Featured

    Featured Posts

    Social Icons

Loading...

KUEPUKA KUBOMOLEWA, KUFUTIWA UMILIKI JIEPUSHE NA HAYA.

Image result for BOMOABOMOA DAR

NA  BASHIR  YAKUB -

Serikali  mpya  imeanza  kwa  kasi  kubwa kufuta  umiliki  wa  viwanja  nyumba na  kubomoa  yale  maeneo  yote  wanayoona  hayastahili. Upo  umuhimu  wa  kujua  namna  ya  kuepuka  kuingia  katika  janga  hili.

1.Kifungu cha 45 (2)(i-vi) cha Sheria ya Ardhi kinaeleza sababu za msingi zinazoweza kusababisha mhusika kubomolewa, kufutiwa umiliki ardhi kama ifuatavyo :

( a ) Kwanza iwapo eneo limetelekezwa kwa muda usiopungua miaka miwili. Muda usiopungua miaka miwili maana yake ni kuanzia miaka miwili na kwenda mbele. Kutelekeza eneo kwa mujibu wa maana hii hapa ni pamoja na kutoonekana ukishughulika na eneo lako kwa namna yoyote tangu upatiwe umiliki.

( b ) Jaribio lolote la kutaka kuuza au kugawa ardhi kwa mtu asiyekuwa Mtanzania. Ni kosa mtu asiyekuwa raia wa Tanzania kumiliki ardhi, hivyo jaribio lolote la kumpatia ardhi linatosha kuwa kosa la kufutiwa umiliki.

( c ) Epuka  kujenga  maeneo  ya  wazi, maeneo  yaliyotengwa  kwa  ajili ya  miundo  mbinu, na  huduma  nyingine  za  umma. Kufanya  hivyo  hutafsiriwa  kama  kuukosesha  umma  manufaa  yaliyokusudiwa  na  ni  kinyume  na tamko  namba 6.6.1 la  sera  ya  taifa  ya  ardhi  ya  mwaka 1995.

 ( d ) Jaribio lolote la kutoa ardhi kwa mamlaka nyingine kinyume na namna ulivyoagizwa na mamlaka wakati unapewa eneo husika.

(  e  ) Kutumia eneo kinyume na masharti yaliyo kwenye hati ikiwa ni pamoja na matumizi yoyote yaliyo kinyume na sheria ya ardhi, sera, miongozo na kanuni zake.

(  f  ) Pia, Rais kwa mamlaka aliyonayo, anaweza kufuta umiliki wa ardhi ya mtu yeyote kwa sababu zozote zinazohusu maslahi ya umma.

2.HATUA  ZA  KISHERIA  ZA KUCHUKUA  KUEPUKA  MIGOGORO  YA  KUBOMOLEWA NA  KUFUTIWA  UMILIKI.

Namna  ya  pekee  ya  kuepuka  kubomolewa na  kufutiwa  umiliki  ni  kufuata  taratibu. Mara  kadhaa  nimeandika  kuhusu  taratibu  rasmi  za  upatikanaji  wa  ardhi.  Ni  taratibu  maalum  za  upoatikanaji  wa  ardhi  pekee  zinazoweza  kukuepusha  na  hasara  kubwa  inayotokana  na  majanga  kubomolewa  na kufutiwa  umiliki. Hatua  za  kuepuka  majanga  haya  huanza  tu  pale  unapotaka  kununua  ardhi. Unapokosea  katika  taratibu  za  ununuzi  wa  ardhi ni  hapo  unapokaribisha   majanga  kama haya.  Zingatia  yafuatayo  ili  kuepuka  kuingia  katika  janga  hili  leo  na huko  mbeleni :

 ( a )  Kitu  cha  kwanza  kabisa  na  cha  muhimu  ni  kufanya  utafiti  maalum  wa  kisheria kama  tutakavyoona
Kama kiwanja/nyumba  ina hati  kuna maombi  rasmi ya kisheria  ambayo  huwa yanafanywa  kwenda  ardhi  wizarani, wizara  ya ardhi makao makuu   kwa Dar es salaam na  kwa mikoani maombi  hayo  mara nyingi huenda makao makuu ya  mkoa ambapo   katika  maombi hayo  mnunuzi  anaiomba  mamlaka ya ardhi  imjulishe mambo yafuatayo;

