Kuna
taarifa kuwa hofu kubwa imetanda juu ya hatma ya vigogo wa taasisi za
umma takriban 18 zilizotajwa na Rais Dk. John Magufuli, kuwa
zinalalamikiwa zaidi na wananchi kwa rushwa, ubadhirifu na utoaji wa
huduma duni.
Vyanzo mbalimbali vimeiambia Nipashe kuwa hivi sasa, ikiwa ni siku
chache tu baada ya Rais Dk. Magufuli kuhutubia Bunge la 11 wakati
akilizindua Ijumaa iliyopita, tayari wakuu kadhaa wa taasisi hizo
wameingiwa na hofu kwa kutojua hatma yao.
Wakati akilihutubia Bunge, Rais Dk. Magufuli alizitaja baadhi ya
taasisi za umma alizosema zinalalamikiwa zaidi na wananchi kutokana na
kasoro mbalimbali za kiutendaji, na kwamba serikali yake imejipanga
kuhakikisha kuwa inazishughulikia mara moja.
Dk. Magufuli alizitaja taasisi hizo kuwa ni pamoja na Bandari, Jeshi la Polisi na Mahakama.
Kadhalika, aliizungumzia kero ya rushwa ambayo hushughulikiwa na
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), ubadhirifu katika
Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) na pia malalamiko kwenye
eneo la ardhi ambalo ni kinara wa chanzo cha migogoro kwa wananchi.
“Wakuu hivi sasa hawana amani tena… wengi hawajui kuhusu hatma yao
baada ya Rais Magufuli kusema wazi kuwa kuna matatizo makubwa katika
utendaji wa taasisi yetu,” chanzo kimoja kiliiambia Nipashe kwa sharti
la kutotajwa jina.
Kadhalika, ofisa mmoja wa cheo cha juu katika halmashauri ya
wilaya, aliiambia Nipashe kuwa kauli ya Dk. Magufuli kuhusiana na
dhamira yake ya kumaliza kero za wananchi wanazokumbana nazo kuhusiana
na ardhi zimeibua hofu kubwa kwa maofisa wa ardhi kwenye wilaya yao
(jina tunalihifadhi).
“Kwa kweli kila mmoja miongoni mwa hawa wakubwa wetu ameingiwa
hofu… wengi wamekuwa wakifanya kazi kwa mazoea na kujiingizia fedha
nyingi kupitia rushwa na pia kujimilikisha maeneo kinyume cha sheria.
Magufuli anatishia hatma yao,” chanzo kingine kiliongeza.
ALICHOSEMA MAGUFULI
Katika hotuba yake, Magufuli alisema kuna maeneo yaliyolalamikiwa
sana na wananchi wakati wa kampeni kabla ya kufanyika kwa Uchaguzi Mkuu
Oktoba 25 ambao alishinda kwa asilimia 58.46 ya kura halali zilizopigwa
na kuingia Ikulu.
Alizitaja baadhi ya kero na taasisi husika kuwa ni tatizo la
rushwa. Alisema tatizo hilo limelalamikiwa na wananchi karibu katika
maeneo yote yanayogusa wananchi.
Magufuli aliitaja pia Tamisemi, akisema ina matatizo ya upotevu wa
mapato, kushindwa kukusanya kodi, ubadhirifu, matumizi mabaya ya fedha
na utekelezaji wa baadhi ya miradi chini ya viwango, wizi na uzembe.
Katika eneo la ardhi, Magufuli alitaja kero zake kwa wananchi kuwa
ni migogoro ya wakulima na wafugaji, viwanja, kuhodhi maeneo bila
kuyaendeleza, mipango miji na kujenga maeneo ya wazi.
Kero katika Bandari ni rushwa, wizi, ubadhirifu na urasimu; kero za
Maliasili na Utalii ni kuwapo kwa ujangili ambao yaonekana wazi kuwa ni
lazima idara husika inashiriki, migogoro ya mipaka kati ya vijiji na
hifadhi na upotevu wa mapato.
