Featured

    Featured Posts

    Social Icons

Loading...

JAMAL MALINZI:NITAFUFUA MPIRA WA MIGUU TANZANIA

Mahojiano iliongozwa na Deodatus Balile, Dar es Salaam

Katika kinyang'anyiro kikali, Jamal Malinzi, mhandisi na shabiki mwaminifu wa mpira wa miguu, mwenye umri wa miaka 53, alichaguliwa kuwa rais mpya wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) tarehe 27 Oktoba.

Jamal Malinzi alichaguliwa kuwa rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu tarehe 27 Oktoba, 2013. [Na Deodatus Balile/Sabahi]

Alimshinda Makamu wa Rais wa TFF Athuman Nyamlan kwa kura 21, na kuchukua nafasi ya Rais wa TFF anayemaliza muda wake Leodeger Chilla Tenga, ambaye anastaafu baada ya kuwa katika nafasi hiyo kwa miaka minane.

Malinzi alishinda uchaguzi huo baada ya kutoa hotuba iliyosisimua, ambapo aliainisha kile kinachoitwa "ndoto zinazotimizika" za kuubadilisha mpira wa miguu wa Tanzania kwa kipindi cha miaka minne hadi minane ijayo.

Sabahi ilimhoji Malinzi kujua nini alichopanga kwa shirikisho la mpira wa miguu kwa nchi.

Sabahi: Nini kimekufanya ugombee urais wa TFF?

Jamal Malinzi: Ni uchungu. Licha ya uchungu niliamua kutoa huduma yangu kwa nchi hii.

Kwa miaka minane iliyopita, serikali imekuwa ikitoa msaada kwa sekta ya michezo katika nchi hii, hususan mpira wa miguu ambapo wafadhili wamekuwa wakifurika, lakini kwa bahati mbaya tumekuwa tukishuka kila wakati katika viwango vya FIFA. Kwa sasa tuko nafasi ya 129 [kati ya 207], wakati tulikuwa nafasi ya 65 mwaka1990 pasipo vifaa au ufadhili.


Kwa miaka minane iliyopita, TFF imekuwa ikipokea misaada na bonasi kutoka FIFA yenye thamani ya shilingi milioni 3 (dola milioni 1.85) lakini huwezi kufuatilia mahali fedha zote hizi zilipokwenda. Benki ya National Microfinance, makampuni ya simu kama vile Airtel, Vodacom na [makampuni] ya vinywaji baridi ikiwa ni pamoja na Coca Cola, Kampuni za bia za Tanzania na Serengeti, yote haya yamekuwa yakitoa fedha ambazo hazionekani.

Nimechoka kwa moyo wangu kuumia. Hii ndiyo sababu niliamua kuchukua hatua. TFF iliundwa kisheria na kupewa mamlaka ya kujiendeleza, kustawi na kusimamia mpira kikamilifu katika nchi hii.

Sabahi: Unafikiri ni wapi Tanzania ilifanya kosa?

Malinzi: Katika kipindi cha mwishoni mwa miaka ya 1990 kuelekea miaka ya 2000 serikali ilibadilisha sera ambapo michezo ilifutwa shuleni. Sera mpya imetupeleka mahali tulipo sasa. Kwa sasa inabidi tuwe wabunifu, kujumuisha na kutengeneza pale tulipofanya makosa.

Sabahi: Utafanyaje hilo?

Malinzi: Nitashirikisha wadau kwa kuzungumza nao kwa kina kuhusu mwisho wetu. Ninapenda kuishirikisha serikali pamoja na kuishawishi kuelewa kwamba mpira wa miguu sio tu kwa ajili ya kuyaunganisha mataifa, kuhamasisha afya au kuwaburudisha Watanzania, lakini pia mpira wa miguu ni biashara kubwa duniani.

Ninataka serikali kuanzisha michezo shuleni na kuanzisha mashindano baina ya shule kuanzia shule ya msingi hadi ngazi ya chuo kikuu. Kupitia mashindano haya tutakuwa tukibaini wachezaji wa mpira wa miguu wenye vipaji na kuvikuza, lakini kwa siku zijazo tutaunda timu za vijana kupitia akademia za michezo.

Tunahitaji kushiriki katika kila mashindano ya mpira wa miguu katika ngazi ya kanda, barani Afrika, na dunia kwa wanaume na wanawake. Nitaunda bodi ya makocha wenye uzoefu wa mpira wa miguu kuanzia Jumamosi hii [tarehe 2 Novemba] kubungua bongo nini cha kufanya kwa haraka.

Sabahi: Je, ni nini mpango wako wa muda mrefu?

Malinzi: Tutaweka kituo cha michezo chenye uwezo wa hali ya juu, ambacho kitakuwa kikitoa mafunzo, kukuza vipaji na kuitunza timu ya taifa wakati wa mafunzo. Kituo kitapunguza gharama za hoteli na kuhakikisha huduma yenye ubora kwa ajili ya timu yetu ya taifa wakati wa kambi ya mafunzo.

Pili, ninalenga kuanzisha mashindano kadhaa ya taifa kwa wachezaji vijana [wa umri wa kati ya miaka 12 na 20] ambapo, hatua kwa hatua, tutakuwa tukiwaandaa wachezaji venye kiwango.

Ninapanga Tanzania kuandaa na kushiriki katika mashindano ya [ubingwa] Vijana wa Afrika mwaka 2019. Tutaitumia CAF [Shirikisho la Mpira wa Miguu la Afrika] barua pepe baada ya mkutano [tarehe 2 Novemba], na kisha kutafuta ridhaa ya serikali kuandaa mashindano ya Vijana wa Afrika ya mwaka 2019 kama mahitaji ya msingi ya CAF na FIFA.

Mara maombi yetu yatakapokubalika, ninajua itaweka msukumo kwetu kujiandaa vizuri katika miaka mitano ijayo. Ifikapo mwaka 2019, tutakuwa na timu bora ya vijana. Timu hiyo itatuongoza katika [Kombe la Mataifa ya Afrika] la mwaka 2021, Olimpiki ya mwaka 2022 na Kombe la Dunia la mwaka 2026.

Sabahi: Umelalamika kuhusu makocha wasiokuwa na viwango. Una mpango wowote kwa ajili ya uboreshaji?

Malinzi: Ni kweli kiwango chetu kiko chini sana. Uingereza ina makocha wa daraja la A lililoidhinishwa 1,100, Ujerumani ina makocha 5,500 na Hispania 12,000 [makocha] wa kiwango hiki. Tanzania ina kocha mmoja tu mwenye daraja lililoidhinishwa kwa jina la Sunday Kayuni.

Tunapaswa kuwa na mtaala wa mpira wa miguu unaofundishwa nchi nzima. Nitawapeleka makocha Hispania, ambao watafundishwa kuwa wakufunzi watakaporejea nyumbani.

Aidha, hatuna refa yeyote wa Kitanzania ambaye anaongoza mechi za FIFA tangia mwaka 1998. Ninapaswa kulimaliza hili kwa kuwapa mafunzo marefa wetu kufikia viwango vya FIFA.

Sabahi: Je, una ujumbe maalumu kwa Watanzania mashabiki wa mpira wa miguu?

Malinzi: Ninawashukuru Watanzania kwa uaminifu walionionyesha na ninapenda kuwaeleza kwamba uvumilivu unatakiwa ili kupata matokeo mazuri.

Tunahitaji msaada wao ili TFF iweze kukamilisha hili.

author

This post was written by: Author Name

Your description comes here!

Get Free Email Updates to your Inbox!
Chediel . Powered by Blogger.
© Copyright Rundugai Blog
Back To Top