Na Benjamin Sawe
HISTORIA
ya jina la Kariakoo na soko la Kariakoo inaanzia tangu enzi za ukoloni
wa Mjerumani wakati Tanzania Bara ikiitwa Tanganyika.
Mahala
lilipo soko hilo palijengwa jengo la utawala wa Wajerumani ambalo
lilikusudiwa litumike kama ukumbi wa kuadhimisha sherehe za kutawazwa
kwa Mfalme Kaiser Wilheim wa Ujerumani kwa wakati huo.
Hata
hivyo baada ya jengo kukamilika halikutumika kama ilivyokusudiwa kuwa
na badala yake lilitumika kama kambi ya kikosi cha wapagazi waliobeba
mizigo ya Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia waliojulikana kama Carrier Corps.
Jina
hilo la maaskari wabeba mizigo katika Kiswahili lilitamkwa ‘karia- koo’
na liliendelea kutumika kama jina la eneo lote linalozunguka jengo hili
la Soko la Kariakoo.
Meneja
Mkuu wa Soko la Kariakoo, Florens Seiya anasema baada ya Vita Kuu ya
Kwanza ya Dunia kuisha rasmi mwaka 1919 na nchi Tanganyika kuanza
kutawaliwa na Waingereza, jengo hilo lilianza kutumika kama soko na
kuhudumia wakazi wa Dar es Salaam.
Anasema
wakati huo wafanyabiashara walikuwa wakiuza bidhaa zao sakafuni kwa
sababu hapakuwa na meza. Wafanyabiashara hao waliendelea kufanya
biashara zao sakafuni hadi miaka ya 1960, meza za saruji zilipojengwa.
Seiya anasema kwa kadiri jiji la Dar es Salaam lilivyokua na wakazi wake
kuongezeka, ndivyo soko hilo la lilivyozidiwa na kushindwa kumudu kutoa
huduma nzuri kwa wananchi.
Wafanyabiashara
walifanya shughuli zao katika hali ngumu kwa sababu kulikuwa na
msongamano mkubwa wa watu pia hapakuwepo ghala za kuhifadhia bidhaa.
Hali
hiyo iliwafanya viongozi wa halmashauri ya jiji kuona haja ya kuwa na
soko kubwa na la kisasa kulingana na maendeleo ya jiji, na hivyo
wakaanza kujadili uwezekano wa kujenga soko jipya kubwa na la kisasa.
Uamuzi wa kujenga Soko Kuu la Kariakoo ulifanywa na serikali mwaka 1970
ambapo Halmashauri ya jiji la Dar es Salaam iliagizwa kujenga soko jipya
la kisasa ambalo lingechukua nafasi ya soko la zamani.
Anasema
matarajio ya serikali ya kujenga soko hilo yalikuwa ni kuwapatia wakazi
wa jiji soko kubwa la chakula ambalo lingetosheleza mahitaji yao kwa
muda wa miaka 50 hadi 70 Mipango ilikamilika na ujenzi ulianza rasmi
Machi 1971.
Ramani
ya jengo la soko ilitayarishwa na mchoraji wa ramani za majengo
Mtanzania Beda Amuli. Kwa mujibu ya machapisho yanayoelezea historia ya
soko hilo, mkandarasi huyo alitakiwa kwenda kujifunza katika nchi za
Accra – Ghana na Lusaka-Zambia, kuangalia masoko yaliyojengwa katika
miji hiyo miwili, ndipo atengeneze ramani yake, ambalo ndiyo soko
linaloonekana hivi sasa.
Anasema
kuwa, mkandarasi aliyechora jengo hili ameweka baadhi ya maumbo
yanayofanana na majengo hayo aliyokwenda kuyatazama. Hii ndiyo sifa
pekee inalolifanya soko hili la Kariakoo kuwa la tofauti na masoko
mengine katika ukanda huu wa Afrika Mashariki na Kati.
Ujenzi
wa soko ulikamilika Novemba 1975 kwa gharama ya Sh milioni 22 na
kufunguliwa rasmi Desemba mwaka huo huo ambapo Rais wa Kwanza wa
Tanzania, Mwalimu Julius Nyerere alikuwa mgeni rasmi. Jengo la Soko Kuu
la Kariakoo lipo katika kiwanja namba 32 mtaani Kariakoo, katikati ya
makutano ya mtaa wa Mkunguni na mtaa wa Nyamwezi na limezungukwa na
mitaa ya Nyamwezi, Mkunguni, Sikukuu na Tandamti.
