Dar es Salaam. Sakata la uhamisho wa mshambuliaji Emmanuel Okwi limeanza kuwatafuna vigogo wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) wakidai kushughulikia suala hilo kiushabiki badala ya kufuata taratibu.
Taarifa ya Ofisa habari wa TFF, Bonifance Wambura
jana ilisema kuwa kiongozi wa idara ya Takwimu, Sabri Mtulla
analalamikiwa na shirikisho hilo kwa madai ya kuidanganya Kamati ya
Sheria na Hadhi za Wachezaji kuwa hakukuwa na pingamizi dhidi ya
usajili wa Okwi huku akijua wazi kuwa jambo hilo si kweli.
“Kamati ilikutana mara ya kwanza, ikahoji kama
kuna pingamizi lolote dhidi ya Okwi, lakini Mtulla alidanganya kuwa
hakuna, kamati ilivyokutana kwa mara ya pili ikabaini pingamizi
lilikuwepo, ila kiongozi huyo alificha wakati alijua wazi kuwa Simba
walikuwa wameweka pingamizi wakipinga Okwi kusajiliwa na Yanga kwa
mkataba wa miaka miwili na nusu.
“Kwa mujibu wa kanuni, malalamiko hayo
yamefikishwa kwenye Kamati ya Maadili ambayo itachunguza ili
kujiridhisha kama yana msingi au la. Ikibaini kuwa kuna kesi ndipo
walalamikiwa watafika mbele ya kamati hiyo kujibu mashtaka yao.”
Hata hivyo, gazeti hili ilipomtafuta Mtulla
kuhusiana na suala hilo alisema kwa kifupi: “Ofisi ndiyo inayonituhumu
nimefanya udanganyifu, mimi nasubiri niitwe nitoe utetezi wangu, ili
suala nalijua undani wake kuanzia mwanzo hadi lilipofika sasa, nitaweka
wazi kila kitu, kwa kifupi wamelikoroga sasa wanatafuta pa kuangushia
jumba bovu.”
Sinema ya usajili wa mshambuliaji huyo raia wa
Uganda ilianza Mei 19, 2013 wakati Shirikisho la Soka nchini Uganda
(Fufa) kupitia mtendaji wao mkuu, Edgar Watson lilipotuma barua kwa
Shirikisho la soka la Tunisia likimwombea kibali Okwi kujiunga na
kambi ya timu ya taifa (Uganda Cranes) iliyokuwa inajiandaa na michezo
miwili dhidi ya Angola na Liberia kufuzu kushiriki Kombe la Dunia
mwaka huu nchini Brazil.
Michezo hiyo ilikuwa ichezwe Juni 8 na 15 jijini
Kampala na baada ya michezo hiyo Okwi hakurejea klabuni kwake, Etoile
du Sahel.
Simba SC iliyomuuza kwa Etoile ilitaka kumrejesha
kundini mwaka jana, lakini aliikwepa na kwenda SC Villa ya Uganda ili
apate nafasi ya kucheza fainali za wachezaji wa ligi za ndani (Chan).
Okwi aliuzwa na Simba kwa Etoile kwa ada ya Dola
300,000 lakini Watunisia hao walishindwa kuwalipa Simba fedha za
usajili huo kwa wakati, pia Okwi aligoma kuwachezea Waarabu hao kwa
madai ya kushindwa kuheshimu makubaliano ya kimkataba.
Baada ya mgomo uliochukua miezi kadhaa SC Villa
ambayo ndiyo iliyomkuza Okwi kabla ya kumuuza Simba, iliomba Shirikisho
la Soka la Kimataifa (Fifa), kumruhusu arudi Uganda ili asipoteze
kiwango chake na Fifa ilimruhusu kwa kumpa kibali cha miezi sita wakati
suala lake likitatuliwa.
CHANZO:Mwananchi
CHANZO:Mwananchi

Post a Comment