Featured

    Featured Posts

    Social Icons

Loading...

ILI KUUNDA CHAMA KIMOJA CHA UPINZANI CHENYE NGUVU, MBATIA ANENA HAYA…

mbatia
Mwenyekiti Mwenza wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), James Mbatia, amesema ili kuweza kuanzisha chama kimoja cha upinzani chenye nguvu, inahitajika viongozi wa upinzani kujenga msingi wa uaminifu miongoni mwao.

Pamoja na kwamba hakutaka kutamka wazi kuwa uaminifu huo kwa sasa haupo, Mwenyekiti huyo pia wa Chama cha NCCR-Mageuzi, amesisitiza kuwa bado lengo la kuanzisha chama hicho kimoja cha Ukawa lipo palepale na linaendelea kufanyiwa kazi.

Mbatia alikuwa akihojiwa katika kipindi kinachorushwa kila Jumapili na Televisheni ya Azam. Alisema katika kuanzisha chama hicho, suala la uaminifu miongoni mwa viongozi ni muhimu ili kufikia malengo halisi ya uanzishwaji wa chama hicho.

“Hata mwaka 1964 hayati Baba wa Taifa Julius Nyerere pamoja na Abeid Amaan Karume, waliaminiana kwanza na kwa kutumia utashi wao wakaunganisha nchi mbili za Tanganyika na Zanzibar na kuzaliwa Tanzania. Waliamiana,” alisisitiza.

Alipohojiwa kwamba, kwa sasa Ukawa hakuna uaminifu ndio maana bado uanzishwaji wa chama hicho unasuasua, mbunge huyo wa Vunjo, aligoma kueleza kwa uwazi zaidi kusisitiza kuwa uaminifu ni lazima katika suala nyeti kama hilo.

Alisema kwa sasa azma hiyo ya kuwa na chama kimoja imeanza kuonekana zaidi kwa vitendo kuliko maneno kwani kupitia umoja huo walisimamisha mgombea mmoja wa urais hali iliyowapatia mafanikio.
“Ni kweli kwenye umoja wetu kuna migongano ya hapa na pale lakini hiyo ni kawaida lazima tuwe na fikra tofauti, lakini tungefikiria kwenye chanya zaidi ila bado kuna haja ya kujengeana uaminifu kwanza,” alisema.
Aidha, alisema uanzishwaji wa Ukawa ni wazo la NCCR-Mageuzi kwa kuwa tangu chama hicho kilipoanzishwa mwaka 1991 kilikuwa na lengo la kuunganisha nguvu ya upinzani.
“Kwa maana hiyo Ukawa ni mtoto wa NCCR-Mageuzi ambayo ni mama wa upinzani. Kususia vikao vya Bunge Akizungumzia kitendo cha wabunge wa upinzani kuendelea kususia vikao vya Bunge pindi inapotokea kutoelewana ndani ya chombo hicho, Mbatia alisema hiyo ndio njia pekee ya kupatiwa haki wanayoidai badala ya kukaa kimya.”
Hata hivyo, alipobanwa na kuhojiwa kwa nini wasitumie fursa waliyonayo na kubaki ndani ya Bunge na kuwasilisha maoni yao, alisema hiyo ni njia mojawapo ya kuonesha hasira waliyonayo juu ya mfumo uliopo unaoliendesha bunge hilo.
“Hakuna mtu aliyesomea kuwa mbunge au Rais, mabunge yote yaliyopita yaliyoongozwa na Samuel Sitta na Anne Makinda, yote yalikuwa na malalamiko, lakini Bunge hili la 11 malalamiko yamezidi. Ndio maana na sisi tunaamua kutoka ikiwa ni njia ya kuonesha hasira hasa pale tusiposikilizwa,” alisema.
Kuhusu hoja kwamba kwa sasa tangu Serikali ya Awamu ya Tano iingie madarakani, Ukawa imeanza kudhoofu, Mbatia alikanusha hoja hiyo na kusisitiza kuwa kwa sasa umoja huo ndio umeonesha mshikamano hasa kutokana na matukio ya bungeni.

Ukawa na nguvu za Chadema Pamoja na hayo, Mbatia alisema kitendo cha Ukawa kuinufaisha zaidi Chadema kwa kuwapatia wabunge wengi ni jambo lililotegemewa kwani hata mwaka 1995 NCCRMageuzi nayo iliposimamisha mgombea urais aliyekuwa na nguvu kipindi hicho, ilijipatia umaarufu na mafanikio ya kisiasa.

Maridhiano bungeni Aidha, mbunge huyo alipongeza jitihada za Spika wa Bunge, Job Ndugai za kurejesha maridhiano yaliyovunjika katika mkutano uliopita baina ya wabunge wa upinzani na chama tawala na kusisitiza kuwa hatua za spika huyo ni jambo zuri la kuungwa mkono.

Alisema kinachotakiwa ndani ya chombo hicho ni kuhakikisha taratibu zilizowekwa zikiwemo kanuni za Bunge zinafuatwa huku akiendelea kumtupia lawama Naibu Spika, Dk Tulia Ackson kuwa ndiye tatizo la mvurugano ndani ya chombo hicho.
“Hata hivyo, Tanzania hii ni yetu sote, keshokutwa tunakutana na viongozi wa dini zote kuzungumza suala la amani ya nchi yetu. Naamini juhudi hizi zikiendelea tutafikia mahala pazuri,” alisema.

SASA NI CCM VS UKAWA

MAMBO yanazidi kwenda mrama kati ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), anaandika Dani Tibason.

Msimamo uliotolewa na Baraza la Vijana wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Bavicha) unaakisi mwanzo mpya wa msuguano wa kisiasa nchini.

Tayari Bavicha wametangaza msimamo wa kutoshirikiana na vijana wa CCM katika tukio la aina yoyote.

Mbali na kutangaza msimamo huo pia wametangaza kuzuia mikutano yote ambayo itaandaliwa na CCM kama inavyozuiwa ya Chadema.

