Makamu
wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan,
akizungumza na Uongozi wa Mtandao wa Wanawake Tanzania (WFT) wakati
viongozi hao walipofika Ofisini kwake Ikulu jijini Dar es Salaam,leo Nov
24, 2015 kwa mazungumzo.
Makamu
wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan,
akipokea baadhi ya Vipeperushi na Vitabu vya Mtandano wa Wanawake
Tanzania (WFT) kutoka kwa mwenyekiti wa mtandao huo, Prof.Ruth Meena,
baada ya mazungumzo yao yaliyofanyika Ofisini kwa Makamu Ikulu jijini
Dares Salaam, leo Nov 24, 2015.
Makamu wa
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan, akiwa
katika picha ya pamoja na Viongozi wa Mtandao wa Wanawake Tanzania
(WFT) baada ya mazungumzo yao yao yaliyofanyika Ofisini kwa Makamu Ikulu
jijini Dares Salaam, leo Nov 24, 2015.
Picha na OMR
JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
OFISI YA MAKAMU WA RAIS.
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Makamu
wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan leo
amekutana na uongozi wa Mtandao wa Wanawake na Katiba Tanzania (WFT)
ambapo amezungumzia dhamira ya serikali katika kuyatafutia ufumbuzi
matatizo mbali mbali yanayowakabili wanawake na watoto wa kike nchini.
Katika
mazungumzo hayo Makamu wa Rais aliueleza ujumbe huo kuwa wakati wa
kampeni aliahidi pamoja na kazi za kumsaidia Mhe. Rais bado kama mama
atafuatilia kwa karibu utekelezaji wa ahadi ya kupatikana kwa maji safi
na salama, kuboresha afya ya mama na mtoto, elimu na mazingira.
“Nilipokuwa
kwenye kampeni nimejionea shida ya maji na wanawake ndiyo wanaopata
tabu ya kutembea mwendo mrefu kutafuta maji. Kwa hiyo, pamoja na kazi
zangu za kumsaidia Mhe. Rais nitasimamia miradi yote ya maji, alau
tuhakikishe maji yanapatikana umbali wa mita 400 kutoka eneo wananchi
wanakoishi au karibu zaidi”.
Alisema
kinachofurahisha zaidi suala la maji liko kwenye Mpango wa Matokeo
Makubwa Sasa (BRN) na miradi mingi ikiwemo ya kuchimba visima virefu
katika mikoa kama vile ya Singida na Dodoma iko kwenye mchakato na cha
msingi ni kusimamia fedha zinatumika kuleta maji kama ilivyokusudiwa.
Kuhusu
afya ya mama na mtoto alisema kazi hiyo ataianza hivi karibuni kwa
kushirikiana na Mashirika yasiyo ya kiserikali yanayotetea haki za
wanawake ili kupunguza vifo vinavyosababishwa na mimba za utotoni.
“Hili
tutajitahidi kulipunguza kwa kiasi kikubwa na hasa baada ya serikali ya
Awamu ya Nne kusema kwamba shule ya msingi ya lazima ni kutoka darasa la
kwanza hadi kidato cha nne”, alisema na kuongeza
“Katika
kipindi hicho binti atakuwa amefikisha miaka 17, atakuwa tayari
kukabiliana na mambo ya uzazi tofauti na ilivyo sasa ambapo anamaliza
darasa la akiwa mdogo na matokeo yake anapata mimba katika umri mdogo.
Mtusaidie kupiga debe huko nje utekelezaji uweze kufanikiwa.”
Hata
hivyo, alisisitiza kusimamia suala la kuhakikisha zahanati, vituo vya
afya na hospitali nchini zinakuwa na dawa na vifaa tiba vya kutosha
katika wodi za wazazi kwa ajili ya kuhudumia akina mama na wananchi kwa
ujumla ambao wengi wanaonekana ni watiifu kwa serikali yao.
Kwa
upande wa elimu Mhe. Samia alisema atasimamia ujenzi wa mabweni kwa
watoto wa kike na kuhakikisha mazingira yanatunzwa kwa sababu uharibifu
wa mazingira ndiyo umekuwa chanzo cha upungufu wa maji nchini.
Aidha
aliuambia ujumbe huo kuwa hivi sasa tuna mpango wa kuimarisha utendaji
serikalini kuanzia serikali kuu hadi serikali za mitaa ili
kinachopatikana kidogo kimfikie kila mwananchi.
“Tutaendelea
kuaihirisha sherehe ili fedha hizo ziweze kutumika kwa mambo ya
kijamii. Kwa msimamo huu amabao Mhe. Rais ameanza nao labda watu wote
tushirikiane kwa kutatua matatizo yetu kwa gharama nafuu kwa ufanisi
mkubwa.”
Mapema
akizungumza kwa niaba ya wenzake Mwenyekiti wa Mtandao huo Prof Ruth
Meena alimpongeza Mhe. Samia kwa kushika nafasi ya juu ya uongozi akiwa
mwanamke wa kwanza kuweka historia katika Tanzania.
Alimweleza
Mhe. Makamu wa Rais matarajio yao kwa serikali ya Awamu ya Tano kuwa
itatetea misingi ya haki na usawa katika Nyanja zote.
Imetolewa na Ofisi ya Makamu wa Rais
Dar es salaam
24/11/2015.
Post a Comment