Katibu Mtendaji wa Necta, Dk, Charles Msonde.
Baraza la Taifa la Mitihani (Necta), limeagiza
kusitishwa kwa ugawaji wa vyeti vya kidato cha sita kwa wanafunzi
waliohitimu mwaka 2015, huku vile vilivyokwisha gawanywa kwa watahiniwa
hao vikitakiwa kurejeshwa kwenye chombo hicho.
Hali hiyo imeibua utata mkubwa, huku baadhi ya wadau wakiwamo
maofisa elimu, wakihisi hatua hiyo ya Necta huenda inalenga kuvibadili
vyeti hivyo kutoka kwenye mfumo wa wastani wa alama (GPA), kwenda kwenye
ule wa jumla (division).
Hata hivyo, Katibu Mtendaji wa Necta, Dk, Charles Msonde,
alipoulizwa na Nipashe jana alikanusha vikali madai hayo, akisema vyeti
hivyo havitabadilishwa kutoka kwenye mfumo wake bali vimesitishwa
kugawanywa ili baraza lijiridhishe na baadhi ya vitu.
MAOFISA ELIMU, WAKUU WA SHULE
Ofisa Elimu Mkoa wa Dodoma, Juma Kaponda, alipoulizwa na Nipashe
jana kama amepokea agizo hilo, alithibitisha kuwa shule zote za mkoa huo
zenye kidato cha tano na sita zimepewa taarifa ya kutakiwa kurudisha
vyeti hivyo Necta.
Alisema sababu ya kuvirudisha vyeti hivyo anadhani ni kufanya mabadiliko kutoka GPA na kurudi kwenye divisheni.
Ofisa Elimu Mkoa wa Arusha, Nestory Mloka, alisema amepata barua ya
maelekezo hayo kutoka Necta ikimuelekeza kuwataka maofisa elimu wilaya
wawasiliane na wakuu wa shule za kidato cha tano na sita wasigawe vyeti
vya wanafunzi waliohitimu mwaka 2015.
Mkuu wa Shule ya Sekondari ya St. Matthew iliyoko Kongowe, Mkuranga
mkoani Pwani, Abraham Shafuri, naye alikiri kuwapo kwa agizo la Necta
la kusimamisha utoaji wa vyeti hivyo kwa wahusika.
Alisema aliambiwa na maofisa wa Necta kuwa vyeti hivyo vinatakiwa
kurejeshwa kwenye baraza hilo na kwamba sababu zilizotolewa ni kuwa
kuna marekebisho kidogo yanabapaswa kufanyika.
“Nilichoambiwa ni kwamba shule karibu zote za Dar es Salaam
zimesharejesha vyeti hivyo na kwamba kwa sisi wa mkoa wa Pwani, maofisa
hao watapita kuvichukua lakini hatujui ni lini watakuja,” alisema
Shafuri.
Katika Manispaa ya Moshi, mmoja wa wakuu wa shule za sekondari
ambaye hakutaka kutajwa jina lake, aliithibitishia Nipashe kwamba
wameagizwa na serikali kuvirejesha vyeti hivyo, ikielezwa kwamba
vinahitaji kufanyiwa maboresho.
"Ni kweli tumeagizwa hilo na kesho (leo) asubuhi naletewa barua,
kwa hiyo nafikiri nitakuwa katika nafasi nzuri ya kulizungumzia baada ya
kuiona rasmi," alisema mkuu huyo wa shule.
Mmiliki mmoja wa shule ya sekondari na chuo cha ualimu binafsi,
ambaye aliomba hifadhi ya jina lake, alisema ni kweli wamepata taarifa
ya kutotoa vyeti hivyo na kama wamevitoa kuhakikisha vinarejeshwa.
Hata hivyo, alisema kwa taarifa alizosikia ambazo si rasmi ni
kwamba vinatakiwa kubadilishwa kutoka GPA na kuwa kwenye mfumo wa
Divisheni.