Msimamo huo umetolewa leo na Julius Mwita, Katibu Mkuu wa Bavicha wakati akizungumza na waandishi wa habari Dodoma.

Mwita amesema, kutokana na kitendo cha Serikali ya CCM kushirikiana na Jeshi la Polisi kuzuia mikutano ya Chadema kinaonesha wazi kuwa, serikali ina mpango wa kuhakikisha inaua upinzani jambo ambalo haliwezi kukubalika.

Amesema, kutokana na hali hiyo kwa sasa Bavicha wametangaza kutoshirikiana na vijana wa CCM katika mazingira yoyote ikiwa ni pamoja na katika masomo, nyumba walizopanga, misiba na katika majamga mengine mbalimbali.

“Kutokana na kuwepo kwa vitendo vya kikatili vinavyofanywa na Serikali ya CCM vya kuzuia mikutano ya upinzani, sasa tunatangaza sisi vijana wa Bavicha hatutashirikiana na wanachama wa CCM kwa njia yoyote ya kijamii wala kimaendeleo.

“Natangaza kwa vijana wote wa Chadema hatutashiriki katika mazizi, hatutashiriki kusoma nao wale waliopo katika vyuo, hatutashiriki sherehe mbalimbali zinazowahusu wao wala hatutashiriki katika jambo lolote la kimaendeleo, na hii ni msimamo wetu.

“Pia tunawapongeza wabunge wetu kwa kususia shughuli zote za ambazo zinafanywa na CCM kwani kwa kufanya hivyo inaonesha kuwa sasa tumechoka na uongozi wa kiimla,” amesema Mwita.
Hata hivyo amedai, Rais John Magufuli ni muoga kuliko marais wote kwa kuwa ni rais ambaye hapendi kukosolewa na kuambiwa ukweli pale ambao amekuwa akikosea jambo ambalo anatakiwa kujitafakari na kujikosoa.

“Sasa vijana vijana tumejipanga kuhakikisha Jeshi la Polisi linazuia mikutano au mikusanyiko ambayo inafanywa na CCM na ikumbukwe kuwa, 23 Julai mwaka huu CCM watakuwa na vikao vya kumkabidhi rais Magufuli kuwa mwenyekiti wa CCM.

“Sasa tunataka Jeshi la Polisi kuzuia mkusanyiko huo na kama haitawezekana vijana wa Chadema na Ukawa watazui mikutano hiyo.

“Haiwezekani mikutano ya Chadema ikawa ndiyo inayozuiliwa wakati mikutano na mikusanyiko ya CCM inaendelea kufanyika, jambo hili kamwe haiwezi kukubalika na tunasema sasa imefika mwisho wa uvumilivu,” amesema Mwita.

Edward Simbeye, Katibu Mwenezi Bavicha amesema, yeye ndiye mratibu wa mahafali za wanafunzi wa Chadema vyuo vikuu (Chaso) nchini hivyo polisi walipaswa kumkamate yeye na si kuzuia mahafali hayo.

WABUNGE WA UKAWA WATOA MPYA BUNGENI

Wabunge wa Kambi ya Upinzani Bungeni leo wametumia mtindo mpya kueleza hisia zao baada ya kuamua kutoka kwenye ukumbi wa Bunge wakiwa wamejifunika midomo kwa karatasi.

Hii ni wiki ya pili mfululizo wabunge hao wamekuwa wakitoka bungeni baada ya kutangaza kutohudhuria kikao cha bunge kinachoongozwa na Naibu Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson.

Mbunge wa Vunjo (NCCR-Mageuzi), James Mbatia amesema wameamua kutumia mtindo huo mpya kwa sababu Bunge limekataa kuwasikiliza hoja zao.

BUNGENI LIVE:MBUNGE WA CCM ANUSURIKA KICHAPO KUTOKA WABUNGE WA UKAWA

Mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Jackline Msongozi juzi jioni alinusurika kipigo kutoka kwa wabunge wanawake wa UKAWA baada ya kuwaeleza kuwa upande huo una wabunge wawili tu wenye michango ya maana ambao ni Upendo Peneza (Viti Maalumu Chadema) na Magdalena Sakaya (Kaliua - CUF).

Akichangia mjadala wa bajeti kwa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Msongozi aliishambulia kambi ya upinzani akieleza kuwa kuna mlevi mmoja amechangia upande wa upinzani kuhusu uuzwaji wa nyumba za Serikali wakati waliohusika na uuzwaji huo wamehamia upinzani ambao ni Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye.

Msongozi alisema hakuna mke mwenza anayeweza kumsifia mwenzake, hivyo upinzani hauwezi kuisifia CCM kutokana na kazi wanayoifanya.

Baada ya kusema maneno hayo na wabunge wengine kuchangia, Bunge lilipoahirishwa wabunge wanawake wa upinzani wakiongozwa na Sabrina Sungura na Ester Matiko walimfuata Msongozi wakitaka kumshambulia, lakini aliondoka moja kwa moja pasipo kusimama popote.

Sungura alipoulizwa alisema kuwa mbunge huyo angesimama wangemshughulikia

SAKATA LA UDA:UKAWA Wawakaanga Ridhwan Kikwete na Mama Salma

HALMASHAURI ya Jiji la Dar es Salaam imewakaanga wanaotajwa kumiliki Shirika la Usafiri Dar es Salaam (UDA) bila kufuata utaratibu, anaandika Pendo Omary.

Hatua hiyo imekuja baada ya Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam inayoongozwa Ukawa kuzuia Sh. 5 bilioni, fedha mali ya Kampuni ya Simon Group Limited.

Mama Salma Kikwete, Mke wa Rais Mstaafu, Jakaya Kikwete na Ridhwan Kikwete, mtoto wa rais huyo na Prof. Juma Kapuya, aliyekuwa Mbunge wa Urambo Magharibi wanatajwa kuwa miongoni mwa wana hisa kwenye shirika hilo.