Soko
hilo lina majengo mawili ambayo yameunganishwa katika Ghorofa ya chini
ya ardhi. Jengo la kwanza linaweza kuitwa soko kubwa na jengo la pili
soko dogo. Soko kubwa limegawanyika katika sehemu tatu ambayo ni ghorofa
ya kwanza, sehemu ya katikati na ya chini maarufu kama shimoni.
Eneo
la Shimoni kuna mabucha 16 yanayouza nyama iliyokaguliwa kiafya toka
mikoa ya Dodoma, Mwanza na Shinyanga, na samaki wabichi toka maziwa na
mito ya Tanzania. Soko dogo ni la rejareja ambalo si tofauti na masoko
mengine katika Jiji la Dar es Salaam.
Ingawa
eneo la Kariakoo limezungukwa na maduka yanayouza bidhaa mbalimbali,
bado Soko la Kariakoo ndio soko kuu la mazao na bidhaa ya kilimo nchini.
Linauza mazao kwa bei ya jumla ya rejareja pamoja na vifaa vya kilimo.
Shirika
la Masoko ya Kariakoo (SMK) linasimamia uendeshaji wa biashara za Soko
la Kariakoo, kuweka kipaumbele katika shughuli za biashara mbili:
Anasema shirika linakodisha ardhi ya biashara kwa wauzaji wa Rejareja.
Pia
eneo la soko hilo lina maduka 82 katika soko kuu, yanayokodishwa kwa
SMK kwa wauzaji wa rejareja. Mbali na mazao ya kilimo, maduka mengi
yanauza vifaa vya kilimo na elektroniki. Pia, soko linatoa baadhi ya
maduka nje yanayouza mboga za majani za rejareja katika soko dogo la
nje.
Kuhusu
uendeshaji wake shirika hilo linasimamia soko la jumla kwa mazao ya
kilimo na jamii ya samaki wakavu linalofanyika eneo la soko. SMK inatoza
asilimia ya faida ambayo si zaidi ya asilimia nane tu ya bei ya mauzo
kwa biashara ya jumla. Vile vile shirika linawatoza wafanyabiashara wa
jumla ada ya usajili.
Kwa
masoko ya jumla na rejareja, Shirika linaweka daraja kati ya wakulima
na wateja, ili wateja waweze kupata mahitaji yao yote ya nyumbani katika
sehemu moja kwa bei nafuu na kuleta uthabiti kwa sekta ya kilimo ya
nchi. Seiya anasema Soko la Kariakoo limekua na kupanuka kwa kiasi
kukubwa ikilinganishwa na wakati lilipofunguliwa rasmi mnamo Desemba 8,
1974.
Kwa
kuwa muendeshaji mkuu wa biashara za mazao yatokayo mikoani kuingia
katika jiji la Dar es Salaam. Pamoja na mafanikio makubwa yaliyopatikana
hivi sasa soko hilo linakabiliwa na changamoto kubwa ya miundombinu.
Ili
kukabiliana na changamoto hiyo kuu na nyinginezo za kuboresha huduma
kwa watumiaji wa soko, shirika linategemea kuunda upya soko na kuanzisha
soko la jumla Dar es Salaam. “Kuanzisha vituo vipya vya jumla ni njia
mojawapo ya mipango ya maendeleo ya jiji na maeneo yao ya jirani.
Anaelezea
miradi inayotarajiwa kuanzishwa na shirika hilo kuwa ni ujenzi wa
upanuzi wa soko la rejareja la Kariakoo la leo, kukuza idadi ya magenge
na kurahisisha maegesho ya magari sokoni. “Kwa sasa soko la nje linakosa
maegesho salama ya magari, maduka ya kisasa, ofisi, vyoo, sehemu za
kukaa kwa ajili ya mikutano na mikusanyiko ya kijamii.
Uundaji
upya wa soko utalisaidia shirika kukabiliana na baadhi ya changamoto,”
anasema Seiya. Vile vile ujenzi wa soko la kisasa, litakalokuwa
Buguruni-Chanika, wilaya ya Ilala na ujenzi wa kituo kingine cha soko
litakalokuwa Tabata kwa ajili ya biashara na shughuli za burudani.
Ili
kufanikisha haya, Shirika linahitaji mtaji wa kuanzia ili kufikia
malengo hayo . Kwa juhudi na ufadhili wa serikali, itatoa fursa kwa ubia
binafsi kuwekeza kwenye mradi huu.
Post a Comment