupeleka bungeni taarifa yenye maelezo juu ya uamuzi huo.
Kabla ya Serikali kutoa kauli yake, watendaji na viongozi wa Wizara ya
Elimu walikutana na Kamati ya Bunge ya Huduma za Jamii Mjini Dodoma
mwezi huu ambapo wajumbe wa kamati hiyo walikataa viwango hivyo vipya na
kuitaka wizara kuendelea kuvifanyia kazi viwango hivyo kwa
kuishirikisha Bodi ya Necta.
Mjumbe mmoja aliyekuwa ndani ya kikao hicho alisema hoja kuu
zilizosababisha kukataliwa kwa alama hizo ni ile iliyosemwa kuwa ni
kushusha sana viwango vya ufaulu, pia kutaka shughuli hiyo ifanywe kwa
kushirikisha Bodi ya Necta ambayo kisheria ndiyo yenye jukumu la kutunga
sera za mitihani.
“Tulichosema ni kuwa viwango vya ufaulu pamoja na utaratibu uliotumika
mwaka jana, viendelee kutumika kwa mitihani ya kidato cha nne
inayoendelea kwa sababu viwango vipya vimekosa uhalisia,” alisema mmoja
wa wajumbe wa kamati hiyo.
Wajumbe hao walisema haiwezekani ufaulu wa A ukaanzia 75 wakati hakuna
nchi duniani yenye A ya namna hiyo, pia haiwezekani 20 ikahesabika pia
kama ufaulu.
“Pia ukiangalia, Kifungu cha Nne cha Sura ya 10 ya Sheria ya Necta
kinasema kuwa taasisi hiyo ndiyo yenye jukumu la kutengeneza sera ya
mitihani,” alisema mjumbe huyo.
Hata hivyo, Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Philipo Mulugo
alisema bungeni kuwa daraja sifuri litaendelea kuwapo lakini
hakuzungumzia chochote kuhusu alama ambazo kamati ilishauri wizara hiyo
izifanyie kazi.
Mulugo ambaye ndiye aliyehudhuria kikao hicho hakupatikana jana
kuzungumzia suala hilo. Hata alipopigiwa simu yake ya mkononi, iliita
bila kupokewa.
Ofisa Habari wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Ntambi Bunyanzu
alisema kwamba hana taarifa za maagizo hayo ya kamati hiyo.
Ufaulu wa chini
Kwa mujibu wa kitabu kinachoonyesha viwango vya ufaulu duniani kila
mwaka cha International Qualification, baada ya Tanzania kutangaza alama
hizo mpya, sasa inaongoza duniani kwa kuwa na alama za chini za ufaulu.
Nchi zinazofuatia kwa viwango vya chini baada ya Tanzania ni Kenya,
Rwanda, Uganda, Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo (DRC) ambazo
hata hivyo, viwango vyake vipo juu kwa kiwango kikubwa vikilinganishwa
na vile vya Tanzania.
Chanzo: mwananchi.co.tz