Featured

    Featured Posts

    Social Icons

Loading...

TAARIFA KWA UMMA: Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki atembelea watumishi katika ofisi zao



Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki atembelea watumishi katika ofisi zao

Watumishi wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wameaswa kufanya kazi kwa bidii na kujituma ili kuongeza ufanisi kwenye maeneo yao ya kazi.

Kauli hiyo ilitolewa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Augustine Mahiga (Mb) alipokuwa anatembelea ofisi za watumishi hao jijini Dar es Salaam jana asubuhi.

”Nimekuja kuwatembelea katika maeneo yenu ya kazi ili nijionee mazingira mnayofanyia kazi pamoja na changamoto zinazowakabili ili kwa pamoja tutafute namna ya kuzitatua”. Mhe. Mahiga aliwaeleza watumishi hao kila ofisi aliyopita.

“Lengo la ziara yangu kwenu ni kuwatia morari ili mfanye kazi kwa bidii na kwa ubunifu wa hali ya juu ili tuweze kufikia malengo tuliyojiwekea kwa mwaka huu wa fedha 2016/2017. Kutimia kwa Malengo ya taasisi moja moja kama yetu ndiyo itapelekea kufikiwa kwa malengo ya Dira ya Maendeleo ya Taifa awamu ya pili ambayo imejikita katika uwekezaji wa viwanda”.

Alisema watumishi hawana budi kufanya kazi kwa bidii na kutoa huduma bora kwa wananchi kwa kuwa Serikali yao chini ya Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli imejipanga kuboresha maslahi yao. Alisema dhamira hiyo imedhihirishwa na kitendo cha Rais Magufuli kupunguza kodi ya mapato (payee) kutoka asilimia 11 hadi 09.

Aliwataka watumishi kuepuka vitendo vya ubadhirifu badala yake kufanya kazi kwa kuzingatia kanuni za utumishi na kuonya kuwa, Serikali haitamvumilia mtumishi yeyote atakayebainika kwenda kinyume na maadili ya utumishi.

Waziri Mahiga aliendelea kuwaeleza watumishi wake kuwa Wizara ya Mambo ya Nje ambayo inajukumu la kuratibu Sera ya Mambo ya Nje ya Nchi ina mchango mkubwa wa kuhakikisha kuwa Tanzania inaendelea kuwa na jina zuri na kubwa ulimwenguni kote ili sifa hiyo itumike vizuri kuvutia uwekezaji wa viwanda nchini.

“Alisema kwa nafasi zenu nyie watumishi mlio hapa Makao Makuu na wale wa Balozini lazima  mshirikiane kwa pamoja kwa kutumia taaluma zenu na vipaji alivyowapa Mwenyezi Mungu kuzitangaza rasilimali za Tanzania ulimwenguni kote, kwa madhumuni ya kuvutia uwekezaji na utalii ili kuongeza mapato ya Serikali na ajira kwa Watanzania”.

Alihitimisha nasaha zake kwa kuwakumbusha watumishi kaulimbiu ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli ya  “Hapa kazi tu” Alisema kauli hiyo lazima itafsiriwe kivitendo kwa kila mtumishi bila kusahau kuweka mbele uzalendo na uadilifu katika utekelezaji wa majukumu.



Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki
Dar es Salaam, 23 Juni 2016.

RAIS DKT. JOHN POMBE MAGUFULI AMUAPISHA DKT. ASHA-ROSE MIGIRO KUWA BALOZI WA TANZANIA NCHINI UINGEREZA

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akimpongeza Dkt. Asha-Rose Migiro mara baada ya kumuapisha kuwa Balozi wa Tanzania nchini Uingereza katika Ikulu ndogo ya Chamwino mkoani Dodoma.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akimpongeza Dkt. Asha-Rose Migiro mara baada ya kumuapisha kuwa Balozi wa Tanzania nchini Uingereza katika Ikulu ndogo ya Chamwino mkoani Dodoma.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akiwa katika picha na Dkt. Asha-Rose Migiro Balozi wa Tanzania nchini Uingereza, Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan pamoja na Katibu Mkuu Kiongozi Balozi John Kijazi katika Ikulu ndogo ya Chamwino Mkoani Dodoma.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akizungumza jambo na Dkt. Asha-Rose Migiro Balozi wa Tanzania nchini Uingereza huku Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan pamoja na Waziri wa Mambo ya Nje Balozi Augustine Mahiga wakisikiliza.

