KITONGOJI
cha Kitanewa katika
kijiji cha Mapogoro, tarafa ya Idodi wilayani Iringa mkoani Iringa,
jimboni Isimani kwa Waziri wa Ardhi William Lukuvi kimeendelea
kuathiriwa na mafuriko na kuwa katika hatari ya kutoweka baada ya
kuzingirwa na maji ya
mto Mapogoro yaliyobadili mkondo wake.
Katika mazingira ya kushangaza
baadhi ya kaya 83 zinazoishi kitongojini hapo zimekataa kuhama katika eneo hilo
mbele ya Mkuu wa Wilaya ya Iringa, Richard Kasesela aliyefika katika eneo hilo
juzi kujionea hali halisi zikidai kwamba zitafanya kila ziwezalo kudhibiti
mafuriko hayo.
Akiwa na baadhi ya wanahabari,
Kasesela na msafara wake walilalazimika kuvua viatu kabla kuvushwa kwa msaada
wa askari Polisi na wananchi wengine hadi katika kitongoji hicho kupitia mkondo
mpya mkubwa wa maji uliozingira kaya hizo.
Baada ya kujionea hali hiyo mkuu wa
wilaya huyo alizimbia kaya hizo kwamba zipo katika hatari ya
kuendelea kuathiriwa na mafuriko hayo ikiwa ni pamoja na kupoteza maisha yao endapo
hazitahama eneo hilo ambalo baadhi ya nyumba zake zimebomoka kutokana na mvua
zinazoendelea kunyesha, huku ardhi yake ikiendelea kumegwa na mkondo wa maji ya
mto Mapogoro yaliyochepuka.
“Hali hii ni hatari sana na kwa kweli
tunahitaji nguvu ya ziada ya kuzuia maafa haya, nyumba zinaendelea kubomoka,
mashamba yanaharibiwa na hata miundombinu mingine kama nguzo za umeme ipo
hatarini kung’olewa,” Kasesela alisema huku akiwasihi wananchi hao kuhamia
katika eneo lililotengwa.
Alisema kwa upande wake serikali itafanya
kila iwezelo kutekeleza jukumu lake la msingi la kuwapatia makazi ya muda
wananchi hao na kushirikiana na wadau wengine kuhakikisha wanapata mahitaji
mengine ya msingi.
Afisa Tarafa ya
Idodi, Ayubu Kiwanga alisema wananchi hao wanatakiwa kuhamia kwenye eneo
maalumu lililotengwa katika kijiji cha Mapogoro ambako pia watapewa maeneo ya
kujenga makazi yao ya kudumu.
Post a Comment