Eneo lingine lenye kero zinazolalamikiwa na wananchi kwa mujibu wa
Dk. Magufuli ni katika huduma za afya, akisema kuwa kuna ukosefu wa
dawa, hujuma kwenye vifaa vya vipimo, msongamano wa wagonjwa na tozo
zisizostahili, lugha mbaya za watumishi kwa wagonjwa, uhaba wa majengo,
vitendea kazi, rasilimali watu na fedha, kushindwa kukusanya mapato
yanayowahusu n.k.
Uhamiaji ni eneo mojawapo ambalo Rais Magufuli alilitaja kuwa ni
kero kubwa kwa wananchi kwa kueleza kuwa kuna wageni wengi kutoka nje
ambao wapo nchini wanafanya kazi ambazo hata mzawa angezifanya.
Aligusia suala la kutoa ovyo hati za uraia kwa wageni pasipo
kuzingatia sheria na taratibu, utoaji wa vibali vya kuishi kwa wageni na
mambo mengineyo ambayo yalikuwa yanafanywa.
Kadhalika, Rais Magufuli wakati akihutubia Bunge, pia alielezea
suala la elimu ataipa kipaumbele zaidi kwa kutekeleza sera yake ya elimu
bure kuanzia shule ya msingi hadi sekondari itakayoanza kutolewa
mwakani.
Alieleza kuwa utoaji wa elimu bure ambayo haitakuwa na michango yoyote kwa wanafunzi.
“Ninaposema elimu bure, ninamaanisha elimu bure kweli kweli,
sitasikia masuala ya michango, tena walimu watakaotoza michango ya ajabu
ajabu watakiona,” alieleza Rais Magufuli.
Pia Rais Magufuli alielezea kuboresha vifaa vya kujifunzia,
kutatua matatizo ya walimu, kuboresha mazingira ya kusomea ikiwa ni
pamoja na majengo, Madawati, Ukosefu wa nyumba za walimu, n.k.
Polisi ni sehemu mojawapo ambayo Rais Magufuli aliielezea kwa
mapana zaidi kwa kueleza uovu waliokuwa wanautenda jeshi la polisi kwa
kuwabambikizia kesi raia wasiokuwa na hatia.
Pia aliezea kuboresha madai ya askari, ukosefu wa nyumba za askari, ukosefu wa vitendea kazi vya kisasa.
Vile vile Rais Mgufuli aligusia utendaji wa kikosi cha zimamoto kwa
kuchelewa kufika kwenye matukio, kufika kwenye matukio bila vitendea
kazi kama maji, huku akihaidi kulishughulikia suala hilo hivi karibuni.
Pia Rais Magufuli pia alizungumzia wafanyakazi wanaofanya kazi
katika Mizani kwa kuwaelezea uzembe wanaoufanya ukiwamo wa
kucheleweshwa kwa magari yanayosafiri.
Vilevile katika hotuba yake, alizungumzia Mahakama kwa kusema
anatambua jitihada zake katika kushughulikia mrundikano wa kesi na
kuahidi kulishughulikia suala hilo kwa haraka zaidi ikiwamo malalamiko
mengi juu ya ucheleweshaji wa kesi.
Eneo lingine ni madini akisema taifa kutokufaidika na rasilimali hiyo huku wageni wakifaidika kwa kiwango kikubwa.
Masuala ya vilio vya wachimbaji wadogo wadogo kutengewa maeneo ya
uchimbaji na kupatiwa mikopo, kutolipa kodi stahiki, usumbufu kulipa
fidia, pia alielezea kuanza nayo kwa haraka.
Aidha, Rais Magufuli alizungumzia Idara ya Kilimo na Mifugo kwa
kusema uhaba wa pembejeo za mifugo na kilimo, tatizo la masoko, kukopwa
mazao ya wakulima, ukosefu wa wataalam wa ugani, upungufu wa maghala,
mabwawa, malambo, majosho, n.k.
Katika hotuba hiyo, Pia Rais Magufuli alielezea sekta ya uvuvi kwa
kutaja changamoto zinazowakabili wavuvi ikiwamo vifaa duni na masoko,
uvuvi haramu, uwekezaji mdogo katika sekta ya uvuvi hususan viwanda vya
mazao ya uvuvi hasa katika ukanda wetu wa bahari.
Suala la reli, Rais Magufuli alieleza kuwa reli ya kati inahitaji
kufanyiwa maboresho zaidi kwa kujenga reli nyingine ya Standard Guarge
kutoka mkoani Dar es Salaam hadi Kigoma.