BALOZI MAHIGA:MKE WANGU HAKUMTUKANA ASKARI,WALIPISHANA KAULI


Amesema mke wake hakumtukana askari aitwaye Deogratias Mbando bali walipishana. "Nilifuatilia suala hili, walitofautiana tu kauli. Mama hakutukana" alisema. Hata hivyo alisema suala hilo limeisha na asingependa kuendeleza malumbano hayo.
Chanzo: Mtanzania
 

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Italia afanya ziara nchini Tanzania

 Naibu Waziri wa Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, Mhe. Dkt. Susan Kolimba akimkaribisha Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Italia, Mhe. Dkt. Mario Giro ambaye yupo nchini kwa ziara ya kikazi ya siku tatu kuanzia tarehe 5 Februari, 2016, ambapo alitembelea ofisi za Wizara kwa ajili ya kufanya mazungumzo ya kuimarisha ushirikiano kati ya nchi hizi mbili.
Mhe. Dkt. Mario Giro akizungumza na Mhe. Dkt. Susan Kolimba ambapo katika mazungumzo yao walijadili uhusiano wa kidiplomasia baina ya mataifa hayo hasa katika sekta ya uchumi na kusisitiza juu ya suala la kukuza na kuendeleza sekta binafsi. Pia nafasi ya Italia katika kusaidia sekta ya elimu ambapo kwa upande wa Tanzania nchi hiyo imekuwa ikitoa ufadhili kwa Taasisi ya Teknolojia ya Dar es Salaam (DIT)
Kushoto ni Mkurugenzi kutoka Wizara ya Mambo ya Nje ya Italia, Dkt. Raffaelle De Lutio  na Balozi wa Italia nchini Mhe. Luigi Scotto ambao waliambatana na Mhe. Dkt. Mario Giro.
Mkurugenzi wa Idara ya Ushirikiano wa Kikanda katika Wizara ya Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa,  Balozi Innocent Shio (kushoto) kwa pamoja na  Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali na Msemaji wa Wizara Bi. Mingi Kasiga ( wa pili kushoto) wakiwa na Bi. Olivia Maboko,  Afisa Mambo ya Nje na Bw. Adam Isara, Msaidizi wa Naibu Waziri wakifuatilia mazungumzo
        Sehemu nyingine ya Wajumbe wakifatilia mazungumzo
Wakiwa katika picha ya pamoja mara baada ya mazungumzo
Balozi Innocent Shio akijadili jambo na Mhe. Dkt. Mario Giro huku Mhe. Kolimba na Bi. Kasiga wakishuhudia.

KONSELI MKUU WA TANZANIA JEDDAH AKARIBISHWA RASMI NA MKURUGENZI MKUU WA WIZARA YA MAMBO YA NJE YA SAUDI ARABIA, NAYE AMWALIKA KUTEMBELEA TANZANIA MWEZI JULAI 2016

Pichani Balozi Muhammad Tayeb, Mkurugenzi Mkuu katika Wizara ya Mambo ya Nje ya Saudi Arabia akimkaribisha Bw. Suleiman Saleh, Konseli Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jeddah, na kufanya nae mazungmzo kuhusu mahusiano baina ya Saudi Arabia na Tanzania.

Kwa mujibu wa Balozi Tayeb, kusainiwa kwa makubaliano hayo kumefungua ukurasa mpya wa mahusiano baina ya Saudi Arabia na Tanzania na hakusita kuonyesha furaha yake kutokana nakuainishwa maeneo mahususi ya mashirikiano  katika sekta za uchumi, uwekezaji na biashara. Kwa upande wake Bw. Saleh alimshukuru Balozi Muhammad Tayeb kwa kumkaribisha Ofisini kwake na alifarijika na upendo alionyesha Balozi huyo kwa Tanzania ambapo  alichukwa fursa hiyo kumualika kutembelea Tanzania kujionea vivutio vya utalii Tanzania Bara na Visiwani ambapo aliukubali mwaliko huo na kuahidi kutembelea Tanzania yeye na familia yake mwezi Julai, 2016.

========================================

Konseli Mkuu wa Ubalozi Mdogo wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania uliopo Jeddah, Saudi Arabia, Bw. Suleiman Saleh, Jumanne Machi 29, 2016, amekaribishwa rasmi katika Wizara ya Mambo ya Nje ya Saudi Arabia alipokutana na kufanya mazungumzo na Balozi Muhammad A. Tayeb, Mkurugenzi Mkuu wa Wizara hiyo.

