Featured

    Featured Posts

    Social Icons

Loading...

MAMBO 15 YALIYOTOKEA KWENYE MKUTANO MKUU WA TAIFA WA CHAMA CHA WANANCHI (CUF) JANA, 21 AGOSTI 2016.


  Picha mbili za kwanza zinamuonesha Ofisa wa Juu wa Polisi (mwenye shati ya kitenge) akimsaidia Lipumba na mabodigadi wake kuvamia Mkutano Mkuu wa Taifa wa CUF.


 Picha ya pili na ya tatu zinaonesha wajumbe Mkutano Mkuu wa CUF wakihesabiwa ili kuamua ikiwa Lipumba ANAONDOKA au ANABAKI.


Na. Mtatiro J
1. Akidi ilitimia pande zote, Bara na Zanzibar na mkutano ulimchagua Ndugu. Julius Mtatiro kwa kura takribani 500 kuwa Mwenyekiti wa Kikao, alifuatiwa na Ndugu. Ridhiwani wa Morogoro aliyekuwa na kura takribani 170 na hivyo ndugu Mtatiro alipitishwa rasmi kuongoza mkutano.

2. Mkutano Mkuu kwa kauli moja ulipitisha ajenda mbili: Moja ni Taarifa ya Barua ya Kujiuzulu kwa Prof. Lipumba na mbili ni Uchaguzi wa Kujaza nafasi wazi za Mwenyekiti Taifa, Makamu Mwenyekiti Taifa na Wajumbe wanne wa Baraza Kuu.

3. Mkutano Mkuu ulianza ajenda ya kwanza chini ya Uenyekiti wa ndugu Mtatiro ambapo Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad alipewa ruhusa ya kueleza taarifa ya kujiuzulu kwa Prof. Lipumba na alieleza jambo hilo kwa kina, hatua kwa hatua.

4. Baadhi ya wajumbe wa Mkutano Mkuu wa CUF wapatao 10 kutoka Tanzania Bara walitoa hoja zao kwa kutaka Kikao kimuite Prof. Lipumba ili aje ajieleze kuhusu kujiuzulu kwake jambo ambalo lilipingwa na wajumbe wengine. Mwenyekiti wa kikao aliwataka wajumbe wanaotaka Lipumba aletwe waweze kueleza kifungu cha katiba au kanuni kinachotaka Kiongozi aliyejiuzulu yeye mwenyewe aitwe kujieleza, wajumbe hao walishindwa kutoa mamlaka ya kikatiba au kikanuni. Wajumbe waliokataa Prof. Lipumba kuja mkutanoni walinukuu ibara ya 117(2) ambayo inataka taarifa ya kujiuzulu kwake ndiyo ipelekwe kwenye mkutano mkuu na siyo yeye mwenyewe. Mwenyekiti wa kikao aliujulisha mkutano kuwa Prof. Lipumba si mjumbe wa kikao kwa hiyo hawezi kuitwa kwa sababu yoyote ile na kwamba mkutano ujadili barua zake na ufanye maamuzi ya kumrudisha au kutomrudisha.

5. Baadhi ya wajumbe wa mkutano mkuu wa CUF kutoka Tanzania Bara walikataa Mkutano Mkuu usifanye maamuzi yoyote. Wajumbe wengine wa Bara walitaka maamuzi yafanyike, kwa hiyo Tanzania Bara iligawanyika nusu kwa nusu kwenye jambo hilo. Hofu ya wajumbe wa Bara waliokataa maamuzi yasifanywe ilikuwa ni kuwa yakifanyika yataathiri mipango yao.

6. Majira ya saa 8 mchana wakati mkutano ukiendelea na baadhi ya wajumbe wa bara wakiomba mkutano mkuu umuite Prof. Lipumba, ndipo Profesa alipojitokeza akiwa na kundi la MABAUNSA wapatao 30 wakisindikizwa na Ofisa wa POLISI aliyekuwa na RADIO CALL (Angalia picha ya ukurasa wa mbele gazeti la Mtanzania). Kundi hilo liliwazidi nguvu walinzi wapatao 10 waliokuwa kwenye lango kuu na hivyo Prof. Lipumba akaingia mkutanoni kwa nguvu na kuketi upande mmoja na "genge" lake. Baadhi ya wajumbe wa bara wapatao 150 hivi kati ya 320 waliohudhuria walisimama na kushangilia ujio wa Lipumba kwa dakika kadhaa. Mwenyekiti wa Mkutano aliwatuliza 

7. Mwenyekiti wa Mkutano aliwajulisha wajumbe kwamba kwa hatua iliyopo lazima wafanye uamuzi aidha wa kumrejeshea uenyekiti Lipumba au kumuondoa kabisa, kwa kupiga kura. Wajumbe walewale takribani 150 wa Bara waliendelea kupinga kitendo chochote cha kupiga kura, wakitaka mkutano mkuu umuidhinishe Lipumba kurudi kwenye uenyekiti "kienyeji" na bila kutumia kura.

8. Mwenyekiti wa Mkutano alitoa OPTION ya pili kwamba Mkutano Mkuu uache ajenda ya kwanza uhamie ajenda ya pili na kufanya uchaguzi wa Makamu Mwenyekiti wa chama na ule wa wajumbe wanne wa baraza na kwamba Mjadala juu ya Lipumba uahirishwe na pia uchaguzi wa nafasi ya Mwenyekiti uahirishwe. Wajumbe wa bara walewale takribani 150 kati ya 320 walikataa OPTION hii ya pili wakasimama na kupiga makelele kuwa Lipumba arudishwe bila uamuzi wa kikatiba wa Ibara ya 112.

