Dar es Salaam. Kung’olewa kwa aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar, Othman Masoud Othman katika nafasi hiyo ni kama kumewasha moto visiwani humo huku mwenyewe akisema: ‘Ipo siku ukweli utadhihirika.’
Othman licha ya kutafutwa kutwa nzima ya jana,
hakuwa tayari kuzungumzia kufukuzwa kwake kazi na badala yake alituma
ujumbe mfupi kupitia simu yake ya kiganjani akisema: “Si wakati wake
kulizungumza.”
Alipoulizwa kwamba pengine anaweza kuwa tayari
lini kuzungumzia suala hilo, Mwanasheria huyo aliyepinga baadhi ya Ibara
za Katiba zinazopendekezwa kwa kuzipigia kura za hapana, alijibu pia
kwa kifupi: “I have no idea when (sifahamu ni lini), time will tell (ipo
siku ukweli utadhihiri)”.
Kwa upande mwingine, watu wa kada mbalimbali
nchini wameelezea uamuzi wa Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein
kumtimua kazi kuwa ni uonevu kwa kuwa alitumia haki yake ya kikatiba.
Mwalimu wa Idara ya Lugha za Kigeni na Isimu wa
Chuo Kikuu Dar es Salaam (UDSM), Faraja Christoms alisema, “Sidhani kama
ni matumizi mazuri ya madaraka. Othman katika maelezo yake alitamka
wazi kuwa maoni yake si msimamo wa Serikali ya Zanzibar.
Alichokizungumza ndiyo msimamo wake binafsi na jinsi anavyoona inafaa.”
Alisema Mwanasheria huyo katika maoni yake
alieleza wazi jinsi Katiba ya Zanzibar inavyokinzana na Katiba ya
Jamhuri ya Muungano... “Kilichomtokea ni tatizo la kutokuwapo kwa
maridhiano tangu ulipoanza mchakato wa kuandika Katiba Mpya.”
Mkurugenzi Mtendaji wa shirika lisilokuwa la
kiserikali linalojihusisha na masuala ya kijamii (Fordia), Buberwa Kaiza
alisema wajumbe wa Bunge la Katiba walipiga kura kwa utashi wao na si
ushawishi kutoka katika makundi wanayotoka.
“Alichokizungumza Othman si maoni ya Serikali za
Zanzibar. Alipokuwa bungeni alikuwa sawa na wajumbe wengine na si
mwakilishi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar. Hii ni ishara mbaya kwa
watendaji wa Serikali. Maana yake ni kwamba watendaji wa chini
wakifichua uovu unaofanywa na walio juu yao wanaweza kufukuzwa kazi.”
Mtaalamu wa Lugha ya Kiswahili, Dk Aldin Mutembei
alisema: “Sasa watu wameanza kuzuiwa kuamua mambo yao wao wenyewe.
Othman alipiga kura kama yeye binafsi na si Serikali ya Zanzibar tena
akiwa na mawazo huru kabisa. Kumfukuza kazi ni kutomtendea haki.”
Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alisema:
“Ubatili siku zote huzaa ubatili. Nchi yetu sijui inakwenda wapi, maana
watu wanazuiwa kufanya mambo yao ambayo yapo kikatiba. Maandamano
hakuna, ukisema ukweli unafukuzwa kazi?
“Watanzania wataendelea kudai Katiba yenye maoni
yao. Hii ni ishara ya kutaka kuwafumba midomo wengine wanaopenda kueleza
ukweli.
Mhadhiri wa UDSM, Dk Benson Bana alikuwa tofauti
na wenzake, akisema kilichomkuta mwanasheria huyo alikitarajia kwa
sababu kitendo chake cha kupiga kura ya hapana kilimaanisha kuwa
amekwenda tofauti na msimamo wa Serikali ya Zanzibar.
Habari zaidi Endelea Hapa>>>>
Habari zaidi Endelea Hapa>>>>
Post a Comment