Rais
wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein, amekutana na kuzungumza kwa saa
sita na nusu na mgombea mwezake wa urais kupitia CUF, Maalim Seif Sharif
Hamad, kujadili mgogoro wa uchaguzi, baada ya Mwenyekiti wa Tume ya
Uchaguzi Zanzibar (Zec), Jecha Salim Jecha, kufuta matokeo.
Uchaguzi huo ulifanyika Oktoba 25, mwaka huu na Jecha alitangaza kuufuta Oktoba 28, kwa madai kuwa kulikuwapo na kasoro kadhaa.
Taarifa zilizopatikana kutoka vyanzo vyetu mbalimbali, zimeeleza
kwamba kikao hicho kati ya Rais Shein na Maalim Seif, ambaye pia ni
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, pia kilihudhuriwa na viongozi
kadhaa wastaafu.
Viongozi hao ni Rais mstaafu wa Janhuri ya Muungano wa Tanzania,
Ali Hassan Mwinyi na Rais mstaafu wa Zanzibar, Amani Abeid Karume.
Mazungumzo hayo yalifanyika Ikulu ya Zanzibar na kumalizika saa
kumi jioni na ajenda kubwa ilihusu mgogoro wa uchaguzi visiwani humo.
Mkurugenzi wa Mawasiliano na Kampeni wa CUF, Ismail Jussa Ladhu,
alithibitisha viongozi hao wakuu wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK)
kukutana, lakini alisema hafahamu mambo yaliyojadiliwa katika kikao
hicho.
“Kweli wamekutana kwa mazungumzo baada ya Zanzibar kukubwa na
mgogoro wa uchaguzi, lakini mimi nipo Dar es Salaam, sifahamu
kilichoendelea katika kikao hicho,” alisema Jussa, baada ya kutakiwa
kueleza ajenda madhumuni ya kikao hicho pamoja na ajenda zilizojadiliwa.
Kwa upande wake Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais wa Zanzibar, Salum
Maulidi Kibanzi, alisema hafahamu chochote kwa sababu yuko safari nje ya
Zanzibar.
“Watafute wahusika mie nipo safari nje ya Zanzibar,” alisema Kibanzi.
Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu, Hassan Khatibu, alisema hana
taarifa zozote kuhusiana na kikao hicho kwa sababu yupo nje ya ofisi na
kutaka watafutwe wasaidizi wa Rais.
Hata hivyo, Katibu Mkuu Kiongozi, DK Abdulhamid Yahya Mzee,
hakupatikana, kutokana na simu yake ya kiganjani kuiita zaidi ya mara
moja bila kupokelewa, baada ya kumalizika kwa kikao hicho.
Hata hivyo, chanzo kimoja kimeeleza kuwa hatua ya Mwenyekiti Zec
kufuta matokeo ya uchaguzi na hatua ya Maalim Seif kujitangaza mshindi
kabla ya Zec kutangaza matokeo ni mambo yaliyochukua nafasi kubwa
kujadiliwa pamoja kasoro zilizodaiwa na Jecha wakati akitangaza kufuta
matokeo ya uchaguzi huo.
Imeelezwa kuwa viongozi hao wastaafu waliombwa kushiriki katika
kikao hicho kwa lengo la kuongeza nguvu na kutumia busara katika
kutafuta ufumbuzi wa mgogoro huo.
Karume ndiyo alieweka msingi wa maridhiano, baada ya Zanzibar
kukumbwa na mpasuko wa kisiasa wa muda mrefu tangu uchaguzi wa kwanza
baada ya kurejeshwa kwa mfumo wa vyama vingi uliofanyika mwaka 1995 na
kuundwa kwa SUK Novemba, 2009.
Juhudi za kutafuta maelewano zimekuja wakati vyama vya CUF na CCM
vikiwa vimegawanyika kufutia uamuzi wa Jecha kufuta matokeo ya uchaguzi
mkuu wa Zanzibar.
Wakati CCM wanaunga mkono uamuzi wa kurudiwa uchaguzi huo, CUF
inasisitiza kuwa haikubaliani na uamuzi wa kurudiwa na kwamba
haitashiriki, kwa kuwa inasubiri Maalim Seif aapishwe kwa madai kuwa
alishinda.
CUF inamtaka Jecha aendelee kuhakiki majimbo yaliyobakia na kumtangaza mshindi wa uchaguzi huo.
Uamuzi wa Jecha umekuwa ukipingwa na waangalizi mbalimbali wa
uchaguzi wa kitaifa, kimataifa pamoja na mataifa kadhaa yakiwamo
Uingereza, Ireland na Marekani, wakisema hakuna kasoro zilizobainika
wakati wa uchaguzi huo na kuishauri Zec kuendelea na mchakato wa
kutangaza matokeo.
Wakati mgogoro huo ukiendelea, kumekuwapo na jitihada za upatanishi
zinazofanywa na viongozi wa dini, Msajili wa Vyama vya Siasa na
viongozi wastaafu.
CHANZO:
NIPASHE
Post a Comment