CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Mkoa wa Konondoni,
kimempitisha Diwani mteule wa Ubungo, Boniface Jacob (Chadema), kuwa
mgombea umeya wa Manispaa ya Kinondoni, huku akiwakilisha mwamvuli wa
vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).
Mgombea huyo alikuwa akiwania nafasi hiyo huku akipambana na diwani
mwenzake mteule wa Kata ya Mbweni, Abdunel Elibariki (Chadema) ambaye
alishindwa kutamba.
Akitangaza matokeo ya uchaguzi huo jana jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti
wa uchaguzi huo Venus Kimei , alisema Jacob alishinda kwa kura 20 kati
ya kura 28 zilizopigwa.
“Wagombea walikuwa wanne lakini watatu ndio ambao walikidhi
vigezo, hata hivyo waliopigiwa kura ni wawili kutokana na mgombea mmoja
Ndeshukurwa Tungaraza ambaye ni Diwani mteule wa Kata ya Makongo kujitoa
katika hatua za mwisho,” alisema.
Akizungumza baada ya kutangazwa kushinda kinyang’anyiro hicho, Jacob
alisema ana imani atashinda katika uchaguzi utakaowajumuisha wagombea wa
vyama vingine kikiwamo Chama Cha Mapinduzi (CCM).
“Nitasimamia kwa vitendo sera ya elimu ambayo chama chetu
iliisimamia katika kampeni na jambo zuri ni kwamba hata Rais Dk. John
Magufuli amesisitiza kwamba watoto wasome bure kuanzia msingi hadi
sekondari.
“Hivyo ninaamini hilo linawezekana endapo tutasimamia mapato ya
ndani kwa umakini nataka Manispaa Kinondoni iwe mfano katika hili ambayo
tutahakikisha tunaboresha maslahi ya walimu na kuondoa kabisa michango
ya aina zote,” alisema.
Alisema atasimamia kwa kuzingatia sera ya utatu akijumuisha wananchi,
wanasiasa na wataalam bila kuwabagua kwani kwa pamoja watainua maendeleo
ya manispaa hiyo.
Kwa upande wa Chama cha Wananchi (CUF), ambacho ni mshirika wa Ukawa,
kinatarajia kumsimamishwa Diwani mteule wa Kata ya Tandale, Jumanne
Mbunju (CUF) ili awanie nafasi ya unaibu meya wa manispaa hiyo.
Katika Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni yenye majimbo manne, Chadema
imenyakua majimbo matatu ambayo ni Ubungo, Kawe na Kibamba, huku jimbo
moja la Kinondoni likienda CUF.
Kata zinazounda halmashauri hiyo ni 34 ambapo Chadema ilishinda kata 18
na kupata madiwani wa viti maalumu 7, CCM kata 11 na viti maalumu 4 na
CUF ikishinda kata 5 na viti maalumu 2.
Post a Comment