Mdogo Wangu Sitti; U-Miss Bangulile Usikufanye Uabike!
Na. M. M. Mwanakijiji
Sitti mdogo wangu umeishi Marekani kwa muda mrefu; unajua mambo ya
kuwajibika yanavyofanya kazi hasa pale ambapo mtu anajikuta amebanwa na
ukweli. Madai ya kwamba kuna mahali umeongopea ili upate unachotaka ni
madai mazito na hamna namna ya kukwepa kuwajibika kwake. Ukweli kwa
asili yake unaweza kupuuzwa kwa muda au hata kukataliwa lakini hauwezi
kugeuzwa uongo halafu ukakubaliwa. Ukweli unasimama wenyewe kama shahidi
wake mwenyewe; mtu yeyote mwenye kuutafuta na akaupata anapaswa kuutii
na wakati mwingine kuutii hadi mwisho.
Madai dhidi yako kimsingi kabisa ni madogo – kwa maana ya uzito wake –
ila ni muhimu sana kwa sababu yanahusu taasisi ambayo mabinti na wazazi
kadha wa kadha Tanzania wamekuwa wakiuangalia. Haya Mashindano ya
Ulimbwende au “Umiss Bangulile” kama Sheikh wangu Kipozeo amewahi
kuyaita ni mashindano siyo tu ya uzuri na maumbo (beauty and figure); ni
mashindano juu ya mtu; tabia (character) na mitazamo. Yule anayevishwa
taji la Umiss Bangulile (Miss Tanzania) anatakiwa kuwa ni mdada mwenye
kuwakilisha mabinti wa rika yake na kuwa mfano kwa wale wa chini ya umri
huo kwa mitazamo, tabia n.k Siyo mashindano ya sura tu au maumbo!
Lini umewaliza; siyo swali gumu hivyo. Wewe mwenyewe unaweza kuwa huna
uhakika kwani kila mmoja anajua siku yake ya kuzaliw kwa kuambiwa;
hakuna anayejua amezaliwa lini. Tunaambiwa na wazazi wetu au walezi wetu
na wakati mwingine kuambiwa huku kuna kuja na ushahidi wa vyeti vya
kuzaliwa. Kinachonisikitisha kwa kweli kwenye sakata lako ni jinsi gani
Wazazi wako wamekuacha mpweke ujibu swali ambalo huna uwezo wa kulijibu.
Baba na Mama yako wanapaswa kuwa watu wa kwanza na pekee ambao wana
uwezo wa kutuambia kuwa umezaliwa lini. Tatizo ni ukimya wao na hilo
wengine linatusumbua sana.
Kwamba umezaliwa mwaka 1989 au 1991 siyo hoja sana; tatizo ni kuwa
lazima iwe ni kweli ili kuonesha kuwa unastahili kushiriki na kushinda
mashindano haya ya Ulimbwende a.k.a UMiss Bangulile. Vielelezo
mbalimbali vya huku kwa Mjomba Obama vinaonesha ulizaliwa mwaka 1989
wakati kielelezo kimoja cha hati ya kuzaliwa ambayo ni nakala (siyo
halisi) inaonesha umezaliwa 1991. Wewe mwenyewe umesema umezaliwa 1991.
Sasa, kuna mahali hukusema kweli. Ama uliwadanganya kina Uncle hapa
Marekani au uliwadaganya huko nyumbani. Taarifa zote mbili haziwezi kuwa
kweli kwa wakati mmoja hasa kwa vile zinapingana. Ni kwa sababu hiyo
naamini milango yako yote ya kutokea imefungwa isipokuwa mmoja.
Kurudisha taji la Umiss Bangulile na kuomba radhi mashabiki na wapenzi
wako na wale wote ambao wamekwazika.
Hautakuwa wa kwanza kati ya ma Miss duniani kurudisha taji la Umiss.
Wengi tunakumbuka yaliyomkuta Vanessa Williams Mmarekani Mweusi wa
kwanza kushinda taji la Miss America baada ya picha za utupu alizopiga
miaka michache nyuma kuibuliwa. Alijiuzulu na kuvuliwa taji japo
alifanikiwa baadaye kujijenga katika fani ya uigizaji. Kashfa siyo
mwisho wa maisha. Na wapo wengine ambao nao wamewahi kuachilia mataji
yao kwa sababu ya kashfa mbalimbali na hivyo isikuwie vigumu kuliachilia
taji hilo kwani madhara yameshafanyika. Siamini kama utaweza kusimama
kuwakilisha Tanzania katika mashindano mengine bila ya maswali haya haya
kuibuliwa na labda yakaibuliwa mazito zaidi.
Naamini hata hivyo hupaswi kujiuzulu peke yako; naamini naye Mkurugenzi
wa Mashindano hayo Hashim Lundenga ambaye amesababisha ama kwa uzembe,
kushiriki au kwa tamaa nyingine tu kufanya suala hili liibuliwe anapaswa
kujiuzulu. Tayari kumeshawahi kuwa na kashfa nyingine zilizomezwa chini
kwa chini lakini hii inapaswa kuondoka nay eye ili hatimaye mashindano
hayo yapate mtu anayepeswa kuyasimamia kwa uhakika na kwa weledi usio
mfano.
Rudisha taji lao jijengee heshima yako tena. Usije ukajikuta katika kuutetea uongo unapoteza na utu wako.
MMM
This post was written by: Author Name
Your description comes here!
Get Free Email Updates to your Inbox!
Filed Under:
Michezo
on Monday, October 27, 2014
Post a Comment