Simon Group Limited ililipa fedha hizo kwa halmashauri hiyo ikiwa ni sehemu ya malipo ya ununuzi wa hisa za UDA.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo, Saed Kubenea, Mbunge wa Jimbo la Ubungo amesema halmashauri haikuuza UDA licha ya Simon Group Limited kudai kununua.

Kwenye mkutano huo ambao pia uliohudhuriwa naIsaya Mwita Charles, Meya wa Jiji la Dar es Salaam Kubenea amesema, mkutano uliokabidha UDA kwa Simon Group uliitishwa bila baraka za wenye mali – Baraza la Madiwani la Jiji na Msajili wa Hazina na kwamba, ulihudhuriwa na watu wanne tu.

“Kwanza tunataka mtambue halmashauri haikuuza UDA kwa kuwa, Simon Group Limited wametumia hati ya UDA – mali ya wananchi kufanya biashara. Haturudishi fedha hizi mpaka tufanye hesabu, tujue kampuni hii imepata faida kiasi gani.

“Hata katika mradi wenyewe wa UDA-TR, kumesheheni utapeli. Unaoitwa mkutano mkuu maalum wa wana-hisa wa tarehe 10 Juni 2011, uliosimamiwa na Didas Masaburi, aliyekuwa Meya wa Jiji kuidhinisha pamoja na mengine, uuzaji wa hisa za UDA, haukuwa halali,” amesema Kubenea.

Kubenea amesema, mkutano uliokabidha UDA kwa Simon Group uliitishwa bila baraka za wenye mali – Baraza la Madiwani la Jiji na Msajili wa Hazina na kwamba, ulihudhuriwa na watu wanne tu

“Watu hawa ni Dk. Didas Masaburi mwenyewe ambaye alikuwa mwenyekiti; Mkurugenzi wa Simon Group, Robert Kisena ambaye alikuwa katibu; Mwanasheria wa jiji, Isaac Nassor Tasinga na Kaimu Mkurugenzi wa Jiji, Phillip Mwakyusa,” amesema Kubenea.

Amesema, kwenye mkutano huo Masaburi alitangaza Kampuni ya Simon kuwa ‘imetimiza masharti yote ya mkataba wa kupewa hisa, mali na uendeshaji wa UDA.’

Ameeleza kuwa, mwaka 1983, Msajili wa Hazina alitoa asilimia 51 ya hisa na kuipa Halmashauri ya Jiji huku Serikali Kuu ikibakiwa na asilimia 49 na kwamba, shirika hili liliwekwa katika orodha ya mashirika ya kurekebishwa na serikali mwaka 1997.

“Taarifa ya serikali ya tarehe 3 Agosti 2011 kwenda Kamati ya Bunge ya Miundombinu inaeleza mkutano huo ulikuwa batili kwa kuwa, ulikiuka Katiba ya UDA, kifungu namba 45 kutokana na kutotimia kwa akidi na kukosekana kwa msajili wa hazina,” amesema Kubenea.

Taarifa hiyo imeeleza, kikao hicho hakikuwa na mamlaka ya kufanya uamuzi, na kuwa maazimio yote yaliyofikiwa yalikuwa batili.

“Kwa taarifa hii pekee, serikali ilipaswa kuiondoa Simon Group kwenye uendeshaji wa UDA ikiwemo kukodishwa mali zake, hadi hapo uchunguzi wa suala hilo utakapokamilika. Haikufanya hivyo,” amesema Kubenea.

Kubenea amesema, kwa taarifa hiyo pekee ilitosha serikali kuchunguza na kuwachukulia hatua wote waliohusika, hasa kwa kuzingatia kuwa, kabla ya kikao hicho, tayari Masaburi alishapokea barua ya tarehe 28 Februari 2011 kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu iliyomuagiza kusitisha mara moja mchakato wa kuuza hisa za serikali ambazo hazijagawiwa.

Akinukuu barua kutoka kwa Waziri Mkuu yenye Kumbukumbo Na. 185/295/01/27, amesema Masaburi na wenzake waliendesha mkutano huo wakiwa na kabrasha la Katiba ya UDA ambayo vipengele vyake vilikuwa vinakataza walichokifanya.

“Kipengele cha 2.0 cha mkataba kinaeleza mauzo ya hisa 7,880,303 ambazo hazijagawanywa ambapo kwa majibu wa kipengele cha 2.2, mnunuzi alipaswa kulipa kwa awamu kiasi cha Sh. 1.1 bilioni,” amesema.

Aidha, anasema malipo ya kwanza ya Sh. 285. 6 milioni sawa na asilimia 25 ya malipo yalipaswa kufanywa katika kipindi cha siku zisizozidi 14 tangu mkataba kufungwa.

Lakini Simon Group haikulipa kiasi kamili kwa mujibu wa mkataba na hata kiasi ilichotoa ilikilipa nje ya siku zilizotajwa na mkataba.

Chanzo:Mwanahalisi

KAFULILA:BILA UPINZANI IMARA CCM ISINGEMPITISHA DK.MAGUFULI 2015


David Kafulila alipokuwa bungeni.
...........................
Tangu ulipoanzishwa mfumo wa vyama vingi hapa nchini mwaka 1992, kumekuwa na mambo mengi hususani katika siasa za Tanzania.
 
Miongoni mwa mambo hayo ni pamoja na vyama vya upinzani kuweka mbele mapambano dhidi ya ufisadi ndani ya serikali kuanzia awamu ya pili uongozi wa nchi chini ya Rais mstaafu Ali Hassan Mwinyi.
 
Katika kipindi hicho chote wapinzani waliendelea na mapambano hayo na kuyafanya ajenda ya kudumu kwa serikali ya awamu ya tatu ya Rais mstaafu Benjamin Mkapa na awamu ya nne ya Rais mstaafu Jakaya Kikwete.
 
Ni mapambano mazuri ambayo yalisaidia kuikumbusha serikali hizo dhidi ya ufisadi na matumizi mabaya ya fedha za umma hapa nchini.
 