Balozi Tayeb alimpokea Bw. Saleh Ofisini kwake Jeddah na kuahidi kutoa ushirikiano unaohitajika katika kuimarisha mahusiano baina ya Saudi Arabia na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kufuatia kusainiwa hivi karibuni Ikulu, Dar-es-Salaam, makubaliano ya mashirikiano baina ya nchi hizo mbili. Makubaliano hayo ambayo yalisainiwa na  Mhe. Adil Jubeir, Waziri wa Mambo ya Nje wa Saudi Arabia na Mhe. Balozi Augustine Mahiga, Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, yalishuhudiwa pia na Mhe. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Mkurugenzi Mkuu Msaidizi wa UNESCO kwa upande wa Afrika atembelea Wizara ya Mambo ya Nje

Mkurugenzi wa Idara ya Ushirikiano wa Kimataifa katika Wizara ya Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, Balozi Celestine Mushy (kulia) akisalimiana na Mkurugenzi Mkuu Msaidizi wa UNESCO kwa upande wa Afrika, Bw. Firmin Matoko walipokutana kwa ajili ya mazungumzo kwenye Ofisi za Wizara ya Mambo ya Nje.


Balozi Mushy akiwa katika mazungumzo na Mkurugenzi Mkuu Msaidizi wa UNESCO kwa upande wa Afrika, Bw. Firmin Matoko. Mazungumzo hayo pamoja na Mambo mengine yalijikita katika vipaumbele vya UNESCO ambavyo ni elimu na jinisia. Kwa upande wa elimu, Balozi Mushy alieleza hatua ya Serikali ya awamu ya tano kutoa elimu bure kwa shule za msingi na sekondari. Kuhusu jinsia, alieleza hatua ya Serikali ya kujumuisha wanawake katika nafasi za uongozi ikiwa ni pamoja na kuimchagua Makamu wa Rais Mwanamke wa kwanza. Mwingine katika picha ni Mwakilishi wa UNESCO nchini Tanzania, Bi. Zulmira Rodrigues.

Wajumbe wakiendelea na mazungumzo


Afisa kutoka Wizara ya Mambo ya Nje, Bi. Ngusekela Nyerere na Afisa wa UNESCO wakinukuu mambo muhimu ya mazungumzo.


Balozi Mushy akisikiliza kwa makini maelezo kutoka kwa Bw. Matoko.


Picha ya pamoja.

MUENDELEZO WA HABARI: AGIZO LA RAIS MAGUFULI LAANZA KUTEKELEZWA WAZIRI MAHIGA ARUDISHA FOMU

Baada ya waziri mkuu kutaja majina ya mawaziri wanne na naibu waziri mmoja ambao hawajarudhisha fomu za Sekretariati ya maadili ya umma na kutakiwa wawe wamerejesha fomu hizo mpaka saa kumi na mbili jioni ijumaa ya leo mpaka sasa ni waziri mmoja aliyetii agizo hilo

Aliyerudisha fomu hizo ni waziri wa mambo ya nje,ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa Mhe.Balozi dkt.Augustine Mahiga ambapo amekiri kuwa ni kweli alikuwa hajarudisha fomu hizo kutokana na majukumu ya kazi yaliyokuwa yamembana
 
ITV pia imefanikiwa kuongea na waziri wa mambo ya ndani Charles Kitwanga ambaye naye ametajwa kutorudisha fomu hizo ambapo ameshangaa jina lake likitajwa wakati ameshazirudisha na kwa sasa  ameelekea ofisi za Sektretariati ya maadili kuwasilisha malalamiko yake
 
Pia ITV  naibu waziri wa ofisi ya makamu wa rais,Muungano na Mazingira Mhe.Luhaga Mpina ambapo amesema kuwa atawahisha kurudisha fomu hizo kabla ya saa kumi na mbili jioni.

TANZANIA MWENYEJI WA MKUTANO WA JPC NA ZAMBIA

Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali na Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, Bi. Mindi Kasiga  akiwakaribisha wageni waalikwa ambao ni Viongozi na Maafisa wa Serikali za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Zambia katika Mkutano wa Tume ya Kudumu ya Pamoja ya Ushirikiano kati ya Tanzania na Zambia (JPC) unaofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere kwa muda wa siku mbili kuanzia leo.
Mkurugenzi wa Idara ya Afrika katika Wizara ya Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, Balozi Samuel Shelukindo akimkaribisha Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, Mhe. Balozi Ramadhan Mwinyi hayupo pichani ili aweze kufanya ufunguzi wa Mkutano huo.
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, Mhe. Balozi Ramadhan Mwinyi akifungua rasmi Mkutano wa JPC kati ya Tanzania na Zambia.
Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Ushirikiano wa Kimaendeleo na Mashirika ya Kimataifa, Bw. Sylvester Mundanda  ambaye alimuwakilisha Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje ya nchini Zambia akiwasilisha ujumbe wa Serikali ya Zambia katika mkutano huo.




Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya nchini Zambia, Bi. Angela Mulenga ambaye aliambatana na ujumbe wa maafisa walioiwakilisha Serikali ya Zambia katika Mkutano huo akijadili jambo na Bw. Sylvester Mundanda.
Balozi wa Zambia nchini Tanzania, Mhe. Judith Kapijimanga (kushoto) na Balozi wa Tanzania nchini Zambia, Mhe. Balozi Grace Mujuma wakijadili jambo wakati wa mkutano huo.





 Sehemu ya maafisa wa Serikali ya Zambia wakifuatilia Mkutano.
Sehemu ya maafisa wa Serikali ya Tanzania wakifuatilia Mkutano.

Serikali za Tanzania na Zambia zinakutana katika kikao cha siku mbili kujadili na kukubaliana maeneo ya ushirikiano ambayo watayasimamia  kwa pamoja kwa lengo la kuongeza kasi ya maendeleo ya nchi hizo mbili. Kikao hicho kinachojulikana kama Tume ya Kudumu ya Pamoja ya Ushirikiano kati ya Tanzania na Zambia (JPC) kinafanyika kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere kuanzia leo.

Katika hotuba yake ya ufunguzi, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, Balozi Ramadhan Muombwa Mwinyi alieleza kuwa uhusiano wa Tanzania na Zambia ni mzuri na kufanyika kwa kikao hicho ni uthibitisho dhahiri.

 Aidha, Balozi Mwinyi  alieleza kuwa kufanyika kwa kikao hicho kunatoa fursa kwa wajumbe kuchambua kwa pamoja hatua zilizofikiwa na changamoto  zilizojitokeza katika utekelezaji wa maeneo yaliyoafikiwa wakati wa kikao cha 8 cha JPC kilichofanyika Lusaka Juni 2006. Maeneo hayo ni pamoja na biashara, viwanda, mawasiliano, uchukuzi, nishati, uhamiaji, kilimo, elimu, michezo, madini, utalii, maliasili na utamaduni.

“Haya ni baadhi ya maeneo ambayo nchi zote mbili zinayapa umuhimu mkubwa ili kuharakisha maendeleo ya pande zote mbili Katika majadiliano yetu tutalenga zaidi maeneo haya ili tubuni utaratibu mzuri wa kushirikiana katika utekelezaji kwa lengo la kuleta tija kwa nchi na wananchi wake”. Balozi Mwinyi alifafanua.

Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Ushirikiano wa Kimaendeleo na Mashirika ya Kimataifa kutoka Wizara ya Mambo ya Nje ya Zambia, Bw, Sylevester Mundanda alieleza kuwa Tanzania na Zambia zimejaliwa kuwa na maliasili lukuki kama vile ardhi, madini, maji na wanyama pori, hivyo, endapo kama zitatumiwa vizuri zinaweza kubadilisha uchumi wa nchi hizo kwa ajili ya kuwaletea maisha bora wananchi wake.

Alisisitiza umuhimu wa kukubaliana maeneo machache ya kipaumbele na kuyawekea mikakati ya utekelezaji na ubunifu bila kusahau kujiwekea utaratibu wa kupima ufanisi kila baada ya muda. 

Bw, Mundanda alihitimisha kwa kusema kuwa vikao vya JPC ni fursa nzuri kujadili changamoto za kiuchumi na kubuni mikakati ya pamoja kukabiliana nazo ili uchumi uweze kukua kwa faida ya wananchi wa pande zote.

Watumishi wa Mambo ya Nje wapata somo kuhusu umuhimu wa Viwanda vidogo katika maendeleo ya nchi

 Meneja Mkuu wa Kampuni ya SG ya nchini India, Dkt. Pralay Dey akiwasilisha mada  kuhusu Role of SMEs in Industrialization: Lessons from India kwa Watumishi kutoka Wizara ya Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, Taasisi na Idara mbalimbali za Serikali (hawapo pichani), katika mhadhara huo uliofanyika katika Ukumbi wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam Dkt. Dey alieleza umuhimu wa Tanzania kuwa na mradi wa Mfano wa Uzalishaji wa Viwanda Vidogo "incubator" ili kufikia mapinduzi ya viwanda na kuwawezesha Watanzania kupata ajira.
Mkurugenzi wa Idara ya Asia na Australasia, Balozi Mbelwa Kairuki (kushoto) pamoja na Naibu Balozi wa India, Bw. Robert, wakifuatilia mada kutoka kwa Dkt. Dey (hayupo pichani).