9. Mwenyekiti wa Mkutano Ndg. Julius Mtatiro aliuahirisha mkutano kwa zaidi ya saa moja ili wajumbe wakapate chakula. Katika muda huo wa mapumziko viongozi wa kitaifa wa CUF waliwasiliana na viongozi wa jeshi la Polisi kuanzia kanda, mkoa, wilaya ili kujua ni kwa nini polisi waliokuwepo walimruhusu na kumsindikiza Lipumba ukumbini na kutaka kujua ni kwa nini wanashindwa kumuondoa kwa sababu si mjumbe. Polisi walieleza kuwa wanao ulinzi wa kutosha hapo hotelini na kwamba mkutano ukirejea wataimarisha ulinzi na kuzuia makundi yoyote yasiyo wajumbe kuvamia mkutano kama lilivyofanya kundi la Lipumba na watu wake. Polisi walikataa katakata kumuondoa Lipumba na genge lake ukumbini.

10. Mkutano uliporejea, Mwenyekiti wa kikao aliwaongoza wajumbe kufanya maamuzi ikiwa LIPUMBA aondoke au abaki kwa mujibu wa katiba ya CUF ibara ya 117 (2). Wajumbe takribani 150 wa bara walisimama na kupinga. Wajumbe takribani 130 wa bara na wajumbe takribani 340 wa Zanzibar walipiga kura na kuamua kuwa Lipumba AONDOKE RASMI. Jumla ya wajumbe waliomuondoa Lipumba ni kwa kura zilizphesabiwa rasmi ni 476 huku waliosema ASIONDOKE wakiwa 14 tu. Wajumbe takribani 150 hususani kutoka Tanzania Bara walikataa kushiriki katika upigaji kura lakini wasingeliweza kuathiri akidi au maamuzi. Baada ya uamuzi huo muhimu na ukilishwaji wa ajenda ya kwanza, mwenyekiti wa kikao alikiahirisha kwa saa nzima.

11. Kikao kiliporejea saa 1 jioni hivi, Mkutano Mkuu ulihamia kwenye ajenda ya pili ya Uchaguzi wa Nafasi ya Mwenyekiti, Makamu Mwenyekiti na Wajumbe wanne wa Baraza. Mwenyekiti wa kikao alimkaribisha Mwenyekiti wa Uchaguzi wa ndani ya chama Wakili msomi Awadh Said akisaidiwa na Wakili msomi Job Kralio ili waongoze shughuli uchaguzi. Wakili awadh alitoa taarifa ya utangulizi akawatambulisha wajumbe wa kamati yake na wakajipanga mbele ya wajumbe.

12. Wakati Wakili Awadhi (Mwenyekiti wa Uchaguzi) akiendelea na zoezi lake, wajumbe wale 150 wa Tanzania bara walisimama wakijaribu kuzuia uchaguzi usifanyike. Mwenyekiti wa Mkutano Mkuu aliwatuliza na wakamsikiliza lakini ghafla, milango mikuu ya Blue Pearl ilivamiwa na kundi la vijana zaidi ya 200 wakitokea nje, vijana hao wavamizi ambao kwa vyovyote vile lazima walikuwa wamekodiwa kwa ajili hiyo, waliwazidi nguvu walinzi wetu wa mlangoni wakaingia ukumbini.

13. Polisi kikosi kizima waliokuwepo hawakufanya chochote baada ya hali hiyo, wameshuhudia makundi ya watu wasio wajumbe wakiingia ukumbini na wamewaacha wafanye hivyo bila kuwazuia. Viongozi wa Polisi waliokuwepo "walitorokea mlango wa pili" immediatelly baada ya kundi la wahuni kuvamia.
Kundi lile lote likawa limo ukumbini ukijumlisha na lile kundi la Lipumba na mabodigadi wake wa kukodi. Kundi jipya la wavamizi mia mbili lilianza kuleta vurumai kwa kupiga baadhi ya wajumbe wa mkutano mkuu (wajumbe kamwe hawakupigana wao kwa wao, hata mara moja, walivamiwa kutoka nje na wahuni na baadhi ya wajumbe kunyang'anywa viti na kupigwa au kutishiwa kupigwa).

14. Kutokana na hali hiyo majira hayo kwa mamlaka ya kikatiba aliyokuwa amepewa na Mkutano Mkuu, ndugu Julius Mtatiro aliahirisha Mkutano Mkuu wa CUF hadi itakapotangazwa vinginevyo. Baada ya kuuahirisha viongozi walilindwa na kuondoka mkutanoni kwa utaratibu na wajumbe wa mkutano mkuu wakaongezewa ulinzi wa hoteli ili wawe salama.

15. Kwa maoni yangu, pamoja na kuwa Prof. Lipumba ameamua rasmi kuingia vitani na chama chake tena kwa malengo halisi ya AJENDA NA MASLAHI YAKE BINAFSI, ukweli unabakia kuwa POLISI walikuwa ni sehemu ya Mkakati wa kuuvuruga mkutano wa CUF. Kama Polisi wangelitoa ulinzi kidogo tu, mkutano ungelifanyika na uchaguzi ungelifanyika hadi mwisho. Lakini USALITI wa LIPUMBA akishirikiana na VYOMBO VYA DOLA unaweza kuwa mzizi mkuu wa hali ya jana.

‪#‎Note‬ 1: Leo nimeelezea kwa kirefu nini kilitokea mkutanoni jana. Kesho ntaeleza maoni yangu binafsi kwa ujumla.
author

This post was written by: Author Name

Your description comes here!

Get Free Email Updates to your Inbox!

Post a Comment

CodeNirvana
Chediel . Powered by Blogger.
© Copyright Rundugai Blog
Back To Top