Sasa tupo katika uongozi wa awamu ya tano ya Rais John Magufuli ambaye amekuja na kauli mbiu ya 'kutumbua majipu' ikiwa ni namna ya kipekee ya kupambana na ufisadi.
 
Anafanya hivyo baada ya kukiri kwamba alikuta uozo mkubwa ndani ya serikali na kwamba ni kazi kubwa kutumbua majipu na anahitaji Watanzania wamuombee kwa Mungu.
 
Ametangaza kujitoa sadaka ili kuikomboa nchi hii dhidi ya vitendo viovu vya ufisadi.
Moja ya wapinzani ambao wamekuwa mstari wa mbele kupambana na ufisadi hadharani ni mwanasiasa kijana, David Kafulila.
 
Kafulila ambaye alikuwa Mbunge wa Kigoma Kusini (NCCR-Mageuzi) kati ya 2010 hadi 2015, anasema juhudi za Rais Magufuli zinapaswa kuungwa mkono na watu wote.
 
Mwanasiasa huyo akizungumza katika mahojiono maalum anasema, wazalendo wote wanapaswa kumuunga mkono kwa sababu mapambano haya yanaleta nidhamu ya utendaji serikalini.
 
Anasema kwa muda mrefu serikali zote zilikuwa katika hali mbaya katika nidhamu ya utendaji ambao ulitokana na kuwapo mfumo mbovu.
 
 Kikubwa anachokisema Kafulila ni kujenga mfumo imara ambao utasimamia nidhamu ya matumizi ya fedha za umma hata kama Rais Magufuli atamaliza kipindi chake na kuondoka.
 
"Rais anatakiwa ajenge mfumo unaotisha ili hata  asipokuwapo kwa sababu yoyote ile nchi ibakie na nidhamu ya utendaji kazi na hofu ya ufisadi.
 
Kafulila anasema panapokuwa  na mfumo mzuri wa utendaji  kazi hata kiongozi mwingine anapokuja lazima atabanwa ili afanye hiki kinachofanywa na Rais Magufuli kwa sasa.
 
Hata hivyo, Kafulila anasema  Rais Magufuli anapaswa kutambua kuwa hofu ya sasa ni ya muda mfupi kwani anaogopwa yeye na sio mfumo.
 
Anasema kuwa njia pekee ya kuhakikisha hilo linatendeka ni pamoja na kuwapo kwa katiba mpya itakayojenga mifumo thabiti katika utendaji kazi.
 
“Zaidi anapaswa kuruhusu demokrasia hasa ya Bunge ili limsaidie kutumbua majipu kwani peke yake hawezi,” anasema Kafulila.
 
SAKATA LA UFISADI  WA KASHFA YA ESCROW 
Kafulila ambaye alijinyakulia umaarufu bungeni baada ya kuibua tuhuma nzito akiwahusisha mawaziri wawili kuhusika katika uchotwaji wa fedha zaidi ya bilioni 200 katika akaunti ya Tegeta Escrow iliyokuwa inamilikiwa kwa pamoja kati ya Shirika la Umeme (Tanesco) na kampuni ya kufua umeme ya  IPTL.
 
Kuhusu sakata la Escrow anasema anachokiona kwa Rais Magufuli bado anaivutia pumzi.
 
”Simuoni  akiigusa ingawa sioni akiicha iendelee,” anasema Kafulila.
Anasema anachokifanya kwa sasa ni kuhangaika na kesi yake ya kupinga ushindi alioupata mgombea wa CCM katika jimbo la Kigoma Kusini mwaka jana.
 
Anakiri kwamba alikuwa mwiba mkali kwa serikali ya Kikwete na kwamba bado anawaza kuendelea na juhudi hizo za kupinga ufisadi hadharani.
 
Mwanasiasa huyo kijana anasema  kinachofanywa na Rais Magufuli hususani kuwafukuza wezi wa fedha za umma kwa sasa mtu anaweza kudhani Ikulu haikuwa na Rais miaka mitano iliyopita.
 
Akizungumzia uchaguzi wa mwaka jana, Kafulila anasema ulikuwa na ushindani mkali ambao haujawahi kutokeo katika chaguzi zote zilizowahi kufanyika nchini.
Kafulila anasema ushindani huo ulikuwa ni jaribu  kwa mfumo kuona kama upo imara  kusimamia uchaguzi wa ushindani kuanzia ngazi ya Udiwani, Ubunge na Urais.
 
“Jambo moja kubwa nililoliona ni udhaifu wa mfumo hasa kuanzia kwa Tume ya Taifa ya  Uchaguzi (NEC),  kunahitajika mabadiliko ya kikatiba kwa sababu kwa kiasi kikubwa hii ni Tume ya serikali na siyo ya umma,” anasema Kafulila.
 
Anasema mfumo unaifanya iwe hivyo kwamba wasimamizi wote wa uchaguzi kwenye majimbo ambako kunaamua nani awe mbunge na diwani na hata Rais ni watendaji kata na wakurugenzi ambao hakika ni sehemu ya Tamisemi ambao ni serikali.
 
“Sheria inasema wasimamizi hao wa uchaguzi ndiyo wenye kauli za mwisho katika kumtangaza mshindi, na baada ya hapo labda mtu aende mahakamani,"  anasema Kafulila.
 
Anatoa mfano kwamba kama NEC ingekuwa kwa ajili ya wananchi ingeweza kutatua migogoro mingi ya uchaguzi na kuimaliza na isingeenda mahakamani.
 
Kafulila anatoa mfano kuwa kuna wagombea wanalalamika kwamba alitangazwa mshindi ambaye hakushinda  na fomu za matokeo zinaonyesha hivyo na kwamba jambo kama hilo lingepaswa  kuishia kwa Tume kwa mfumo wa rufaa na kurekebisha kasoro kama hizo.
 
Anasema masuala ya kufikishana mahakamani yangebaki yale ambayo yanayohitaji sayansi kubwa kutambua haki ni ya nani.
 