Mkurugenzi wa Idara ya Ushirikiano wa Kimataifa katikaWizara ya Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, Balozi Selestine Mushi akiwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Viwanda Vidogo Vidogo nchini (SIDO) Injinia Omary Bakari wakifuatilia mada.
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali na Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa. Bi. Mindi Kasiga ambaye pia alikuwa mratibu na muongozaji wa Mdahalo naye akifuatilia mdahalo huo.

Mmoja wa washiriki wa mdahalo huo akichangia hoja.
Baadhi ya Maafisa kutoka Taasisi na Idara mbalimbali za Serikali walioshiriki Mhadhara ulioandaliwa na Wizara ya Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa.
Baadhi ya Wakurugenzi wa Wizara ya Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa wakijadili jambo na mtoa mada mara baada ya kumaliza mhadhara huo.
Picha ya pamoja.

PICHA NA IKULU:WAZIRI WA MAMBO YA NJE DKT MAHIGA AMWAKILISHA RAIS MAGUFULI KUWAANDALIA MABALOZI MCHAPALO WA MWAKA MPYA (SHERRY PARTY) IKULU JIJINI DAR ES SALAAM JANA

Mahi1: Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, Mhe. Dkt. Augustine Mahiga akihutubia wakati  akimuwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano ya Tanzania Dkt John Pombe Joseph Magufuli katika Mchapalo wa Mwaka Mpya kwa Mabalozi na Wawakilishi wa Taasisi mbalimbali za Kimtaifa maarufu kama "Sherry Party" Ikulu jijini Dar es salaam leo Jumatatu February 8, 2016


  Mabalozi na Wawakilishi wa Taasisi mbalimbali za Kimtaifa wakimsikiliza Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, Mhe. Dkt. Augustine Mahiga akihutubia wakati  akimuwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano ya Tanzania Dkt John Pombe Joseph Magufuli katika Mchapalo wa Mwaka Mpya  maarufu kama "Sherry Party" Ikulu jijini Dar es salaam leo Jumatatu February 8, 2016.PICHA NA IKULU

VACANCY ANNOUNCEMENT-WORLD METEOROLOGICAL ORGANIZATION (WMO)




VACANCY ANNOUNCEMENT FROM THE WORLD METEOROLOGICAL ORGANIZATION (WMO)
The Ministry of Foreign Affairs, East Africa, Regional and International Cooperation has received Vacancy Notice No. 1950 from the World Meteorological Organization (WMO) for qualified individuals to apply. 
The deadline for application is 17th February, 2016.  Qualified female and male candidates are equally welcome to apply.
The vacancy is attached bellow.
 “The Ministry encourages qualified Tanzanians to apply”.
 =============================================

Issued by: The Ministry of Foreign Affairs, East Africa, Regional and International Cooperation, Dar es Salaam.
08th February, 2015

Mahiga ataka wahisani wamlainishe Maalim Seif.

  Kuteta na mabalozi wa nchi zote leo
Waziri wa Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, Balozi Dk. Augustine Mahiga.
......
Waziri wa Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, Balozi Dk. Augustine Mahiga, amewataka washirika wa maendeleo wakishawishi Chama Cha Wananchi (CUF) kishiriki uchaguzi wa marudio visiwani Zanzibar ili kuwatendea haki wanachama wake.
 
Akizungumza na Nipashe katika mahojiano maalumu mjini Dodoma, Balozi Mahiga alisema wahisani wanapaswa kuchukua jukumu hilo ili CUF iache kususia uchaguzi uliopangwa kurudiwa Machi 20, mwaka huu na kuendelea kumsimamisha mgombea wao wa urais, Maalim Seif Sharif Hamad, kwa vile wao (wahisani) ndio wanaoonekana kusikilizwa zaidi na chama hicho kuliko serikali. 
 
Alisema CUF ambayo miongoni mwa viongozi wake, Katibu Mkuu Maalim Seif, imekuwa karibu zaidi na wahisani ndiyo maana  wameonyesha ghadhabu dhidi ya Serikali ya Tanzania kwa kukatisha misaada, ikiwamo inayotoka Shirika la Marekani la Changamoto za Milenia (MCC).
 
