Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
SIRI imefichuka kuhusu hatua ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa Serikali
ya Umoja wa Kitaifa ya Zanzibar (SUK), Maalim Seif Sharif Hamad, kuishi
hotelini jijini Dar es Salaam.
Maalim Seif ambaye pia ni Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF),
amekuwa akiishi katika Hoteli ya Serena jijini hapa tangu aliporuhusiwa
kutoka Hospitali ya Hindu Mandal Machi 8, mwaka huu alipokuwa amelazwa
kwa matibabu.
Akizungumza na MTANZANIA jijini Dar es Salaam jana, mmoja wa ofisa wa
ngazi za juu wa CUF, alishangazwa na hatua ya baadhi ya watu kuhoji
kiongozi huyo kuendelea kuishi hotelini hapo.
Alisema hatua ya kiongozi huyo kuishi hotelini ni matokeo ya Serikali
ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), kushindwa kutekeleza ahadi ya kumpa nyumba
pindi anapokuwa Dar es Salaam katika shughuli zake.
Alisema kutokana na hali hiyo imekuwa ni utaratibu kwa kiongozi huyo
kufikia katika hoteli hiyo na gharama za kuishi hotelini hapo hulipwa na
SMZ kwa mujibu wa sheria.
“Tangu mwaka 2010 Maalim aliahidiwa atapewa nyumba na Serikali ya SMZ
lakini hilo halijafanyika, hiyo nyumba hajapewa hadi leo ndiyo maana
mara zote akija Dar hufikia hotelini.
“SMZ ndiyo wenye jukumu la kulipa na si vinginevyo, kwani hata kama
kama kuna viongozi wa SMZ wamepewa nyumba kwa muda wote, lakini Maalim
Seif hajapewa, sasa kama unataka kujua kwa undani unaweza kuwauliza
viongozi wa Serikali wao ndiyo wenye majibu zaidi,” alisema ofisa huyo
ambaye hakutaka jina lake liandikwe gazetini.
Gharama zilizotumika kwa siku 7
Kwa mujibu wa chumba anachoishi kiongozi huyo chenye hadhi ya rais
ambacho hutozwa kwa Dola za Marekani 2,801.50, ambapo dola moja ni sawa
na Sh 2,180. Hivyo kwa siku saba hadi kufikia leo Serikali imemlipia
Maalim Seif, Sh milioni 42.946.
Kauli ya CUF
MTANZANIA ilipomtafuta Kaimu Mkurugenzi wa Habari, Uenezi na
Mawasiliano ya Umma wa CUF, Hamad Masoud Hamad, alisema hatua ya Maalim
Seif kuishi hotelini inatokana na maagizo ya daktari wake ambaye
amemtaka apumzike kwa sasa.
Alisema kutokana na hali hiyo baada ya kuruhusiwa kutoka hospitali
alipokuwa akipatiwa matibabu alikwenda katika Hoteli ya Serena
anapofikia kila mara anapokuwa jijini Dar es Salaam.
Alipoulizwa ni nani anayelipa gharama za kuishi hotelini hapo, Hamad
alisema wanaoweza kuzungumzia suala hilo ni viongozi wa SMZ.
“Magufuli (Rais), alipokwenda kumwona alimuuliza ni nani anayemlipia
gharama za hoteli na Maalim alisema wazi ni SMZ, lakini ninachotaka
kuwaambia Maalim Seif hana nyumba Dar es Salaam.
“… kama wapo viongozi waliopewa nyumba wa SMZ ni hao lakini si Maalim
Seif, tangu mwaka 2010 hana nyumba na hufikia hotelini, hana nyumba ya
Serikali wala yake binafsi,” alisema Hamad.
SMZ wazungumza
Alipotafutwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa pili wa Rais wa
Zanzibar, Mohamed Aboud ili kupata ufafanuzi wa suala hilo, alisema
Maalim Seif anastahiki zake kama kiongozi wa SMZ ikiwemo kupatiwa haki
ya matibabu pamoja na mahala pa kuishi.
“SMZ ni wajibu wake kuwahudumia viongozi na wananchi wake kwa ujumla,
Maalim Seif bado ni Makamu wa Kwanza wa Rais hivyo ana wajibu wa
kuhudumiwa.
“Na katika hili anahudumiwa na SMZ ikiwemo kulipiwa hoteli pindi
awapo nje ya Zanzibar na si hilo tu pia tunahusika kumpa stahiki zake
zote ikiwemo matibabu.
“Kwa kawaida pindi kiongozi yoyote wa kitaifa anapokuwa Dar es Salaam
na kama hana nyumba SMZ hulipa malazi ya kiongozi wake na Maalim bado
ni kiongozi na hata kama akiondoka kwenye uongozi bado anazo stahiki
zake ikiwemo kuhudumiwa kama kiongozi mstaafu,” alisema Waziri Aboud.