Kafulila alishauri kuwa serikali iondolewe kwenye mfumo wa Tume ili iajiri watu wake watakaowajibika kwa yenyewe na siyo kuwa na watumishi wanaowajibika kwa serikali.
 
NAFASI YA VYAMA VYA UPINZANI KWA SASA.
Akizungumzia nafasi ya upinzani kwa sasa anasema kuwa bado upinzani una nafasi kubwa hasa ukizingatia kuwa Rais Magufuli ameeleza yupo tayari kujiuzulu urais kama akishindwa kupambana na ufisadi.
 
Anasema hoja ya ufisadi ni ya upinzani kwa miaka mingi, hivyo nafasi ya upinzani bado ipo hususani kumuelekeza Rais yalipo majipu.
 
“Jambo la msingi ni Rais asimamie kwa dhati kauli yake kuwa yeye ni rais wa wote  bila kujali itikadi za  siasa,  dini,  rangi wala ukanda na kikabila kwani itamsaidia kujenga uwajibikaji,” anasema.
 
Aliongezea kuwa “Rais aone upinzani ndiyo ustawi wa taifa lake, kwani hata yeye,  asingepewa nafasi ya kugombea kupitia CCM kama CCM isingehofu upinzani. 
 
Alionekana kama mtu anayeweza kukabili wimbi la mabadiliko ili kuinusuru CCM ndio sababu akapewa siyo kwamba wenye CCM walimpenda,” anasema Kafulila.
 
Kuhusu serikali ya sasa ya  CCM  kama imekidhi kiu ya upinzani kwa kile walichokuwa wanakililia kwa miaka mingi, Kafulila anasema kuwa bado ni mapema kusema haya.
 
“Bado hata mwaka haujamalizika siasa zinaendelea tena kwa kasi, hata serikali ifanye nini upinzani utazidi kukua kwani unaweza kubadili mbinu ndiyo maana nchi zenye maisha bora duniani kama Finland bado kuna upinzani mkali,” anasema Kafulila.
 
MAISHA YAKE KISIASA BAADA YA KUSHINDWA UBUNGE
Kafulila anasema yeye bado ni mwanachama halali wa NCCR-Mageuzi na pia ni Katibu mwenezi Taifa.
 
“Sijui habari za kuhama NCCR msingi wake ni nini,  kwa sasa nipo mahakamani nashughulika na kesi ya ubunge wangu hilo ndilo jambo kubwa naweza kusema hayo mengine sina nafasi kuyazungumzia,” anasema Kafulila.
CHANZO: NIPASHE

JULIUS MTATIRO AHOJI UKIPEWA SHS.LAKI NNE UTAWEZA KUENDESHA SHULE MWEZI MZIMA ?

UKIPEWA SHS. LAKI NNE UTAWEZA KUENDESHA SHULE MWEZI MZIMA?
Mpango wa serikali wa elimu bure unaonesha kuwa serikali inatenga shilingi elfu kumi (10,000) kwa mwaka mzima kwa kila mwanafunzi wa shule ya msingi. Hiyo ina maana kwamba kila mwanafunzi anapelekewa shilingi 833 za kutumia mwezi mzima - kama shule ina wanafunzi 500 inapelekewa shilingi 416,500 kwa mwezi.


Kama shule moja ina walinzi wawili na inawalipa shs 150,000 kwa mwezi mmoja ina maana fedha zinazotumwa zinaishia kwa walinzi na kubakiza shilingi 116,500. Hizi zikitumika kulipa maji na umeme haibakii hata senti tano. Nimeongea na baadhi ya walimu wakuu wanasema wamechanganyikiwa na hawajui cha kufanya.


Sijui kama mahitaji ya shule zetu yamekamilika? Hebu serikali ijipange zaidi ili tusije kuzua bomu jingine kwenye elimu. “Pump more money on education”, hakuna njia nyingine!

HATIMAYE ALPHONSE MAWAZO AZIKWA KIJIJINI KWAO GEITA


Mheshimiwa Edward Lowassa na Mheshimiwa Freeman Mbowe wakiwa kijijini alipozaliwa Alphonse Mawazo ambapo shughuli za mazishi zimefanyika.

Mke wa Alphonse Mawazo akishriki mazishi ya mumewe yaliyofanyika Kijijini kwao Mkoani Geita.
Mtoto wa Alphonse Mawazo Preciuos Mawazo akionekana mwenye sura ya huzuni wakati wa mazishi ya Marehemu baba yake.
Precious Mawazo akibusu mwili wa marehemu baba yake.


Jeneza lililobeba mwili wa Alphonse Mawazo likiingizwa kwenye kaburi.








Mgombea urais wa UKAWA kupitia Chadema Mh Edward Lowassa akiwa na Mwenyekiti wa chadema Mh Freeman Mbowe wakiangalia mahali ambapo Alphonse Mawazo aliuawa.

CHADEMA YATEUA MEYA MANISPAA YA KINONDONI


CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Mkoa wa Konondoni, kimempitisha Diwani mteule wa Ubungo, Boniface Jacob (Chadema), kuwa mgombea umeya wa Manispaa ya Kinondoni, huku akiwakilisha mwamvuli wa vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).

Mgombea huyo alikuwa akiwania nafasi hiyo huku akipambana na diwani mwenzake mteule wa Kata ya Mbweni, Abdunel Elibariki (Chadema) ambaye alishindwa kutamba.
 
Akitangaza matokeo ya uchaguzi huo jana jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa uchaguzi huo Venus Kimei , alisema Jacob alishinda kwa kura 20 kati ya kura 28 zilizopigwa.

“Wagombea walikuwa wanne lakini watatu ndio ambao walikidhi vigezo, hata hivyo waliopigiwa kura ni wawili kutokana na mgombea mmoja Ndeshukurwa Tungaraza ambaye ni Diwani mteule wa Kata ya Makongo kujitoa katika hatua za mwisho,” alisema.