"Lakini serikali inatakiwa kujua kwamba ikifanya hivyo, hilo ni
kosa la jinai, kwani hata walivyofanya kwa matokeo ya kidato cha nne
kutoka kwa mfumo wa divisheni badala ya GPA, ni kosa la jinai pia kwa
kuwa wanafunzi hawakujiandaa kwa mfumo huo," alisema huku akiomba
hifadhi ya jina lake na kuongeza:
"Unajua huu ni usumbufu mkubwa, kwani kuna wanafunzi wengine wapo
Urusi na kwingineko nje ya nchi wanasoma na huko waliomba kozi zao kwa
kutumia 'transcript' ambazo zinaonyesha mfumo wa GPA, sasa baadaye
wakipeleka vya Divisheni si wataonekana wanadanganya. Huu ni usumbufu
mkubwa hauna maana kwa sasa, ni bora kuacha mfumo uliopita ubaki kama
ulivyo."
Mkuu wa Shule ya Sekondari Aruisha, Christopher Malamsha,
alithibitisha kupokea maagizo ya ofisa elimu wilaya ya Arusha kumweleza
wazuie vyeti kidato cha sita lakini sababu hawajaambiwa.
MZAZI
Kwa upande wake, Audax Rusenene, ambaye ni mzazi wa mwanafunzi
aliyehitimu kidato cha sita mwaka jana kwenye Shule ya Wasichana ya
Feza, alisema uongozi wa shule hiyo umemtaka mwanaye anayesoma Chuo
Kikuu cha Stelenbosch kilicho Afrika Kusini, arejeshi cheti chake.
“Mtoto wangu alienda chuo Januari 17, mwaka huu, lakini nashangaa
hivi karibuni kupigiwa simu na msaidizi wa mkuu wa shule aliposoma
mwanangu na kutaka arudishe cheti,” alisema na kuongeza:
“Nilipomwambia kwamba mtoto yupo chuo Afrika Kusini, akaniambiwa
niwasiliane naye akirudishe kwa sababu hilo ni agizo la serikali.”
“Hiki kitu kinasikitisha kwa sababu kama kuna mabadiliko yatafanywa
kwenye cheti wakati alama alizopata ndizo zilizofanya akapata chuo
unadhani itakuwaje?.”
Alisema mtoto wake huyo alihitimu kidato cha nne mwaka 2012 kwenye
Shule ya St. Francis na kukumbwa na kufutwa kwa matokeo yake na sasa
anatakiwa tena arudishe cheti chake cha kidato cha sita.
NECTA YANENA
Akifafanua jambo hilo, Dk. Msonde alisema: “Baraza halijaagiza
vyeti virudishwe ili vibadilishwe mfumo (GPA), baraza lilichokielekeza
ni utaratibu wa kawaida wa baraza la mitihani kuangalia uhalali wa vyeti
vyake, serial namba ya vyeti vyake na kujiridhisha kama vyeti hivyo
vimetawanyika sawasawa.
“Vyeti hivi baraza limevigawa hivi karibuni na lilichofanya sasa
limezuia kwanza shule zisigawe mpaka litakapotoa maelekezo mengine,
msingi huo wa kuzuia uko kwenye hoja ya kuhakikisha tu kwamba
linajiridhisha kwenye takwimu zake kama zimekaa sawasawa katika vyeti
vilivyokwenda kila shule.”
“Baadhi ya vyeti kwenye mkoa wa Dar es Salaam vipo Necta, lakini kwenye mikoa mingine yote viko shuleni,” alisema Dk Msonde.
Aliongeza kuwa, “Kama mkuu wa shule alikuwa amegawa vyeti viwili,
vitatu kabla havijarejeshwa baraza ni suala jingine, lakini kiujumla
kinachofanywa na baraza hapa ni kuhakiki cheti hiki, kama vimekaa kama
utaratibu wetu ulivyo.”
Alisema suala la kubadilisha kutoka kwenye GPA kwenda kwenye
divisheni halipo na kwamba matokeo yaliyotangazwa kwa utaratibu wa GPA
vyeti vyake vitaendelea kuwa katika mfumo wa GPA na matokeo
yaliyotangazwa kwenye utaratibu wa divisheni vyeti vyake vitabaki kuwa
kwenye divisheni.
Alisema kwa wale ambao tayari wako nje ya nchi, hakuna
atakayeathirika na kama baraza likihitaji cheti chake litafanya
utaratibu wa kukipata.
Habari hii imeandaliwa na Fredy Azzah, Dar, Agusta Njoji, Dodoma, Godfrey Mushi, Moshi, John Ngunge, Arusha.
CHANZO:
NIPASHE
Post a Comment