Zanzibar iko katika mkwamo wa kisiasa baada ya Tume ya Uchaguzi visiwani humo (ZEC) kufuta matokeo ya uchaguzi mkuu uliofanyika Oktoba 25, 2015 kutokana na kile kilichoelezwa na mwenyekiti wake, Jecha Salim Jecha, kwamba ulijawa na kasoro nyingi zilizoupotezea sifa ya kuwa ‘huru na wa haki’. 
 
Maalim Seif na wanachama wenzake wametangaza kutoshiriki uchaguzi wa marudio na badala yake kusisitiza ZEC iendelee na majumuisho ya kura ili mshindi ajulikane. 
 
Hata hivyo, Chama Cha Mapinduzi (CCM) kilichomsimamisha Dk. Ali Mohamed Shein kutetea nafasi yake ya urais, kinaungana na ZEC kuwa uchaguzi ni lazima urudiwe.
       
Akieleza zaidi kuhusu suala hilo la Zanzibar, Balozi Mahiga alisema pamoja na mvutano uliopo sasa visiwani humo, anaamini bado kuna nafasi ya kutosha kwa pande zote kuzungumza ili kufikia maridhiano, ingawa mojawapo ya changamoto zilizopo ni pamoja na hali ya kutoaminiana.  
 
“Naona kwa sababu sisi wenyewe ile inaitwa confidence (kuaminiana) haipo sana. Kati ya sasa na Machi tuendelee na kipindi cha kujenga kuaminiana kwani bado kuna nafasi ya mazungumzo,” alisema Mahiga.
 
Aliongeza kuwa katika kipindi hiki (sasa hadi Machi), kuwe na ushawishi kwa pande zote kuhusiana na uchaguzi huo. 
“Kupeana ushawishi wa namna fulani… unataka kuwe na maandalizi ya namna gani, ushiriki wa namna gani, tuna karibu siku 50. Lakini pia marafiki zao (CUF) wawashawishi,” alisema Balozi Mahiga.
 
Alipoulizwa ni kwa nini anaona CUF iko karibu zaidi na wahisani hadi kusema ni marafiki zao, alisema; “Ni kwa sababu ya ile ghadhabu wanayoifanyia serikali ya  Tanzania.   Ni kama vile kwa nini huyu mmemfanyia hivi.”
 
Kadhalika, Balozi Mahiga alisema leo atakutana na mabalozi wa nchi zote waliopo nchini na kwamba miongoni mwa mambo yatakayopata nafasi ya kuzungumziwa ni pamoja na suala la Zanzibar.
 
“Kwa nini hivi, mimi tarehe 8 (leo), nakutana na mabalozi wote, kwa niaba ya Rais. Nitazungumza hata na hili, ninavyosema rafiki zao ni kwamba wao si tu wanawasikiliza, wanawafuata… jamani eeh, hivi na hivi, na wale wanawasikiliza. Watu wa upinzani wanawafuata wale (wahisani), inawezekana wana imani zaidi na wale wanaowafuata, na wale wanawasikiliza,” alisema.
 
Aliongeza kuwa: “Jamani ni hivi na hivi na hivi… sasa sisi wenyewe, imani kati ya sisi kwa sisi imepungua. Lakini wakikimbilia kule wanasikilizwa, ndiyo tunasema mnavyozungumza na hao marafiki, au kama siyo marafiki, basi  hao watu wanaokuja, mjaribu kuwashawishi.
 
 “Hebu fikiria, chama ambacho kina wafuasi wengi wasishiriki katika uchaguzi… tutakuwa na miaka mitano ya aina gani? Tutarudi kule nyuma tulipotoka. Siyo sahihi, hatuwatendei haki watu wa Zanzibar, hatuwatendei haki Watanzania wengine ambao wote tunabeba mzigo sasa hivi kwa sababu ya maamuzi tu ya chama kimoja.”
 
Bila kufafanua, alisema watu wanaadhibiwa kwa kitu ambacho kina majibu, huku akisema kwenye siasa lazima watu wakubali kuwa na machaguo mbalimbali na siyo kung’ang’ania msimamo mmoja.
 
Alisema amekuwa akiulizwa sana suala la hali ya Zanzibar kila anapokwenda nje, lakini yeye amekuwa akiwaeleza uhalisia wa mambo ulivyokuwa mpaka uchaguzi ukafutwa.
 
Dk. Mahiga alisema jibu ambalo huwapa ni kwamba pamoja na kuwa Tanzania ni Serikali ya Jamhuri ya Muungano, Zanzibar ina madaraka tosha ya mambo yake ya ndani, serikali yake, Katiba, Bunge (Baraza la Wawakilishi)  na Tume ya Uchaguzi.
 