Akizungumza baada ya kutangazwa kushinda kinyang’anyiro hicho, Jacob alisema ana imani atashinda katika uchaguzi utakaowajumuisha wagombea wa vyama vingine kikiwamo Chama Cha Mapinduzi (CCM).

“Nitasimamia kwa vitendo sera ya elimu ambayo chama chetu iliisimamia katika kampeni na jambo zuri ni kwamba hata Rais Dk. John Magufuli amesisitiza kwamba watoto wasome bure kuanzia msingi hadi sekondari.


“Hivyo ninaamini hilo linawezekana endapo tutasimamia mapato ya ndani kwa umakini nataka Manispaa Kinondoni iwe mfano katika hili ambayo tutahakikisha tunaboresha maslahi ya walimu na kuondoa kabisa michango ya aina zote,” alisema.


Alisema atasimamia kwa kuzingatia sera ya utatu akijumuisha wananchi, wanasiasa na wataalam bila kuwabagua kwani kwa pamoja watainua maendeleo ya manispaa hiyo.

Kwa upande wa Chama cha Wananchi (CUF), ambacho ni mshirika wa Ukawa, kinatarajia kumsimamishwa Diwani mteule wa Kata ya Tandale, Jumanne Mbunju (CUF) ili awanie nafasi ya unaibu meya wa manispaa hiyo.

Katika Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni yenye majimbo manne, Chadema imenyakua majimbo matatu ambayo ni Ubungo, Kawe na Kibamba, huku jimbo moja la Kinondoni likienda CUF.

Kata zinazounda halmashauri hiyo ni 34 ambapo Chadema ilishinda kata 18 na kupata madiwani wa viti maalumu 7, CCM kata 11 na viti maalumu 4 na CUF ikishinda kata 5 na viti maalumu 2.

LOWASSA AWATEMBELEA WAHANGA WALIOOKOLEWA MGODINI BAADA YA KUFUKIWA NA KIFUSI SIKU 41



Mgombea urais kwa tiketi ya CHADEMA Edward Lowassa Jana alitoa shilingi milioni mbili kwa wahanga waliookolewa katika mgodi wa Nyangalata wanaopatiwa matibabu katika hospitali ya halmashauri ya mji wa Kahama mkoani Shinyanga.

Akikabidhi fedha hizo kwa wahanga hao, Lowassa alisema ametoa fedha hizo kama msaada ili ziwasaidie kwa matibabu kwa muda wote watakapokuwa hospitalini hapo, ambapo kila mmoja amepatiwa shilingi laki tano.

Mmoja wa wahanga hao, Joseph Burule alisema kitendo cha Lowassa kuwatembelea hospitalini hapo kimewapa faraja kubwa, kwani tangu waokolewe na kuanza kupatiwa matibabu hakuna kiongozi mkubwa aliyefika kuwajulia hali pamoja na kuwapa pole.

Burule alisema kitendo hicho kinatakiwa kuwa mfano wa kuigwa kwa viongozi pindi linapotokea jambo la kusikitisha kama hilo, na kusema kuwa fedha hizo zitawasaidia kujikimu hospitalini hapo.

Kwa upande wake Mbunge wa viti maalumu Mkoa wa Shinyanga kupitia CHADEMA Salome Makamba aliwaambia wananchi waliojitoza kumsabahi Lowassa kuwa, Lowassa amekuja kuwapa pole wahanga hao na hakuja kwa masuala ya kisiasa.

Novemba 15, 2015 wahanga 5 kati ya 6 waliofukiwa na kifusi katika machimbo ya nyangalata wilayani kahama waliokolewa wakiwa hai baada ya kukaa ndani ya mashimo kwa siku 41, ambapo juzi mmoja kati yao alifariki dunia.

Ni hivi karibuni baada ya kuokolewa mmoja wa wahanga hao alikaririwa akimuulizia Lowassa kama alishinda urais wa  Tanzania kwenye uchaguzi na baada ya kuambiwa hakushinda alikosa raha.

JULIUS MTATIRO:SEGEREA HAKUNA KESI YA KUFUNGUA

Napenda kutoa taarifa hii rasmi na ya awali kwa wananchi wa Segerea na watanzania wote ambao walipigana kufa na kupona ili kuhakikisha UKAWA tunashinda madiwani, mbunge na kuongoza kura za Rais hapa jimboni. Kwa bahati mbaya tulifanikiwa kushinda madiwani wote, kuongoza kura za Rais lakini tukashindwa kwenye Ubunge.

Baada ya jimbo letu kwenda CCM nilishauriwa nisisaini kukubali matokeo na nikatekeleza ushauri huo, lengo lilikuwa ni kuwapa muda wanasheria wetu na mawakili waweze kushauri ikiwa kuna kesi ya kufungua kupinga ushindi wa CCM.

Baada ya mashauriano ya wiki kadhaa yaliyohusisha mawakili na wataalam wa sheria wa ngazi mbalimbali, tumejiridhisha na kushauriwa kwamba hatutakuwa na kesi ya kufungua, na kwamba tukiifungua kwa kulazimisha au "kwa kusukumwa na upepo wa wananchi" tutashindwa mahakamani mapema.

Wanasiasa wengi hukimbilia mahakamani wanaposhindwa uchaguzi si kwa sababu wana kesi zenye ushahidi wenye mashiko, bali huogopa maneno na tuhuma wanazoweza kupewa kuwa "wamenunuliwa na wagombea wa CCM", mimi kwa bahati nzuri sijakumbwa na upepo huo na natambua wananchi wa Segerea wananiamini kiasi cha kutosha.

Baada ya wiki moja kutoka sasa, ntatoa taarifa rasmi na ya kina juu ya hoja na sababu zilizopelekea wanasheria na mawakili wetu washauri tusihangaike kufungua kesi na kupoteza muda wa matumaini ya wananchi.

Mtatiro Julius,
Segerea.

