Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohammed Shein na mgombea urais wa Zanzibar
kwa tiketi ya Chama cha Wananchi (CUF) ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa
Rais, Maalim Seif Sharif Hamad.
..............................
NA RAHMA SULEIMAN
24th November 2015
24th November 2015
Mazungumzo ya kutafuta muafaka wa mgogoro wa Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar, yataendelea kufanyika leo Ikulu Mjini Zanzibar.
Mazungumzo ya kikao hicho ambacho ni cha tatu, kitaongozwa na Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohammed Shein.
Wajumbe wa kikao hicho ni Marais wastaafu wa Zanzibar, Dk. Salmin
Amour, Amani Abeid Karume, mgombea urais wa Zanzibar kwa tiketi ya Chama
cha Wananchi (CUF) ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais, Maalim Seif
Sharif Hamad na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi.
Mazungumzo hayo yanasubiriwa kwa hamu kubwa na wananchi baada ya Tume
ya Uchaguzi Zanzibar (Zec), kufuta matokeoi ya Uchaguzi Mkuu visiwani
humu Oktoba 28, mwaka huuu na kuibua mgogoro mkubwa wa Kikatiba.
Naibu Katibu Mkuu wa CUF Nassor Ahmed Mazrui, alisema kuwa hadi sasa
mazungumzo hayo bado siri kubwa hata viongozi wa ndani ya chama chake,
hawafahamu kinachoendelea tangu viongozi hao wa kitaifa kuanza kukutana.
“Hadi sasa usiri umetawala, sielewi chochote kinachoendelea kama
kurejewa kwa uchaguzi au Zec kuendelea kutangaza matokeo, lakini
ninachofahamu kuwa kesho (leo), viongozi wakuu watakutana tena kwa mara
ya nne Ikulu,” alisema Mazrui ambaye pia ni Waziri wa Biashara, Viwanda
na Masoko Serikali ya Umoja wa Kitaifa Visiwani humu.
Alisema inasikitisha mno vikao vyote vitatu vilivyofanyika pamoja na
hicho kinachotarajiwa kufanyika leo, upande mmoja unawakilishwa na watu
watano wakati upande mwingine ukiwa na uwakilishi wa Maalim Seif peke
yake.
Alisema mashariti yaliyowekwa katika muongozo wa mazungumzo, ni
magumu kwa kuwa hakuna mtu mwingine anayeruhusiwa kushiriki katika
mazungumzo ya kutafuta muafaka wa uchaguzi wa Zanzibar zaidi ya Maalim
Seif pekee.
Hali kadhalika, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa
Zanzibar, Mohamed Aboud, alithibitisha kufanyika kwa kikao hicho, lakini
alisema hafahamu kinachoendelea pamoja na bosi wake kuwa mshiriki wa
mazungumzo hayo.
“Yawezekana wewe ndugu mwandishi unafahamu zaidi, lakini na mimi pia
nimesikia kuwa viongozi wetu watakutana, bahati mbaya sifahamu
kinachoendelea,” alisema Waziri Aboud.
Maamuzi ya kufutwa kwa matokeo ya Uchaguzi Mkuu Zanzibar,
yamesababisha Baraza la Wawakilishi kukosa uwakilishi wa wananchi
kinyume na Kifungu cha 90(1) cha Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984.
Kwa mujibu wa kifungu hicho, Baraza la Wawakilishi linatakiwa
kuitishwa mkutano wake wa kwanza tangu kuvunjwa Agosti 13, mwaka huu
ndani ya siku 90.
Spika wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar, Pandu Ameir Kificho, alisema
ataendelea kushika wadhifa huo pamoja na Naibu wake bila ya kuwa na
wajumbe katika chombo hicho cha kutunga sheria Zanzibar.
Mjadala mkubwa umekuwa ukiendelea katika Manispaa ya Mji wa Zanzibar
kuhusu tarehe ya kurudiwa kwa uchaguzi huku CUF wakiendelea kupinga
lakini CCM wanaunga mkono uamuzi wa Zec.
CHANZO: NIPASHE
Post a Comment