Pia alisema huwaeleza kwamba uchaguzi wa Zanzibar ni tofauti na ule wa Tanzania na namna hata walivyomchagua Rais wa Muungano, John Magufuli.
 
“Serikali ya Zanzibar ina uamuzi wake, utaratibu wake, na  utamaduni wake wa kisiasa ambao ni tofauti. Kwa hiyo mtu akisema ni Tanzania lakini Zanzibar  haikuwa hivi, Tanzania si mkoa, Tanzania ni serikali… kwa hiyo hilo lazima lijulikane hivyo,” alisema. 
 
Aliongeza kuwa katika  mantiki hiyo ya Zanzibar kuwa na aina yake ya serikali na mwelekeo wake, pia wana utamaduni wa kutatua matatizo yao wenyewe.
 
“Tuliona huko nyuma wakati ule kuna matatizo kati ya vyama na serikali, na vyama vya upinzani, hatimaye wakakaa na tukapata muafaka wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa. Hii ilikuwa wao tu pamoja na kuwa watu walisaidia na kuwaambia jamani zungumzeni,” alisema.
 
Balozi Mahiga alisema Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) iliona kuna tatizo Pemba, ambapo idadi ya wapigakura ilikuwa kubwa kuliko walioandikishwa na pia kulikuwa na matatizo katika kuhesabu  kura, hivyo wakaona hata wakitangaza matokeo bado kutakuwa na tatizo.
 
“Kwa hiyo wakasitisha kuhesabu kura. Zingine zilikamilika pamoja na kuwa zilikuwa na utata, zingine wala hazikuhesabiwa na likatokea tamko kwamba uchaguzi umesitishwa.
 
“Baadhi ya watu, mashirika, European Union, Marekani, Commonwealth na wote waliona kwamba tume haikutenda haki… kwamba ingemaliza kuhesabu na matangazo yatoke. Lakini tume iliona kabisa kwamba ikifanya hivyo itakuwa imekiuka maadili  yake,“ alisema.
 
“Kwa hiyo kukawa na mvutano. Kwamba kwa upande wa vyama, walivyopewa maamuzi haya ya tume, wakakaa kuona wafanye nini. Na tukadhani katika hivi vyama kuzungumza kule, na sisi bara watatukaribisha, au Serikali ya Muungano watatukaribisha. Lakini wakasema hata, hili mtuachie sisi wenyewe tutalizungumza kuhusu huu uamuzi wa tume,” aliongeza Balozi Mahiga.
 
Alisema mazungumzo baina ya CUF na CCM yalianza na kufanya takriban vikao sita huku kukiwa hakuna kitu kinachosemwa juu ya kinachoojadiliwa.
 
“Tukasema jamani eeeh, mbona hatusikii tamko lolote? Na hapo ndipo Rais Dk. John Magufuli akachukua uamuzi wa kuzungumza na pande zote mbili. Akazungumza na Masalim Seif (mgombea urais wa CUF), na Dk. Shein kwamba jamani vipi?
 
“Na wao walisema wanazungumza wenyewe na wamejumuisha marais wa zamani wa Zanzibar, si marais wa zamani wa Tanzania. Na kila mtu akawa anauliza hivyo, jamani vipi? Sasa wakati wanazungumza hivyo, baadhi ya wadau wetu wa maendeleo na marafiki zetu wakawa wanasema, Jamhuri ya Muungano hawafanyi vya kutosha kusukuma na kutatua suala hili,” alisema.
 
“Wengine wakasema hata misaada tunasimamisha, kama vile Marekani (MCC) tunasimamisha kwa sababu sisi tunaona haya mazungumzo hayatoi majibu na afadhali tu yatangazwe (matokeo ya uchaguzi) kama yalivyokuwa, lakini katika hilo baadaye tume ikasema jamani, afadhali tuite uchaguzi mwingine.
 
“Sasa mimi ninaloeleza katika hili kwa marafiki zetu ni kwamba kama upinzani wanadai waliungwa mkono na kushinda, sasa hivi hawana cha kuogopa… wana uchaguzi mwingine. Wale waliowachagua na wanaodai kwamba waliwapa ushindi kwa nini wasiwachague kama walivyowachagua huko (awali),” alisema Balozi Mahiga.
 
Alisema jambo kubwa hivi sasa ni kuhakikisha uchaguzi huu utapangwa kwa namna ambayo ni ya wazi na utakuwa wa haki na unasimamiwa ipasavyo na watu mbalimbali, ikiwezekana hata wa nje wakaribishwe tena ili watazame.
 