ZITTO KABWE ABAKI BUNGENI HUKU UKAWA WAKITOLEWA NA SPIKA


JE Unakichukuliaje Kitendo cha ZITTO KABWE Kubaki Bungeni Wakati Wabunge wa Upinzani Wote Wametoka Nje Kushinikiza Maalim Seif Atangazwe Mshindi wa Urais Zanzibar?
Toa Maoni yako

LIVE TOKA BUNGENI: Rais Magufuli Ampa Hongera Zitto Kabwe Kwa Kutokuleta Fujo Bungeni na Kubakia Ndani ya Bunge Wakati Ukawa Wametoka

LIVE TOKA BUNGENI:Muda huu Rais Magufuli Anatoa Hotuba yake ndani ya Bunge na Amempa Hongera Zitto Kabwe Kwa Kutokuleta Fujo Bungeni na Kubakia Ndani ya Bunge Wakati Ukawa Wametoka Baada ya Kutolewa na Spika kutokana na Utovu wa nizamu walioonyesha kwa Kupiga Makelele

Yanayojiri Bungeni Dodoma Muda Huu..Wabunge wa Ukawa Walianzisha na Kutolewa Nje ya Bunge na Spika

Wabunge  wanaounga  umoja  wa  Katiba  Ya  Wananchi, UKAWA  wametolewa  nje  ya  ukumbi  wa bunge  muda  huu  baada  ya  kugoma  kutambua  ujio  wa  Dr Shein bungeni  na  kuanza  kuzomea  huku  wakisema  Maalim Seif....Maalim Seif

Spika  wa  bunge,Job Ndugai  aliwataka  wabunge  hao waache kuzomea  na  badala  yake  wakae chini  lakini  wakakaida, hali  iliyomfanya  awaamuru  watoke  nje kwa  hiari  yao  kabla  nguvu  ya  dola  haijatumika  kuwatoa.

LIPUMBA AIBUKA SASA ATOKA KIVINGINE


prof+LipumbaAliyekuwa Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba.
Na Gabriel Ng’osha
HATIMAYE mwenyekiti wa CUF aliyejiuzulu, Profesa Ibrahim Lipumba (pichani) ameibuka na kumgeukia rais wa awamu ya tano, Dk. John Pombe Magufuli ambaye anatarajiwa kuhutubia Bunge leo kwa kumuambia kuwa ana mzigo mzito kutokana na hali ngumu ya bajeti ya nchi.


Akizungumza jana na wanahabari katika ofisi za chama hicho zilizopo Buguruni jijini Dar, Profesa Lipumba alisema Rais Magufuli anakabiliwa na mambo kadhaa yakiwemo ya hali ngumu ya bajeti ya serikali kufuatia taarifa (iliyopo kwenye tovuti) ya Benki Kuu ya Tanzania kuonesha kuwa mwaka wa fedha 2014/2015 serikali ilipanga kukusanya mapato ya ndani ya shilingi bilioni 12,178, sehemu kubwa ikiwa ni makusanyo ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na badala yake serikali ilikusanya shilingi bilioni 10,507.

dk magufuli 
Rais Dk. John Pombe Magufuli.
Alisema mapato halisi ni madogo ukilinganisha na bajeti kwa kiasi cha shilingi bilioni 1,671 sawa na asilimia 14 ya malengo ya bajeti ya serikali.


Aliongeza kuwa halmashauri za wilaya, miji na majiji zilitarajiwa kukusanywa shilingi bilioni 458.5 lakini zilifanikiwa kukusanywa shilingi bilioni 360.1 sawa na asilimia 78. ya malengo ya bajeti.


Kwa upande wa misaada, Profesa Lipumba ambaye ni mtaalam wa uchumi alisema kuna bajeti ya shilingi bilioni 1,481 lakini zilitolewa shilingi bilioni 1,024, upungufu ukiwa ni shilingi bilioni 457 sawa na asilimia 31 ya bajeti huku mikopo yenye masharti nafuu ya shilingi bilioni 1,000 ikafanikiwa kwa kupatikana shilingi bilioni 859.


Akizungumzia Tume ya Uchaguzi ya Zanziba (Zec), Lipumba amemtaka Rais Magufuli kutumia uamiri jeshi wake mkuu kuzungumza na kuishauri Zec kumtangazab mshindi wa urais na siyo kurudia uchaguzi kama serikali ya CCM Zanzibar inavyotaka.


“Kila kitu kiko wazi, mawakala walipata nakala za kila jimbo kwa majimbo yote 54, binafsi namuomba Rais Magufuli aishauri Zec itangaze matokeo halisi,”alisema Lipumba.


Aliongeza kuwa kwa kasi ya Rais Magufuli naungana naye katika kauli mbiu yake ya “Hapa Kazi Tu”, lakini alimtaka azingatie kauli nyingine ya “HAPA HAKI TU’’ili kuinusuru nchi isiingie kwenye machafuko yasiyo na msingi.


“Nampongeza kwa ziara zake za kushtukiza, tumeona zinazaa matunda mfano mzuri ni Hospitali ya Muhimbili baada ya kufika pale mashine za CT Scan na MRI zilitengemaa lakini ziara hizo hazitakuwa na tija kama bajeti ya maendeleo haikidhi matatizo ya Watanzania kama vile afya bora, elimu, ajira, kupambana na rushwa, miundo mbinu na kilimo ili kuwe na chakula cha kutosha nchini.


Aidha, Lipumba amempongeza Waziri Mkuu Mteule, Majaliwa Kassim Majaliwa kwa kuteuliwa kushika wadhifa huo na Bunge kumpitisha.


“Naweza kusema Majaliwa ni kama kaokota embe dodo chini ya mpapai, Rais Magufuli hajakosea sana kwani yeye ndiye kiongozi na mtendaji mkuu, hivyo aliyeteuliwa anafaa kufanya naye kazi kwa karibu zaidi. Ingawa inampasa ajenge uwezo mkubwa sana wa kuwaongoza na kuwakabili wabunge pamoja na baadhi ya vigogo ambao nao walikuwa wanategemea wachaguliwe uwaziri mkuu,” alisema.

