Rais Dk. John Magufuli.
Kauli hiyo ilitolewa jijini Dar es Salaam jana na Kaimu Mkurugenzi
Mtendaji wa hospitali hiyo, Prof. Lawrance Museru, alipokuwa akielezea
mafanikio ya hospitali hiyo katika siku 100 za Rais Magufuli hospitalini
hapo, tangu aingie madarakani.
Prof. Museru alisema utekelezaji wa agizo hilo umekuwa mgumu
kutokana na wingi wa wagonjwa wanaofika kupata huduma, wakati hospitali
hiyo inakabiliwa na ukosefu wa wodi za kulaza wagonjwa.
Rais Magufuli alifanya ziara ya ghafla hospitalini hapo Novemba 9,
mwaka jana, na kukutana na changamoto kadhaa na kuagiza zitatuliwe.
Miongoni mwa changamoto hizo ni kuharibika kwa mashine za MRI na CT
Scan na wagonjwa kulala chini kwa kukosa vitanda na ukosefu wa dawa.
Akiwa mjini Dodoma wakati akizindua Bunge la 11, Rais Magufuli
aliagiza kati ya Sh. milioni 225 zilizochangwa na wadau mbalimbali kwa
ajili ya sherehe ya wabunge, zisitumike zaidi ya Sh. milioni 15 na
zilizobaki zielekezwe katika ununuzi wa vitanda, magodoro na mashuka kwa
ajili ya hospitali ya Muhimbili.
Prof. Museru alisema hawezi kuruhusu kukataa kupokea wagonjwa
kutokana na ukosefu wa vitanda na kwamba wataendelea kuwapokea na
kuwapatia huduma stahiki hadi hapo watakapopata nafasi ya kuweka
vitanda.
“Tumejipanga kuhakikisha wagonjwa wanapata huduma bora lakini
suala la wagonjwa kulala chini ni gumu na haliepukiki kwa sababu
hatuwezi kuwaacha wagonjwa kwa kukosa nafasi ya vitanda,” alisema.
Alisema vitanda 300 vilivyonunuliwa kwa agizo la Rais kutoka fedha
zilizotakiwa kutumika kwenye sherehe ya uzinduzi wa Bunge, vimepelekwa
kwenye jengo jipya la Taasisi ya Mifupa Muhimbili (Moi).
Pia alisema MOI imeanza kuhama katika majengo ya Muhimbili wodi namba 2 la Mwaisela na wodi 17 na 18 za Sewahaji.
“Kuhama kwao kumesaidia kutoa nafasi ya kulaza wagonjwa 120,” alisema.
Aidha, alisema katika kipindi cha miezi miwili wamefanikiwa
kuongeza mapato ya hospitali kutoka Sh. bilioni 2.7 hadi Sh. bilioni
4.3.
“Tumeongeza mapato zaidi ya asilimia 60 baada ya kuongeza kasi ya
usimamizi wa wafanyakazi na kupunguza kero zilizokuwa zinawakabili,”
alisema Prof. Museru
Alisema uzalishaji umeongezeka kwa mwezi Desemba na kufikia Sh.
bilioni 3.3 kutoka wastani wa Sh. bilioni 2.7 zilizokuwa zikizalishwa
kwa miezi mitano kutoka Julai hadi Novemba, mwaka jana.
Mkurugenzi huyo alisema mafanikio hayo yanatokana na juhudi ya
uongozi kutatua kero za wafanyakazi ikiwamo kulipa malimbikizo ya madeni
ya likizo na malipo mengine stahiki kiasi cha Sh. milioni 600.
Alisema kwa sasa morali ya ufanyaji kazi imeongezeka kama
inavyothibitishwa na kuongezeka kwa huduma za kliniki za muda wa ziada.
MAGUFULI ASHTUKIZA MUHIMBILI
Katika hatua nyingine Rais John Magufuli alifanya ziara ya ghafla
katika wodi ya wazazi Muhimbili baada ya kundi la kinamama waliolazwa
katika wodi hiyo kumzuia.
Kinamama walimtaka Rais Magufuli kuwatatulia kero wanazozipata ikiwamo kulala chini na msongamano mkubwa katika wodi hiyo.
“Nimejionea mwenyewe watu wanapata shida, nimejifunza na mimi
mwenyewe nitajua namna ya kulishughulikia msiwe na wasiwasi,” alisema
Rais Magufuli.
Rais Magufuli alizuiwa na kinamama hao baada ya kutoka kumjulia
hali Mufti wa Tanzani, Sheikh Mkuu Abubakary Zubery bin Ali , aliyelazwa
hospitalini hapo.
Imeandaliwa na Moshi Lusonzo, Romana Mallya na Christina Mwakangale.
CHANZO:
NIPASHE
Post a Comment