Na Fidelis Butahe na Musa Juma, Mwananchi
Dar na Arusha. Utata mkubwa umeibuka kuhusu waraka halisi wa ‘Mkakati wa
Mabadiliko 2013’ uliosababisha Zitto Kabwe kuvuliwa wadhifa wake wa
Naibu Katibu Mkuu wa Chadema na kikao cha Kamati Kuu ya chama hicho
kilichofanyika Novemba 20 - 22, mwaka huu.
Mkurugenzi wa Habari na Uenezi wa Chadema,
John Mnyika ambaye amedai, “Waraka utakaotumika katika mashtaka yao
siyo huo. Sisi tutautumia ule ambao uliwasilishwa katika Kamati Kuu
ambao una mambo makubwa na mengi zaidi kuliko huo unaochapishwa sehemu
mbalimbali, ikibidi tutautoa huo waraka halisi,” alisema. Picha na
Maktaba
Baada ya juzi, Mkurugenzi wa Habari na Uenezi wa Chadema, John Mnyika
kuwaeleza wanahabari kuwa waraka uliochapishwa katika magazeti na
mitandao ya kijamii, siyo halisi, aliyekuwa Mwenyekiti wa chama hicho
Mkoa wa Arusha, Samson Mwigamba amejitokeza na kuutetea huku akidai
kwamba huo unaodaiwa na uongozi kuwa ndiyo halisi umeghushiwa.
Zitto ambaye pia ni Mbunge wa Kigoma Kaskazini (Chadema), alivuliwa
uongozi pamoja na aliyekuwa Mjumbe wa Kamati Kuu, Dk Kitila Mkumbo na
Mwigamba kutokana na madai ya kuandaa waraka huo ambao Chadema kimesema
ulikuwa unaeleza mbinu za uasi za viongozi hao ambazo zingetumika wakati
wa uchaguzi mkuu wa ndani wa chama hicho jambo ambalo ni kinyume na
katiba, sheria na itifaki zake.
Katika tamko alilotoa jana, Mwigamba alidai kwamba
kuna njama zinazofanywa na baadhi ya viongozi wa Chadema ili kuubadili
waraka halisi wa ‘Mkakati wa Mabadiliko 2013’ kwa lengo la kupoteza
maana yake, huku akisisitiza kuwa waraka halisi hauna tatizo lolote.
Katika madai yake, Mnyika alisema waraka huo unaosambazwa na
kuchapishwa, si ule uliowasilishwa na kujadiliwa katika kikao cha Kamati
Kuu na kuahidi kuutoa waraka halisi ambao una mambo makubwa na mengi
zaidi.
“Waraka utakaotumika katika mashtaka yao siyo huo. Sisi tutautumia ule
ambao uliwasilishwa katika Kamati Kuu ambao una mambo makubwa na mengi
zaidi kuliko huo unaochapishwa sehemu mbalimbali, ikibidi tutautoa huo
waraka halisi,” alisema.
Hata hivyo, jana Mwigamba alisema waraka halisi ni ule ambao upo katika
kompyuta mpakato (Laptop) aliyonyang’anywa na wanachama wa Chadema,
Oktoba 25, mwaka huu, katika mkutano mjini Arusha.
“Waraka uliosambazwa kwenye vyombo mbalimbali vya habari na mitandao ya
kijamii ni sahihi neno kwa neno kama nilivyousoma katika magazeti ya
jana (juzi), pamoja na nakala iliyopo katika mtandao wa kijamii wa Jamii
Forums.”
Aliongeza: “Ili kuthibitisha kwamba waraka ule ndiyo wenyewe,
nawatumieni ‘soft copy’ kutoka kwenye kompyuta yangu kwani waraka huo
uliibwa kutoka katika kompyuta hiyo ambayo nilirudishiwa baada ya wao
kuikagua na kukuta waraka huo halisi.”
Mwigamba alisema waraka wake unatofautiana kwa kiasi kikubwa na ule
ambao Chadema kinasema kuwa ndiyo halisi: “Lissu na wenzake wana mpango
wa kuuchakachua waraka huu, lakini wamekwama.”
Alisema kuandaa waraka huo siyo uhaini kama ambavyo imekuwa ikielezwa na
viongozi wa Chadema na kusisitiza kuwa ni waraka wa kusaka ushindi
katika uchaguzi halali ndani ya chama hicho uliopangwa kufanyika Desemba
mwaka huu na baadaye kusogezwa hadi Juni mwakani.
“Wakati wa uchaguzi si ajabu kuwepo kwa wanachama wanaounga mkono
wagombea tofauti. Nimekuwa karibu na Mwenyekiti wa Chadema, Freeman
Mbowe kwa miaka mingi, najua hata yeye ana mikakati na wanaoshiriki
mkakati wake ni Lissu na Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema,”
alisema.
Alisema anashangazwa kwa kitendo cha Chadema kuusambaza waraka huo,
wakati ulikuwa ni mpango wa siri kati yake, Dk Kitila pamoja na mtu
mwingine anayetajwa kwa jina la M2.
“Baada ya kugundua madhara ya kusambaza ovyo waraka huo, sasa wameamua
kuukana, waraka wangu ni sahihi na unaeleza ukweli. Binafsi nimefanya
kazi ofisi ya makao makuu ya chama kama Mhasibu Mkuu ningeweza kuanika
mengi lakini sijafanya hivyo kwa masilahi ya chama,” alisema na
kuongeza:
“Tunatambua kwamba viongozi wetu wanamchukia Zitto na tangu siku nyingi
walipanga kumfukuza. Nawashauri watafute sababu nzuri za kumfukuza
uongozi na hata uanachama. Zitto hahusiki na mkakati huu pamoja na
kwamba alikuwa ndiye mhusika mkuu, alikuwa hajui lolote.”
Jumamosi iliyopita, mama yake mzazi Zitto, Shida Salum ambaye ni Mjumbe
wa Kamati Kuu ya Chadema alisema waraka huo ulikuwa umeongezwa maneno.
“Hata ule waraka uliongezwa maneno baada ya baadhi ya wanachama kumpora
Mwigamba `laptop’ yake alipokuwa mkoani Arusha katika kikao cha
Chadema,” alisema bila kutaka kufafanua ulibadilishwa vipi, licha ya
kuwataja kwa majina waliohusika kuubadili wakiwamo wabunge wawili wa
chama hicho na viongozi wa ngazi za juu.
Sitoki Chadema
Kuhusu hatima yake ndani ya Chadema, Mwigamba alisema hana mpango wa
kuondoka hata baada ya kuvuliwa uongozi, huku akisisitiza kuwa hakusudii
kuomba radhi kutokana na kuandaa waraka huo.
Alisema hakusudii kuhama kwa kuwa ana historia ndefu na Chadema na anaamini kuwa ndicho mkombozi wa Watanzania.
“Nimekuwa kiongozi wa kata, wilaya, mkoa hadi taifa. Nimetumia muda
wangu mwingi na hata kuhatarisha maisha yangu kwa ajili ya chama hiki,
siwezi kuondoka kutokana na tofauti za kimitazamo na viongozi wangu,”
alisema.
Mwigamba, ambaye alikuwa mfanyakazi katika Mahakama ya Kimataifa
inayosikiliza Kesi za Mauaji ya Halaiki ya Rwanda (ICTR) na baadaye
kujiondoa ili ajikite kwenye siasa, alisema ana imani yanayotokea sasa
katika chama hicho yatapita salama.
Chanzo: mwananchi.co.tz
Chanzo: mwananchi.co.tz