Alisema anaona kufanya uchaguzi mwingine ni suluhisho kuliko kusema, ‘sisi tumeshinda tutangazwe’, jambo ambalo katikati ya utata uliopo linaweza kuleta fujo.
 
Alisema kwa sababu inaonekana wahisani na nchi zingine wanazungumza zaidi na CUF na wanawabebea mabango, wawaambie kama kweli wana uhakika kwamba walishinda uchaguzi, hawana cha kuogopa bali waende tena kwenye uchaguzi.
 
Balozi Mahiga alisema jambo la msingi ni kuhakikisha mazingira ya uchaguzi yanakuwa huru na haki.
 
SURA YA TANZANIA NJE
Alisema kwa nafasi aliyopewa na Rais Magufuli, atahakikisha sura ya Tanzania nje inakuwa nzuri wakati kiongozi huyo wa nchi (Magufuli) akiendelea kupambana na changamoto za ndani ya nchi.
 
“Nataka kumsaidia Rais ili yeye aunganishe siasa za ndani na maendeleo anayotaka kuyaleta na wizara yangu itakayokuwa inafanya huko nje ya nchi,” alisema.
 
Balozi Mahiga alisema kwa miaka 15, Tanzania imekuwa ikifanya diplomasia ya uchumi, jambo ambalo amepanga kulipeleka mbele zaidi.
 
Alisema katika kuendesha diplomasia hiyo, atahakikisha mkakati wa Rais Magufuli wa kufikia uchumi wa kati na ule wa viwanda, unafanikiwa.
 
“Kuna mambo yanatakiwa kufanyika ili kufika hapo… moja ni kuhakikisha balozi zetu zikishirikiana huku wanapewa majukumu mapya na uwezo mpya. Lazima tufanye uchambuzi kuona ni mambo gani mapya yanatakiwa yafanywe, siyo tu kusema kuleta wawekezaji na kutafuta biashara. Lazima tuende mbali na kusema ni biashara gani,  kama ni mazao, ni yepi? Viwanda vipi,” alisema.
 
Alisema kuna masuala mapya ambayo kama nchi,  yanapaswa kufanyika ikiwa ni pamoja na kuboresha  ushirikiano wa Afrika Mashariki, kikanda na kimataifa.
 
Alisema ushirikiano ni fursa ya kipekee kwani hakuna nchi inayoweza kuendelea yenyewe na pia kwenye jumuiya hizo kuna fursa nyingi.
 
Aliongeza kuwa hata wahisani, wengi wao siku hizi hutoa misaada na mambo mengi kupitia kwenye nchi zilizoungana, hivyo kwa kuwa wizara yake hata jina lake limebadilika na kuhusisha mambo ya Kikanda, Afrika Mashariki na Kimataifa, atahakikisha anafanikisha jambo hilo.
 
MIGOGORO  
Akizungumzia mgogoro wa Ziwa Nyasa, alisema mazungumzo yanaendelea vizuri na kwamba sasa wasuluhishi wanaandaa ripoti ya pili.
 
Kuhusu mgogoro wa Burundi, alisema Tanzania inatambua kwamba kuna tatizo lakini isichoafiki ni Umoja wa Afrika kupeleka jeshi bila ridhaa ya Serikali ya Burundi.
 
Alisema hatua hiyo itasababisha taharuki na watu wataendelea kukimbia na hata kuongeza idadi ya wakimbizi nchini.
 
Alisema hata Marekani iliwahi kupeleka wanajeshi Somalia bila ridhaa ya Serikali ya nchi hiyo, matokeo yake askari wake walikuwa wakiuliwa hovyo na miili yao kuburuzwa mitaani.
 
Kutokana na hali hiyo, alisema Tanzania imefanikiwa kuushawishi Umoja wa Afrika na Umoja wa Mataifa (UN) kuhusiana na Burundi na tayari wamebadilisha uamuzi wao wa kupeleka jeshi nchini humo (Burundi).
 
Alisema hivi sasa, uwezekano unaotakiwa kuangalia ni kuhakikisha mazungumzo yanafanyika na kumalizika na kuangalia uwezekano wa kutumia zaidi polisi kutunza amani na wanajeshi wa kukaa kwenye mpaka wa Burundi ama kunyang’anya silaha kutoka mikononi mwa vikundi visivyostahili kuwa nazo.
CHANZO: NIPASHE

Chediel . Powered by Blogger.
© Copyright Rundugai Blog
Back To Top