Mhe.
Bernard K. Membe (Mb), Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa
Kimataifa akielezea kuhusu hisia za kutengwa kwa Tanzania katika Jumuiya
ya Afrika Mashariki (EAC). Waziri Membe alikuwa katika mahojiano
maalum na Mwandishi Fredy Mwanjala wa Kituo cha Televisheni cha Channel Ten ofisini kwake jana, jijini Dar es Salaam.
Waziri Membe akiendelea na mahojiano hayo, wakati Bi. Fauzia Yusuph wa Channel Ten akirekodi tukio hilo. Picha na Tagir Daisy Mwakawago-Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa
---
Na TAGIE DAISY MWAKAWAGO
Waziri
wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mhe. Bernard K. Membe (Mb)
ameelezea hisia za sintofahamu kuhusu kutengwa kwa Tanzania katika
Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), na kuhoji kuwa iwaje nchi yetu
itengwe na nini maana ya Jumuiya hiyo?
Aliyasema hayo katika mahojiano maalum na Mwandishi Fredy Mwanjala wa Kituo cha Televisheni cha Channel Ten, yaliyofanyika ofisini kwake Jana , jijini Dar es Salaam. Mazungumzo
hayo yalijikita zaidi katika kujua msimamo wa Tanzania kidiplomasia
wakati huu wa sintofahamu ya Jumuiya hiyo inayoendelea, hususan Tanzania
ikionekana kutengwa na nchi za Uganda, Rwanda na Kenya.
“Huu
ni muungano wa watu wenye woga,” alisema Waziri Membe na kuongeza kuwa
Jumuiya hiyo ilishawahi kuvunjika mnamo mwaka 1977.
“Jumuiya
hiyo ilishawahi kuvunjika na kuungwa tena, na Tanzania hatukuathirika.
Tuko tayari kupewa au kutoa talaka, na ikiwezekana labda kutakuwa na
talaka rejea,” alisema Waziri Membe. Jumuiya hiyo ya EAC inazijumuisha
nchi za Uganda, Kenya, Rwanda, Burundi na Tanzania.
“Sisi ndio ‘center of gravity’
na ndio soko kubwa la bidhaa katika ukanda wa Afrika Mashariki - tuna
rasilimali zaidi ya majirani zetu, tuna utajiri wa ardhi na bandari nne
ambazo ni ufunguo wa kutumia bahari kubwa na kufikia nchi nyingine
duniani,” alifafanua Waziri Membe. Bandari hizo ni za Mtwara, Tanga,
Dar es Salaam na bandari ya Bagamoyo ambayo ipo katika ujenzi wa
kuifanya iwe bandari kubwa ya kimataifa barani Afrika.
Waziri
Membe alisema cha kushangaza ni kwamba majirani zetu wanatakiwa
kutambua kuwa Tanzania ni nchi ambayo ni mfano pekee wa kuigwa kwa
uzoefu wa muungano. “Sisi ni taifa na sio muungano wa makabila matatu
au manne,” alisema Waziri huyo.
“Hauwezi
leo ukaitaifisha ardhi ya nchi nyingine na kuviacha vizazi vijavyo bila
mali,” alisema Waziri Membe na kuongeza kuwa “kwa vyovyote vile,
jumuiya hii ya Afrika Mashariki lazima iende kwa taratibu.”
Aidha,
Waziri Membe alienda mbali zaidi na kusema kuwa huenda chokochoko ya
kutengwa kwetu inatokana na wivu au gere kwa Tanzania kupeleka majeshi
yake huko Mashariki ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, jambo alilosema
huenda halijawafurahisha baadhi ya watu katika Jumuiya hiyo.
Vilevile
alisema kuwa kitendo cha Tanzania kukataa ardhi kuwa sehemu ya mali ya
Afrika Mashariki huenda pia imepelekea mchango mkubwa kwenye choko choko
hizo.
Waziri Membe amewaambia Watanzania kuwa “wakae wakijua kwamba akufuzae hakwambii toka, utaona tuu mambo yanabadilika.”
Mwisho.