Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki atembelea watumishi katika ofisi zao
Watumishi
wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wameaswa
kufanya kazi kwa bidii na kujituma ili kuongeza ufanisi kwenye maeneo
yao ya kazi.
Kauli
hiyo ilitolewa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika
Mashariki, Mhe. Dkt. Augustine Mahiga (Mb) alipokuwa anatembelea ofisi
za watumishi hao jijini Dar es Salaam jana asubuhi.
”Nimekuja
kuwatembelea katika maeneo yenu ya kazi ili nijionee mazingira
mnayofanyia kazi pamoja na changamoto zinazowakabili ili kwa pamoja
tutafute namna ya kuzitatua”. Mhe. Mahiga aliwaeleza watumishi hao kila
ofisi aliyopita.
“Lengo
la ziara yangu kwenu ni kuwatia morari ili mfanye kazi kwa bidii na kwa
ubunifu wa hali ya juu ili tuweze kufikia malengo tuliyojiwekea kwa
mwaka huu wa fedha 2016/2017. Kutimia kwa Malengo ya taasisi moja moja
kama yetu ndiyo itapelekea kufikiwa kwa malengo ya Dira ya Maendeleo ya
Taifa awamu ya pili ambayo imejikita katika uwekezaji wa viwanda”.
Alisema
watumishi hawana budi kufanya kazi kwa bidii na kutoa huduma bora kwa
wananchi kwa kuwa Serikali yao chini ya Mhe. Dkt. John Pombe Joseph
Magufuli imejipanga kuboresha maslahi yao. Alisema dhamira hiyo
imedhihirishwa na kitendo cha Rais Magufuli kupunguza kodi ya mapato
(payee) kutoka asilimia 11 hadi 09.
Aliwataka
watumishi kuepuka vitendo vya ubadhirifu badala yake kufanya kazi kwa
kuzingatia kanuni za utumishi na kuonya kuwa, Serikali haitamvumilia
mtumishi yeyote atakayebainika kwenda kinyume na maadili ya utumishi.
Waziri
Mahiga aliendelea kuwaeleza watumishi wake kuwa Wizara ya Mambo ya Nje
ambayo inajukumu la kuratibu Sera ya Mambo ya Nje ya Nchi ina mchango
mkubwa wa kuhakikisha kuwa Tanzania inaendelea kuwa na jina zuri na
kubwa ulimwenguni kote ili sifa hiyo itumike vizuri kuvutia uwekezaji wa
viwanda nchini.
“Alisema kwa nafasi zenu nyie watumishi mlio hapa Makao Makuu na wale wa Balozini lazima mshirikiane
kwa pamoja kwa kutumia taaluma zenu na vipaji alivyowapa Mwenyezi Mungu
kuzitangaza rasilimali za Tanzania ulimwenguni kote, kwa madhumuni ya
kuvutia uwekezaji na utalii ili kuongeza mapato ya Serikali na ajira kwa
Watanzania”.
Alihitimisha
nasaha zake kwa kuwakumbusha watumishi kaulimbiu ya Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli ya “Hapa
kazi tu” Alisema kauli hiyo lazima itafsiriwe kivitendo kwa kila
mtumishi bila kusahau kuweka mbele uzalendo na uadilifu katika
utekelezaji wa majukumu.
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki
Dar es Salaam, 23 Juni 2016.
Post a Comment