Alieleza kuwa uchakavu wa miundombinu ya nchi, kutokuwapo kwa
usafiri wa uhakika wa reli, upungufu wa bandari kavu, mizigo mingi
kusafirishwa kwa barabara ni mojawapo ya matatizo yaliyomo katika sekta
ya reli na yanahitaji kufanyiwa marekebisho ya haraka.
Rais Magufuli alizungumzia Shirika la Ndege la Taifa (ATCL) kwa
kueleza kuwa shirika hilo linawafanya kazi zaidi ya 200 wanaolipwa
mishahara, lakini wana ndege moja tu.
Rais Magufuli pia alielezea makundi maalum kama wazee, walemavu, wanawake na watoto wanavyonyimwa haki zao.
Vilevile Rais Magufuli aligusia kundi la wafanyakazi kama vile
wanamichezo kwa kuelezea matatizo yao ikiwamo makato ya kodi kwa
wafanyakazi yakiwa makubwa.
“Kero hizi tutazishughulikia kwa nguvu zetu zote. Wizara, ofisi na
taasisi husika zijipange ipasavyo kutatua kero hizi. Nimetaja baadhi ya
kero hizi ili nanyi Waheshimiwa Wabunge mzitambue na mshirikiane na
serikali na wadau wengine tuzitatue haraka,” alieleza Rais Magufuli.
MAONI YA WACHAMBUZI
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Iringa (UoI), Essau Ntabindi, alisema
Rais Magufuli aliongea mambo ambayo aliyapata kutoka kwa wananchi
wakati akifanya kampeni za urais hivyo vilikuwa ni vitu vyenye uhalisia.
Aliema Rais Magufuli alichokisema ni sahihi na wala siyo kupoteza
morali kwa maofisa aliowagusa kwa kuzitaja idara zao akiwa Bungeni.
Kadhalika, alisema Rais Magufuli alikuwa anawakumbusha maofisa hao
na watendaji wengine wa serikali wafanye kazi na siyo kupiga porojo
ambazo hazina faida katika kuinua uchumi wa nchi.
“Rais Magufuli alichokuwa anakisema pale Bungeni alikuwa sahihi na
alikuwa anawakumbusha viongozi waliopo ofisini waendane na kauli mbiu
yake ya hapa kazi tu,” anasema Ntabindi.
Naye Mhadhiri kutoka Chuo Kikuu Huria (Out) Idara ya Siasa na
Utawala, Hamad Salim, anasema Rais Magufuli ni jukumu lake kuongelea
masuala yanayogusa taifa, na Bungeni ni sehemu mojawapo ya kuongea
masuala hayo.
Alisema kuzitaja taasisi hizo siyo kwamba alikuwa anaziumbua au
kuziaibisha, bali alikuwa anawaeleza ukweli Watanzania wafahamu uozo
uliokuwa unafanywa na baadhi ya viongozi.
Alisema hotuba yake ilikuwa inazungumzia mwelekeo wa serikali yake
itakavyofanya kazi kwa miaka mitano ijayo, hivyo ilikuwa ni lazima ataje
mikakati yake.
“Rais Magufuli hakutaka kutumia lugha ya falsafa ambayo ingewafanya
Watanzania wasimuelewe anazungumza nini na atafanya nini, aliamua
kutumia lugha nyepesi ili kila mtu amuelewe,” alisema Salim.
Alisema Rais Magufuli alikuwa anawakumbusha viongozi atakaowateua
kuwa watende kazi kwa mujibu wa sheria na kanuni na siyo kwa mazoea kama
walivyokuwa wanafanya kwa viongozi wakubwa waliokwisha tangulia.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Taasisi ya Utafiti na Kuondoa
Umaskini (Repoa), Profesa Samwel Wangwe, alisema Rais Magufuli alikuwa
anazikumbusha taasisi hizo zifanye kazi sawasawa na kuwaonyesha
Watanzania namna viongozi waliotangulia walivyokuwa wanafuja mali.
Alisema Jeshi la Polisi na Wizara ya Maji ni idara zinazofahamika kuwa zina changamoto kubwa katika utendaji wa kazi.
CHANZO:
NIPASHE
Post a Comment