Katibu Mkuu mpya wa Chadema, Dk. Vincent Mashinji.
Mwishoni mwa wiki, Chadema ilimteua Dk. Mashinji kuwa Katibu Mkuu
mpya kushika nafasi ya Dk. Wilbroad Slaa aliyejiuzulu nafasi hiyo Julai
30, mwaka jana kwa kile akichodai kuwa ni utaratibu kutofuatwa wa
kumkaribisha Edward Lowassa, aliyehamia katika chama hicho kutoka Chama
Cha Mapinduzi (CCM) na kisha kuteuliwa kuwa mgombea urais kupitia chama
hicho akiungwa mkono na vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi
(Ukawa).
Hata hivyo, wakati wengi wakihoji uwezo wake, imefahamika kuwa Dk.
Mashinji kwa kushirikiana na kamati yake, ndiyo waliobuni kaulimbiu
(slogan), ya `Lowassa Mabadiliko, Mabadiliko Lowassa,' ambayo ilitumika
katika kampeni za uchaguzi mkuu mwaka jana na kuwa kivutio kikubwa.
Akihutubia mamia ya wananchi wa Jiji la Mwanza katika viwanja vya
Furahisha, Katibu Mkuu huyo, alisema: "Katika mkakati wetu kama kamati
ya wataalam, tulileta kauli ya Mabadiliko Lowassa, Lowassa Mabadiliko,
wameiiga, lakini hawawezi kuwa kama sisi, tunamaanisha mabadiliko
tunayoyazungumzia na tutayatekeleza kimkakati na kimfumo zaidi."
Mbali na hilo, kati hiyo ya ndiyo iliyofanikisha maafikiano tisa
ya Ukawa pamoja na suala zima la chama kipi kipewe nafasi ya kusimamisha
umeya katika umoja huo.
Kauli hiyo ambayo hadi sasa inatumika kwenye vikao vya ndani, nje
na mikutano ya hadhara vya Chadema, alishirikiana na Kamati ya Wataalam
ya Ukawa ambayo imekuwa ikibuni na kushauri mambo mbalimbali ya
uendeshaji wa umoja huo.
Katika umoja huo unaohusisha vyama vya Chadema, NCCR-Mageuzi, CUF
na NLD, kamati ya wataalam iliongozwa na aliyekuwa Katibu Mkuu na Makamu
wa Rais wa Chama cha Madaktari Tanzania, Dk. Rodrick Kabangila na
Makamu akiwa Dk. Mashinji na Katibu alitoka CUF.
AELEZA SAFARI YAKE NA DK. MASHINJI
Dk. Kabangila, alisema alikutana na Dk. Mashinji Chuo Kikuu cha
Makerere, nchini Uganda, akiwa mwaka wa tatu naye wa pili,
wakishirikiana kwenye uongozi wa Umoja wa Wanafunzi wa Tanzania
wanaosoma chuoni humo.
Baada ya kurudi nchini walikutana tena Muhimbili na kuendelea
kushirikiana ikiwamo kuandika majarida mbalimbali ambayo walimpelekea
Mbowe kwa ajili ya utekelezaji.
Anasema mwaka 2011, baada ya kujiondoa katika Chama cha Madaktari
nchini, baada ya kuona mgongano mkubwa na kutoeleweka katika
wanayoyapigania, aliingia kwenye siasa na kwa pamoja waliwekwa kwenye
Kamati ya Afya ya Chadema, yeye akiwa mwenyekiti na Mashinji akiwa
makamu mwenyekiti.
Alisema baada ya kufanya vizuri kwenye kamati hiyo, walipewa Kamati
ya Maandalizi ya Ilani ya Chadema, nako alikuwa mwenyekiti na mwenzake
makamu.
AMFAGILIA DK. MASHINJI
Alisema Dk. Mashinji ni mtu sahihi kwa Chadema kwani ni makini,
mwandishi mzuri, anasoma kwa makini machapisho mbalimbali, amesimamia
miradi mikubwa ya mabilioni ya fedha na ilileta matokeo chanya, anaijua
neno kwa neno katiba na ilani ambayo alishiriki kuiandika na anajua
inavyoweza kutekelezwa na miongozo mingi wameiandaa pamoja.
AMPONDA DK. KIGWANGALLA
Dk. Kabangila, alimshangaa Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii,
Jinsia na Watoto, Dk. Hamis Kingwangala, ambaye amendika kwenye ukurasa
wake wa Facebook akimponda Dk. Mashinji, na kwamba wakati wa mgomo wa
mwaka 2005 alikuwa ni mwanafunzi aliye katika mafunzo ya vitendo
(internship) na kwamba mgomo huo uligawanyika katika maeneo matatu ya
wanafunzi wanaofaya mafunzo kwa vitendo, daraja la kati na wakongwe, na
kwamba Dk. Mashinji alikuwa katika daraja la juu na alisimamia masuala
ya ngazi hiyo.
Alisema katika mgomo wa mwaka 2011, walikuwa na Dk. Kigwangalla,
yeye (Kabangila) akiwa ni Katibu Mkuu wa Chama Cha Madaktari Tanzania na
Makamu wa Rais, na walishirikiana wote na Dk. Mashinji kwa kuwa ni
miongoni mwa watu waliokuwa na misimamo thabiti, mtendaji makini na
mfuatiaji wa mambo.
"Namshangaa sana Dk. Kingwangalla, sijui ni siasa inamlevya au
baada ya kuwa waziri anasahau kabisa jinsi walivyopambana kuboresha
sekta ya afya na maslahi ya madaktari nchini, unapokuwa mtaalam unapaswa
kupinga kitaalam na siyo kusema mambo kirahisi rahisi na pasipokuwa na
taarifa kamili, kwa sasa inaonekana amesahau kabisa udugu wa kitaaluma
tuliofundishwa na tunapaswa kuuhubiri. Ukweli anaujua ila anajilazimisha
kutoujua," alisema.
SOURCE:
NIPASHE
Post a Comment