( b ) Katika  maombi  hayo  unaweza  kuomba kujua hadhi(status)  ya  kimatumizi  ya  eneo  unalonunua  kutokana    na  taratibu  za  mipango  miji. Eneo  kuwa  na  hati  si  hoja  kuwa  linaruhusiwa  kufanyiwa  chochote. Eneo  linaweza  kuwa  na  hati  na  nyumba  ya makazi  ndani  mwake  lakini  kumbe kimipango  miji hapakutakiwa  kuwa  na  makazi . Kawaida  mnunuzi  akiona  hati  na  watu  wanaishi  ni  rahisi  kushawishika  kununua  na  kujikuta  ameingia  kwenye  matatizo. Kwa  hiyo  ni  muhimu  kabla  ya  kunnua  kufanya  utafiti(official  search)  ili  kujua  hadhi(stastus) ya  eneo. Mbali  na  hilo  mambo  mengine  unayoweza  kujua kupitia  utafiti (official  search)  ni  haya :
  
KUJUA  JINA  LA  MMILIKI  HALALI  WA NYUMBA/KIWANJA.

Kujua  jina la mmiliki. Jina hili linatakiwa kufanana sawasawa  bila tofauti yoyote  na yule mtu anayetaka  kukuuzia eneo. Hii husaidia kuthibitisha  kuwa  anayeuza ndiye kweli mmiliki wa eneo.Kama majina yatatofautiana basi haraka sana  achana na hilo eneo ili kuepuka mgogoro.

KUJUA  KAMA  NYUMBA/KIWANJA  UNACHONUNUA  KIMEWEKWA KAMA   DHAMANA  YA  MKOPO.

Kitu  kingine unachouliza kwenye hayo  maombi rasmi  ni  kama hiyo nyumba/kiwanja kimewekwa  kama dhamana kwa ajili ya  vitu kama mkopo . Wakati  mwingine  yawezekana mtu kukuuzia eneo ambalo  limewekwa  dhamana  kwa mkopo wa hela nyingi tu. Na kisheria kama eneo limewekwa dhamana yule anayelimiliki  kwa dhamana  ndiye mwenye nalo kwa muda huo  na wewe uliyenunua  sheria iko wazi unakuwa umeliwa.  

Ieleweke kuwa ni vigumu sana kujua kama  eneo unalouziwa limewekwa  dhamana au hapana  ikiwa hukufanya  upelelezi huu. Wakati mwingine  mtu huweka dhamana eneo lake  na  kubaki na hati . Kwa hati ile  wewe mnunuzi  ni rahisi kuhadaika  kuwa eneo ni lake  lakini kumbe ni eneo lenye  deni kubwa. Ukinunua eneo kama hilo utakuwa umenunua mgogoro  mkubwa ambao  wewe mnunuzi kushindwa na kunyanganywa ulichonunua  ni lazima tu.

KUJUA    KAMA   KUNA   MGOGORO   WA  KIFAMILIA.

Kitu kingine ambacho utaomba kujua  katika yale  maombi  ni kama  kuna mgogoro  wowote  wa  kifamilia  kama migogoro ya mirathi, migogoro  ya kindoa ambapo mwanandoa mmoja anaweza kuwa ameweka  zuio  kuhusu uuzwaji wowote wa nyumba/kiwanja hicho. Usipofanya upelelezi huu utanunua halafu siku ya kubadilisha jina ndio siku utajua kuwa eneo lile lilikuwa haliruhusiwi kuuzwa.

Aidha ifahamike kuwa mamlaka za ardhi hupata taarifa hizi za viwanja vya watu kupitia utaratibu wa mazuio uitwao CAVEAT.

MWANDISHI   WA   MAKALA  HAYA   NI   MWANASHERIA  NA  MSHAURI   WA  SHERIA  KUPITIA  GAZETI  LA  SERIKALI   LA   HABARI   LEO  KILA  JUMANNE  , GAZETI  JAMHURI   KILA  JUMANNE  NA  GAZETI  NIPASHE  KILA  JUMATANO.    0784482959,        0714047241              bashiryakub@ymail.com
author

This post was written by: Author Name

Your description comes here!

Get Free Email Updates to your Inbox!

Post a Comment

CodeNirvana
Chediel . Powered by Blogger.
© Copyright Rundugai Blog
Back To Top