RATIBA RASMI YA MAZISHI YA ALPHONCE MAWAZO ALIYEKUA MWENYEKITI WA CHADEMA MKOA WA GEITA.



Waheshimiwa Viongozi nitumie fursa hii kuwajulisha ratiba ya mazishi ya Mhe. Kamanda A. C. Mawazo. Kama ifuatavyo:

1. Tarehe 21/11/2015 kuaga mwili jijini MWANZA uwanja wa Furahisha na muda SAA 8 -12 jioni.

2.Tarehe 22/11/2015 kuaga mwili Geita, saa 6-10 jioni.

3.Tarehe 23/11/2015 ni Mazishi Kijiji Chikobe Busanda-Geita,nyumbani kwa Marehemu.

UKAWA:TUTAMPOKEA MAGUFULI BUNGENI KWA STAILI MPYA


Rais Dk. John Magufuli
 Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), umesema utakuja na stahili mpya wakati  Rais Dk. John Magufuli, atakapokwenda  kuzindua na kuhutubia Bunge Novemba 20, mwaka huu.
 
Umesema staili watakayoitumia ni tofauti na ile waliyoitumia wakati Rais wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete, alipozindua Bunge la 10 mwaka 2010 ya kutoka nje ya ukumbi kuonyesha kutotambua serikali yake.
 
Akizungumza na Nipashe katika viwanja vya Bunge mjini Dodoma jana, aliyekuwa Mnadhimu wa Bunge la 10 Kambi la Upinzani Bungeni, Tundu Lissu, alisema safari hii hawatatoka nje ya ukumbi wa Bunge  hata kama hawamkubali Rais Magufuli, kwa kuwa ni wajibu wao kushiriki vikao vya chombo hicho cha kuwakilisha wananchi.
 
“Sisi ni wabunge, tumo humu kwa ridhaa ya wananchi, tuna haki ya kuingia bungeni, hivyo siku hiyo tutaingia lakini kitakachotokea tutajua siku hiyo, bali haitakuwa kama walivyotuzoea tunatoka nje,” alisema na kuongeza:
 
“Subira yavuta heri, bado siku tatu tu, Watanzania watajua msimamo wetu tukiwa ndani ya Bunge,” alisema.
 
Hivi karibuni aliyekuwa mgombea urais wa Ukawa kupitia Chadema, Edward Lowassa, alisema hawatambui matokeo yaliyotangazwa naTume yaTaifa ya Uchaguzi (Nec) na kumpa ushindi Rais Magufuli na kwamba hawatashirikiana na serikali yake kutokana na kile alichoeleza kuwa uchaguzi mkuu uligubikwa na wizi wa kura na kuporwa ushindi.
 
CHANZO: NIPASHE

HII NDIO SABABU YA POLISI KUPIGA MABOMU WAFUASI WA CHADEMA HOSPITALI YA BUGANDO ,MWANZA

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mwanza, Charles Mkumbo.
NA DANIEL MKATE

Jeshi la Polisi jijini Mwanza, jana lilitumia nguvu ndani ya Hospitali ya Rufaa Bugando baada ya kuvurumisha mabomu ya kutoa machozi 12 kwa lengo la kuwatawanya wafuasi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).

Tukio hilo lililotokea jana saa 11:30 jioni, liliibuka baada ya baadhi ya viongozi wa Chadema kuzungumza na wafuasi wao waliokwenda kuusindikiza mwili wa aliyekuwa Mwenyekiti wa chama hicho Mkoa wa Geita, Mawazo Alphonce, kwa ajili ya hifadhi.

Hata hivyo, licha ya hospitali hiyo kumilikiwa na Baraza la Maaskofu nchini (Tec), polisi hawakuonea huruma wagonjwa waliolazwa ndani yake na kuamua kuvurumisha mabomu hayo.

Akizungumza na waandishi wa habari hospitalini hapo, mgombea ubunge wa Jimbo la Arusha Mjini, Godbless Lema, aliwataka wafuasi wa chama hicho kukutana ofisi za kanda za chama hicho jijini Mwanza ili kuzungumzia tukio hilo.

“Hapa ni chumba cha kuhifadhi maiti, hivyo tukutane katika ofisi za kanda ambako tumeweka msiba wa kamanda wetu …tukusanyike hapo wote kwani viongozi wetu waliopo Dar es Salaam na Dodoma wanakutana kwa ajili ya tukio hili…hapa hatupo kwa ajili ya kukuna nazi,” alisema Lema.


Alisema hawatakaa vikao vya kuwafundisha wafuasi wao ujinga, bali vikao watakavyokaa ni vya kutiana ujasiri.

Wafuasi hao walianza kupigwa mabomu baada ya kusemekana askari polisi mmoja kuingia katika chumba cha kuhifadhi maiti cha hospitali hiyo kwa madai alitaka kuuchukua mwili wa Mwenyekiti huyo na kuutorosha. Askari huyo alianza kushambuliwa na wafuasi hao ambao walioonekana kuwa na hasira za majonzi za kuuliwa mwenyekiti huyo.

Mwenyekiti huyo alishambuliwa na watu wasiojulikana juzi saa 6:00 mchana kwa kukatwa mapanga na shoka kichwani na sehemu mbalimbali za mwili wake na kumsababishia umauti.

Mawazo ambaye pia alikuwa mgombea ubunge wa Jimbo la Busanda mkoani Geita, atazikwa baada ya mwili wake kufanyiwa uchunguzi.

Alishambuliwa kijijini Katoro wakati akiwa katika bodaboda akielekea kata ya Ludete.

Hata hivyo, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mwanza, Charles Mkumbo, alipotakiwa na Nipashe kuzungumzia tukio hilo, alitaka apigiwe baadaye, lakini hadi gazeti hili linakwenda mitamboni, hakupatikana.

CHANZO: NIPASHE
Chediel . Powered by Blogger.
© Copyright Rundugai Blog
Back To Top