Alisema pamoja na hali hiyo kwa sasa Serikali ya Muungano ndiyo
inayolipa gharama za Maalim Seif kuishi hotelini kwa agizo la Rais Dk.
John Magufuli.
Alisema ahadi ya Rais Magufuli ya kusaidia kulipia hoteli anayoishi
Maalim Seif inaonesha ni namna gani Serikali zote mbili ya Muungano na
ile ya Zanzibar zinavyoshirikiana kwa dhati.
“Kwa ubinadamu wake Rais Magufuli tunamshukuru sana kwani inaonesha
namna gani kiongozi huyo wa Jamhuri ya Muungano alivyo na mapenzi mema
na Zanzibar pamoja na viongozi wake.
“… ila pamoja na yote SMZ bado ina wajibu wa kutekeleza wajibu wake
wa kuwatunza viongozi wake wote wakiwemo waliokuwa ndani ya Serikali
pamoja na wale waliostaafu,” alisema Aboud.
Viongozi wamimika kumjulia hali
Tangu aliporuhusiwa kutoka hospitali kwa kiongozi huyo alikokuwa
amelazwa katika Hospitali ya Hindu Mandal jijini Dar es Salaam, viongozi
mbalimbali wamekuwa wakimiminika kumjulia hali.
Machi 9, mwaka huu Rais Dk. John Magufuli, alikwenda katika Hoteli ya Serena kumjulia hali kiongozi huyo.
Maalim Seif yupo hotelini hapo kwa mapumziko baada ya kutolewa hospitalini hapo Machi 8, mwaka huu alipokuwa amelazwa.
Katika mazungumzo yake na Rais Magufuli, Maalim Seif
aliwawahakikishia Watanzania kuwa afya yake inaendelea vizuri na kwamba
anaendelea na shughuli zake na siku chache zijazo ana matumaini ya
kurejea katika hali yake ya kawaida.
Mbali ya kukutana na kiongozi huyo wa nchi, siku iliyofuata hasimu
wake wa kisiasa ambaye ni Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein naye
alikwenda kumwona pamoja na wanasiasa mbalimbali akiwemo Waziri Mkuu
mstaafu, Dk. Salim Ahmed Salim na Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa.
Msimamo wa Maalim
Maalim Seif, amesema mikutano yake ya hivi karibuni na Rais Dk. John
Magufuli na Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohammed Shein haikuwa na agenda
yoyote ya kujadili hali ya kisiasa inayoendelea visiwani Zanzibar.
Kauli hiyo ya Maalim Seif aliitoa baada ya kuibuka minong’ono baada ya kutembelewa na viongozi hao wa juu wa Serikali.
Hatua hiyo ya kukutana na viongozi hao ilizusha hisia kuwa huenda
kulikuwa na jambo zito la kisiasa hasa ikizingatiwa kwamba zilikuwa
zimebaki siku takriban 10 kufanyika kwa uchaguzi wa marudio visiwani
humo ambao kiongozi huyo wa upinzani ametangaza kuwa chama chake
hakitashiriki.
Maalim Seif alisema Dk. Shein alikwenda kumjulia hali kibinadamu kama
ilivyokuwa kwa Rais Magufuli na watu wengine wenye mapenzi mema, hivyo
hakuna haja kwa Wazanzibari kuwa na hofu yoyote.
“Tusingeweza kuzungumza lolote wakati afya yangu siyo nzuri sana.
Unapozungumza mambo mazito kama hayo ya uchaguzi lazima uwe mzima
kimwili na kiakili,” alisema Maalim Seif baada ya kujuliwa hali na
Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa.
Maalim ambaye alikuwa mgombea wa urais kwa tiketi ya CUF katika
Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25 mwaka jana alisusia uchaguzi huo wa marudio
uliopangwa kufanyika Machi 20, mwaka huu.
Marudio hayo ni kutokana na Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya
Zanzibar (ZEC), Jecha Salim Jecha kufuta matokeo ya awali kutokana na
kile kilichodaiwa kukiukwa kwa taratibu.
Jecha na karatasi za kura
Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), Jecha Salim Jecha,
amesema ZEC imefanya marekebisho ya katarasi za kura na zinatarajiwa
kufika visiwani humo Machi 17, mwaka huu.
Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari aliyotolewa jana Jecha
alisema baada ya kubainika kasoro katika jina la mgombea wa Chama cha
ADA-TADEA, ZEC imefanya marekebisho.
“Tunaishukuru Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kwa mashirikiano
iliyoyaonesha katika kusahihisha kasoro zilizojitokeza na tunapenda
kuwahakikishia wananchi na jumuiya za kimataifa kuwa uchaguzi utakuwa wa
haki, huru na uwazi,” alisema Jecha katika taarifa yake.
CHANZO:MTANZANIA
Post a Comment