Waziri Mkuu Mstaafu, Edward Lwoasa
.....
Katika taarifa yao waliyoitoa kupitia Idara ya Habari Maelezo jana jijini Dar es Salaam, wenyeviti hao, walisema kuwa hawakuwahi kukaa kikao chochote kwa lengo la kukubaliana kutoa tamko hilo na hivyo kukosa uhalali wa kumpa mwenyekiti wao mamlaka ya kutoa tamko hilo alilolitoa Januari Mosi mwaka huu.
Msindai alitoa kauli hiyo katika hafla iliyoandaliwa na Lowassa kwa ajili ya kuukaribisha Mwaka Mpya wa 2014 wilayani Monduli, mkoa wa Arusha.
Hata hivyo, taarifa hiyo ilitolewa bila kuwa na saini wala jina la mmoja wa wenyeviti hao.
NIPASHE lilipowasiliana na mmoja wa maofisa wa Maelezo kuhusu mwenyekiti aliyewasilisha taarifa hiyo, alisema vyombo vya habari vinaweza kumnukuu Mwenyekiti wa CCM wa Mkoa wa Iringa, Jesca Msambatavangu.
Kwa mujibu wa Msambatavangu, wao ni viongozi na wajumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa (Nec), hivyo hawatarajii kukiuka katiba, sheria, kanuni na taratibu zozote ikiwamo za uchaguzi kwa kuwa wanatambua kuwa kumuunga mkono mgombea mtarajiwa siyo sahihi hasa katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.
Alisema wenyeviti hao hawatarajii kuwa chanzo cha kumharibia mgombea yeyote kwa kumsababishia kukosa sifa za kugombea, pia hawatarajiwi kusigina demokrasia ndani ya chama kwa kumbeba mgombea mmoja.
“Tunafahamu kuwa kumbeba mgombea mmoja au muonyesha nia ni kuwanyima wagombea au waonyesha nia wengine fursa za kupimwa, kutetewa, na kuruhusu demokrasia ichukue mkondo sahihi na kumteua mgombea kwa mujibu wa sifa zake. Tunazijua sheria na tunaziheshimu taratibu na miongozo ya chama iliyoko kwenye katiba na kanuni zake, hivyo hatuko tayari kupuuza dhamana tuliyopewa na wanachama wenzetu kwa maslahi binafsi,” alisema Msambatavangu.
Aidha, wenyeviti hao kupitia taarifa hiyo walikiomba radhi cha hicho, uongozi wa ngazi zote na wanachama wake wote na wenye nia ya kuingia katika chama hicho pamoja na wagombea wote kwa usumbufu uliotokea kutokana na taarifa hiyo.
Januari Mosi mwaka huu, Msindai ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Singida, alikaririwa na vyombo vya habari akisema kuwa wenyeviti wote wako tayari kumuunga mkono Lowasa katika safari yake aliyotangaza kuianza ya kutimiza ndoto zake.
Lowassa ambaye pia ni Mbunge wa Monduli, mkoani Arusha alikaririwa na vyombo vya habari akisema:
“Safari hii tumeianza yenye matumaini, yenye ndoto za Mtanzania kuwa na elimu bora na bure, ndoto ya Mtanzania kuwa na elimu makini, ndoto ya Mtanzania yenye kuwa na maji safi, ndoto ya Mtanzania ya kuwa na matumaini ya maisha.”
Hata hivyo, Lowassa hakueleza ni safari gani, lakini wachambuzi wameitafsiri kuwa ni mbio zake za kuusaka urais wa mwaka 2015.
Kauli hiyo iliungwa mkono na Msindai wakati wa ibada ya kuukaribisha Mwaka Mpya kwenye Kanisa la Kiinjili na Kilutheri Tanzania (KKKT) wilayani Monduli na baade kwenye tafrija iliyofanyika nyumbani kwake mkoani humo ambayo pia ili hudhuriwa ni baadhi ya viongozi wengi wa ngazi zote wa CCM.
Aidha, mapema wiki hii, baadhi ya vyombo vya habari vilimkariri Msindai akidai kuwa kauli aliyoitoa katika tafrija hiyo ilikuwa ni yake binafsi na haiwahusishi wenyeviti wenzake.
Baada ya kauli ya Msindai, Makamu mwenyekiti wa CCM Bara, Philip Mangula na Katibu wa Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye, walitoa kauli za kuwatishia walioanza kujinadi kabla ya wakati wake huku Nape akisema makada hao wameshakosa sifa.
CHANZO:
NIPASHE